Wanahabari wajeruhiwa mkutano wa Linda Mwananchi Homa Bay
WAANDISHI wawili wa habari walijeruhiwa na biashara kusitishwa katika Mji wa Homa Bay Jumapili huku mvutano ukizuka kabla ya mkutano wa Linda Mwananchi. Waandishi wa AFP Fred Ooko na Brian Ongoro walishambuliwa karibu saa tatu asubuhi walipokuwa wakiripoti matukio katika mji huo. Wawili hao walisema walivamiwa na kundi la watu waliokuwa na silaha za kienyeji. Vitambulisho vyao vya kazi, leseni za udereva, kamera na mali nyingine zilichukuliwa. Bw Ooko alisema alibururwa barabarani na kupigwa kwa marungu kabla ya mhudumu wa bodaboda aliyemfahamu kuingilia kati na kumsaidia kutoroka hadi Olare. "Mwenzangu Brian Ongoro pia alipigwa. Alipoteza simu na kamera. Leseni yangu, kitambulisho cha kazi na vitu vingine vilichukuliwa," akasema. [caption id="attachment_191227" align="alignnone" width="1600"] Vioo vya magari vilivyovunjwa vyatapakaa katika barabara za Homa Bay wakati wahuni walipokabili msafara wa Linda Mwananchi. Picha|George Odiwuor[/caption] Mji wa Homa Bay ulikuwa kama eneo lisiloweza kufikika baada ya vijana kufunga barabara kadhaa kwa mawe na magogo, huku wengine wakiwasha moto. Biashara zilisitishwa huku maduka na baadhi ya maeneo ya ibada yakifungwa. Msafara wa Linda Mwananchi uliokuwa ukielekea Homa Bay ulilazimika kubadili njia baada ya baadhi ya barabara kuzuiwa. Polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji na kufungua barabara. Hapo awali, polisi walikamata washukiwa 15 wa genge la uhalifu katika Kaunti ya Kisumu na kuwapokonya mapanga, visu, kamba, marungu na silaha nyingine. Polisi walisema washukiwa hao walikuwa wakielekea Homa Bay kwa magari matatu. Mmoja wao, Oliver Jaoko almaarufu Oliveti, anadaiwa kuwa kiongozi wa kundi hilo lakini alitoroka wakati wa operesheni. Washukiwa hao 15 wamewekwa chini ya ulinzi wakisubiri kufikishwa mahakamani.