WIRE โ CHAMA cha Wiper Patriotic Front (WPF) kimeunda kikosi cha viongozi watatu kuongoza kampeni zake eneo la Pwani huku kinyang'anyiro cha kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kikishika kasi. Kikosi hicho kinajumuisha Mbunge wa Nyali Mohammed Ali, Mbunge wa Wundanyi Danson Mwashako na aliyekuwa Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa. Viongozi hao wanawakilisha maeneo yenye ushawishi mkubwa kisiasa ya Mombasa, Taita Taveta na Kilifi. Hii ni katika hatua ambayo kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka amesema inalenga kuimarisha upinzani na kuteka Pwani kama ngome yake. Hatua hiyo imeongeza ushindani Pwani ambako washirika wa Rais William Ruto wanajaribu kuunganisha magavana, wabunge na viongozi wengine chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza ili kudhibiti kura za eneo hilo. Kwa upande wa upinzani, viongozi hao watatu wanatarajiwa kusuka mtandao wa kisiasa utakaosaidia kukabili ushawishi unaoongezeka wa muungano tawala Kenya Kwanza, na kuzuia Pwani kuwa eneo linaloegemea upande mmoja wa kisiasa. Akizungumza akiwa Kakuyuni, Kaunti ya Kilifi, wakati wa kumpokea rasmi Jumwa katika chama cha Wiper Patriotic Front (WPF), kinara Musyoka alipendekeza achaguliwe kuwa naibu kiongozi wa chama hicho. Alisema tajriba ya Jumwa katika siasa, pamoja na ushawishi wa Mohammed Ali na Mwashako, zitaipa Wiper nguvu mpya Pwani na kusaidia upinzani kujenga kampeni imara. "Jumwa amepanda ngazi za uongozi kutoka Mwakilishi wa Wanawake, Mbunge hadi Waziri. Sasa nawaomba mnipe Jumwa ili twende pamoja kukomboa nchi hii. Nitampa tiketi ya chama kugombea ugavana na pia nataka awe katika siasa za kitaifa. Kama kiongozi wa WPF, napendekeza awe naibu kiongozi wa chama," alisema Kalonzo. Aidha, alidai kwamba mazingira ya kisiasa Pwani yanabadilika na kwamba Wiper inaelekea kuchukua nafasi iliyoshikiliwa na ODM kama chama kikuu cha upinzani katika eneo hilo. "Ninatangaza kuwa ngome iliyokuwa ya ODM sasa ni ya Wiper," akasema. Kalonzo alikumbusha wakazi wa Pwani kuhusu ushirikiano wake wa muda mrefu na kinara wa zamani wa ODM Raila Odinga katika harakati za kukuza demokrasia na haki za kijamii. Kwa upande wake, Ali alisema viongozi hao watatu wataanzisha kampeni kubwa ya hamasisho kuanzia Lamu hadi Taita Taveta na Lunga Lunga ili kuwashawishi wananchi kuunga mkono Kalonzo na upinzani. "Bi Jumwa na mimi ni kama Ronaldo na Messi. Kuanzia Lamu hadi Taita-Taveta na Lunga Lunga, tutaondoa serikali hii mamlakani," alisema. Alishutumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kuwasahau baadhi ya viongozi walioisaidia kupata ushawishi katika Pwani. Kulingana naye, hatua ya Jumwa kuondoka UDA ni ishara ya kutoridhika miongoni mwa baadhi ya washirika wa zamani wa serikali. Naye Mwashako, ambaye anatazamiwa kuwania ugavana Taita-Taveta mwaka 2027, alisema amesalia Wiper licha ya kushinikizwa kujiunga na serikali. Alifichua kuwa amekuwa akishawishiwa mara kwa mara kujiunga na serikali jumuishi, ikiwemo kuahidiwa msaada wa kifedha kwa azma yake ya kugombea ugavana. "Nilichaguliwa kupitia Wiper mwaka 2017 na chama hiki ni nyumbani kwangu. Wamekuwa wakinishawishi mchana na usiku nijiunge na serikali lakini nimekataa. Hata walinitishia lakini sikuyumba," alisema. Mwashako pia alifichua kuwa alijiuzulu kama mwenyekiti wa Kikundi cha Wabunge wa Pwani mwezi Januari baada ya kudaiwa kuambiwa kwamba angeendelea kushikilia nafasi hiyo tu ikiwa angeondoka Wiper. ย "Hata pesa zao nilikataa. Nilikuwa mwenyekiti wa kikundi hicho kwa miaka mitatu lakini nikajiuzulu kwa sababu ya shinikizo. Niliambiwa lazima nitoke Wiper ili nibaki katika nafasi hiyo," alisema. Kauli yake imeonyesha ushindani mkubwa unaoendelea nyuma ya pazia huku kila upande ukijaribu kuvutia viongozi wenye ushawishi eneo la Pwani kabla ya uchaguzi wa 2027. Mwashako alisema upinzani hautaruhusu viongozi wake kuvutwa kwa ahadi za nyadhifa serikalini au fedha. ย "Kenya ni nchi ya kidemokrasia na hakuna mtu anayepaswa kulazimishwa kujiunga na serikali," alisema. Mbunge huyo wa Wundanyi alisema hatua ya Jumwa kujiunga na Wiper imepatia upinzani nguvu mpya Pwani na kwamba sasa viongozi hao watatu watashirikiana kuhamasisha wapigakura katika kaunti zote sita za eneo hilo. "Kwa sasa tuko watatu; mimi, Jumwa na ndugu yangu Mohammed Ali. Kazi yetu ni kuwashawishi wananchi wasivutiwe na pesa ili kuunga mkono serikali," alisema. Kuundwa kwa timu hiyo kunajiri huku viongozi wa Kenya Kwanza nao wakiongeza juhudi za kuimarisha ushawishi wao katika eneo la Pwani. Mohammed Ali tayari ametajwa na viongozi wa upinzani kama mmoja wa wanaoweza kuwania ugavana wa Mombasa mwaka 2027, hatua inayomfanya kuwa miongoni mwa nyuso kuu za upinzani katika eneo hilo. Mwashako alisema ana imani viongozi wengine watajiunga na kundi hilo kadri kampeni zinavyoendelea. "Kwa sasa tuko watatu lakini nina uhakika wengine watajiunga nasi. Tuna Mohammed Ali, Shakila Abdalla kule Lamu, mimi Taita-Taveta na wengine Tana River na Kwale. Lakini lengo kuu ni kuhakikisha Kalonzo Musyoka anashinda urais mwaka 2027," alisema. Bi Jumwa aliwasihi wakazi wa Pwani kujifunza kutoka kwa wapigakura wa Ol-Kalou ambao, kwa mujibu wake, walipokea miradi na fedha za serikali lakini bado wakachagua mgombea wa upinzani. Aliwaonya kwamba serikali itatumia rasilimali nyingi kabla ya uchaguzi wa 2027 lakini akawasihi wapigakura kutoruhusu ahadi na zawadi za kampeni kuathiri maamuzi yao. Alisema wananchi wanaweza kupokea maendeleo na manufaa yanayoletwa kwao, lakini watumie haki yao ya kidemokrasia kwa uhuru wakati wa kupiga kura.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.