WIRE โ KWA miaka mingi, bonasi ya chai imekuwa ikichukuliwa na wakulima wadogo kama kipimo cha mafanikio yao shambani. Malipo makubwa ya mwisho wa mwaka yamekuwa yakitafsiriwa kuwa ushahidi wa uzalishaji mzuri, bei nzuri za chai na usimamizi bora wa viwanda. Hata hivyo, ukaguzi uliofanywa na Bodi ya Chai Kenya umefichua ukweli tofauti. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa katika baadhi ya viwanda, sehemu ya bonasi iliyolipwa wakulima haikutokana na mapato ya mauzo ya chai bali ilitokana na mikopo kutoka benki za kibiashara. Kwa maneno mengine, baadhi ya wakulima walilipwa kile kilichoonekana kuwa bonasi ilhali fedha hizo zilikuwa mikopo ambayo baadaye ilibaki kama deni la kiwanda. Madeni hayo sasa yanapaswa kulipwa kutoka kwa mapato ya baadaye ya wakulima hao hao. Ripoti ya Machi 2026 iliyoandaliwa baada ya agizo la Wizara ya Kilimo inaonyesha kuwa kufikia Desemba 31, 2025, viwanda 69 vya chai vilikuwa na madeni ya jumla ya Sh34.05 bilioni. Kati ya fedha hizo, Sh30.36 bilioni zilikuwa mikopo iliyochukuliwa kwa jina la kufadhili shughuli za chai na bonasi za wakulima. Sekta ya chai ni muhimu sana nchini Kenya. Viwanda 71 vya wakulima wadogo vinamilikiwa na zaidi ya wakulima 650,000 na huzalisha zaidi ya nusu ya chai yote nchini. Mwaka 2025, sekta hiyo ilileta zaidi ya Sh215 bilioni. Lakini sasa baadhi ya viwanda vinakabiliwa na mzigo mkubwa wa madeni. Ripoti ya ukaguzi imeonya kuwa uwezo wa baadhi ya viwanda kuendelea kufanya kazi uko mashakani kutokana na kiwango kikubwa cha madeni. Kiwanda cha Kapkoros kiliongoza kwa kuwa na deni la Sh2.77 bilioni, kikifuatiwa na Litein na deni la Sh1.88 bilioni, Mogogosiek Sh1.60 bilioni na Kapset Sh1.48 bilioni. Wakaguzi walibaini kuwa katika kipindi cha miezi sita hadi Desemba 2025, kampuni ya KTDA Management Services iliratibu mikopo ya mabilioni ya fedha kupitia benki mbalimbali kwa viwanda 55 ili kufadhili malipo ya pili ya wakulima. Jumla ya Sh30.47 bilioni zilichukuliwa kutoka benki mbalimbali. Hata hivyo, mahitaji halisi ya viwanda kwa ajili ya bonasi na malipo mengine yalikuwa Sh25.29 bilioni pekee. Hivyo, wakaguzi hawakuweza kueleza sababu ya kukopa Sh5 bilioni zaidi. Ripoti hiyo pia imeibua maswali kuhusu jinsi fedha hizo zilivyotumiwa. Imebainika kwamba sehemu ya mikopo iliyochukuliwa kwa jina la bonasi ilitumika pia kulipa madeni ya zamani gharama za uendeshaji wa viwanda na mikopo mingine iliyokuwepo awali. Matokeo yake ni kwamba baadhi ya wakulima waliamini walikuwa wanapokea faida kutokana na mauzo ya chai ilhali fedha walizopokea zilikuwa sehemu ya mikopo. Ukaguzi huo pia umebaini udhaifu mkubwa katika usimamizi wa mikopo. Katika baadhi ya viwanda, bodi za wakurugenzi ziliidhinisha mikopo bila kutaja kiwango kinachopaswa kukopwa. Katika visa vingine, viwanda vilikopa zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa. Tatizo jingine lilihusisha tathmini ya thamani ya chai iliyokuwa bado haijauzwa. Wakaguzi waligundua kuwa baadhi ya viwanda viliongeza thamani ya chai hiyo kwa kiwango kikubwa kuliko bei halisi ya soko. Hatua hiyo iliviwezesha kukopa fedha nyingi zaidi na kutangaza bonasi kubwa kuliko uwezo wao wa kifedha. Bodi ya Chai sasa inapendekeza kuwa malipo ya bonasi yajayo yawe yanategemea mapato halisi na fedha zilizopo, badala ya mikopo na makadirio yaliyopandishwa ya thamani ya chai. Kwa wakulima, funzo kuu kutoka kwa ripoti hiyo ni kwamba bonasi kubwa si lazima iwe ishara ya mwaka mzuri wa biashara. Wakati mwingine inaweza kuwa fedha za mkopo ambazo baadaye hulipwa kupitia mapato yao ya siku zijazo.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.