WIRE โ€” WAKULIMA wa miradi midogo ya ng'ombe wa maziwa watanufaika na mpango mpya wa kidijitali unaolenga kuwasaidia kupata huduma za kifedha, masoko rasmi na mikopo nafuu kwa kujenga rekodi za miamala za ukopaji zinazoweza kuthibitishwa. Farmer Visibility Project, ni mradi uliozinduliwa na Heifer International Kenya kwa ushirikiano na Mastercard, KCB Foundation na KCB Bank Kenya, na unalenga kuangazia changamoto za muda mrefu zinazokabili wakulima wa maziwa, zikiwemo biashara za fedha taslimu, ukosefu wa rekodi bora na ugumu wa kupata fedha. "Mpango huu wa majaribio wa miezi tisa unalenga wakulima wadogo 30,000 wa maziwa kote nchini na unatarajiwa kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kwa kuweka kidijitali uwasilishaji wa maziwa, malipo, akiba na ununuzi wa pembejeo," alisema Mkurugenzi wa Heifer International Kenya, Wairimu Munyinyi-Wahome, wakati wa uzinduzi wa mpango huo Nairobi. Kulingana na Wairimu, wakulima wengi wa maziwa kwa sasa hutegemea miamala (transactions) isiyo rasmi, hali inayofanya iwe vigumu kwao kuonyesha historia ya kifedha inayohitajika na taasisi zinazotoa mikopo. Alisema kucheleweshwa kwa malipo ya maziwa na changamoto za fedha katika vyama vya ushirika pia zimewalazimu wazalishaji wengi kuuza maziwa kupitia njia zisizo rasmi, hali inayopunguza uwazi na kuwanyima fursa ya kupata masoko rasmi yanayolipa vizuri. Chini ya mradi huo, wakulima na vyama vyao vya ushirika watapewa mafunzo kuhusu matumizi ya teknolojia za kidijitali na elimu ya kifedha. Hali kadhalika, watasaidiwa kufungua akaunti za benki na kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali. [caption id="attachment_191120" align="aligncenter" width="300"] Mkulima akikama maziwa. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mpango huo unatarajiwa kuwezesha wakulima kujenga rekodi za kuaminika za miamala ambazo taasisi za kifedha zinaweza kutumia kuunda bidhaa zinazokidhi mizunguko ya uzalishaji na mahitaji ya fedha ya wakulima wa maziwa. Wairimu alisema mpango huo umeundwa kufanya wakulima waonekane zaidi katika mfumo wa kifedha na kutambuliwa kama wajasiriamali wanaoendesha biashara zinazoweza kuleta faida. "Wakulima wadogo ni wajasiriamali. Ni wamiliki wa biashara, wasambazaji, waajiri na wawekezaji katika jamii zao. Hata hivyo, wengi wao bado hawaonekani katika mifumo ya kifedha na masoko ambayo inaweza kuwasaidia kukua," alisema. Alidokeza kuwa mradi huo utawapa wakulima uwezo mkubwa wa kudhibiti data zao za biashara na kuwaunganisha na huduma za kifedha, masoko na fursa za kiuchumi. Chini ya ushirikiano huo, Mastercard inafadhili Heifer International Kenya kama mshirika mkuu wa utekelezaji, huku KCB Foundation na KCB Bank Kenya zikiwa washirika wa utekelezaji. Mastercard itatoa teknolojia yake ya Farm Pass kupitia jukwaa la Community Pass, litakalosaidia kuunda wasifu wa kidijitali wa wakulima, kufuatilia miamala na kuimarisha uhusiano katika mnyororo wa thamani, ikiwemo maeneo ya vijijini yenye upatikanaji mdogo wa huduma za kidijitali. Makamu Mkuu wa Rais wa Mastercard na Meneja wa Nchi za Afrika Mashariki na Visiwa vya Bahari ya Hindi, Shehryar Ali, alisema kuweka miamala ya wakulima katika mfumo wa kidijitali kutaimarisha ufuatiliaji na ujumuishaji wa kifedha. "Kwa uwekezaji wetu na matumizi ya suluhisho la Farm Pass, miamala ya wakulima itawekwa kidijitali, ufuatiliaji wake utaimarishwa na upatikanaji wa malipo na huduma za kifedha kurahisishwa," alisema. [caption id="attachment_191121" align="aligncenter" width="300"] Maziwa kwenye ndoo tayari kupelekwa sokoni. Picha|Sammy Waweru[/caption] Jukwaa hilo pia litawezesha malipo ya kidijitali, utoaji wa kadi na ununuzi wa pembejeo kupitia ushirikiano na taasisi za kifedha kama vile KCB Bank, huku wakulima wakijenga rekodi za kifedha zinazoaminika. KCB Foundation itasimamia uhamasishaji wa wakulima, kuimarisha vyama vya ushirika, kujenga uwezo, mafunzo ya elimu ya kifedha, ufuatiliaji na uratibu wa mradi. KCB Bank Kenya itawezesha wakulima kufungua akaunti, kutumia huduma za malipo ya kidijitali na kupata kadi, huku ikisaidia wafanyabiashara na mawakala kupokea malipo kwa njia ya kidijitali. Mkurugenzi Mkuu wa KCB Foundation, Mendi Njonjo, alisema ushirikiano huo unachanganya teknolojia na ujumuishaji wa kifedha ili kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa nchini. "Maendeleo endelevu ya jamii huanza kwa kuunda majukwaa yanayowawezesha watu kushiriki kikamilifu katika uchumi," alisema. Aliongeza kuwa mpango huo utasaidia wakulima kujenga biashara zinazostahimili misukosuko, kuongeza uzalishaji na kuboresha mapato ya jamii. Mradi huo unalenga kubadilisha mfumo wa malipo ya maziwa, kuimarisha vyama vya ushirika na kupanua huduma za kifedha za kidijitali katika sekta ya maziwa nchini iwapo utaenezwa kote nchini Kenya.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.