WIRE โ€” PUNDE tu baada ya mkewe kujifungua, David Omollo alijikuta kati ya furaha na wasiwasi. Mkewe alijifungua ujauzito ukiwa na miezi saba badala ya muda wa kawaida wa miezi tisa.Hali hiyo ilichangiwa na uvimbe aliokuwa nao kwenye kizazi wa fibroids. "Mke wangu alijifungua salama sana bila kufanyiwa upasuaji lakini kwa sababu tulimpata mtoto kabla ya muda, muuguzi alisema kuwa anastahili kuwekwa kwenye incubator. Hata hivyo, nilikataa jambo hilo. Nilitaka kumlinda mwanangu nje ya hospitali," anasimulia mzazi huyo. Usimamizi wa hospitali hatimaye uliitikia wito wa David na kumshauri kufanya mpango wa Kangaroo Mother Care (KMC)ambapo ngozi zinatagusana. "Nilionyeshwa jinsi ya kuufanya mpango huo. Nilichukua likizo ya wiki mbili kazini na kutumia fursa hiyo kumweka mtoto wangu kwenye kifua wakati wote huku mke wangu alipokuwa akiendelea kupona. Usiku tulikuwa tukisaidiana. Nilikuwa baba mwenye furaha sana," anaeleza kwa tabasamu. Kwa pamoja, anasema kuwa walimfanyia mwanao mpango huo wa KMC katika kipindi cha miezi sita mfululizo. Wakati huo, David anasema kuwa mtoto wao alikuwa ameonyesha ishara za kuwa mchangamfu na kuwa na uwezo wa kula vyakula vingine kando na maziwa. "Mtoto wetu alipofikisha umri wa miezi mitano, tulianza kumlisha aina tofauti ya vyakula. Uzuri ni kuwa hakuwa akisumbua kula, alipenda kula vizuri. Pia alikuwa akilala vizuri sana kwenye kifua na hata kitandani tulipomaliza mpango wa Kangaroo," David anasimulia. Ili kufanya mpango wa KMC, mzazi anahitaji kiti au kitanda ambacho anaweza kukalia kwa muda mrefu sana bila kuchoka au kuhisi maumivu. Mzazi anayefanya mpango huu, anastahili kutoka tu kwenye kiti au kitanda hicho anapoenda msalaani. Mtoto anastahili kuvuliwa nguo na kuvalishwa tu kofia, nepi na soksi kisha mtoto anawekwa wima katikati ya matiti kisha anafunikwa na shuka iliyo na joto la kutosha kumzuia mtoto kupata baridi. Haya ni kwa mujibu wa muuguzi anayesimamia kitengo cha watoto walio chini ya umri wa mwezi moja katika hospitali ya Aga Khan University, Joyce Njoki Wanjohi. "Mpango wa Kangaroo Mother Care unashauriwa pindi tu mtoto anapozaliwa. Mtoto anastahili kuwekwa wima kwenye kifua cha mama bila nguo. Unastahili kuwa kwa muda wa kati ya saa 20-24 mfululizo lakini kutokana na sababu tofauti, baadhi ya wazazi hawawezi timiza muda huo. Hivyo hata dakika 60-90 kila siku bado zina faida," anaeleza muuguzi huyo. Lakini je, ni sayansi gani iliyo chini ya mpango wa KMC? "Kuna uhamisho wa bakteria zilizo na kinga kutoka kwenye ngozi ya mama au baba wa mtoto ambazo ni salama zinapohamishwa kwenye ngozi ya mtoto zinafanya kazi ya kumkinga mtoto. Hivyo, watoto wengi wanapofanyiwa mpango huu huwa hawapati maambukizi makali wakilinganishwa na wenzao ambao hawajawekwa kwenye mpango huo," anaeleza muuguzi. Mpango huo anasema kuwa una manufaa mengi yanayohusiana na ukuaji wa ubongo na mwili kwa kusaidia sana ustawi wa mtoto. Pia unapunguza msongo wa mawazo miongoni mwa watoto. "Kunakuwa na ubora wa mtoto anavyokuwa kiuzito, urefu na pia mzingo wa kichwa jambo ambalo ni muhimu sana likiboreshwa miongoni mwa watoto wa njiti. Pia kunakuwa na kinga bora na kupunguza maambukizi makali," anasema Bi Joyce. Aidha anaeleza kuwa mpango wa KMC huongeza unyonyeshaji. "Punde tu mtoto anapowekwa kwenye titi, mpango huo hufanya miujiza kwa sababu kunakuwa na uzalishaji wa homoni ya oksitosin inayosaidia mtiririko wa maziwa. Mara nyingi unaona mama anapomshikilia mtoto na maziwa yanatiririka kwa sababu kuna uhusiano kati ya mama na mtoto," anaeleza. Licha ya kuwa mpango wa KMC kwa kiasi kikubwa unafanywa na kina mama, muuguzi huyo anasema kuwa, kina baba pia wanashauriwa kuufanya. "Kumshika mtoto wako kuna faida kadhaa na hivyo unahisi mtoto wako si mgonjwa sana. Pia kunakuwa na ushirikiano bora kati ya mtoto na mzazi. Wakati uo huo, mzazi anakuwa na matumaini kwa sababu yeye pia ni miongoni mwa wanaomtunza mtoto. Anapoona mabadiliko kwenye afya ya mtoto, anapiga ripoti kwa wahudumu wa afya," anaeleza. Mpango wa Kangaroo Mother Care unafanywa katika kiwango kikubwa kwenye mazingira ya hospitali ambapo mama wa mtoto anakusudiwa kutokuwa na kazi yoyote ya kufanya isipokuwa kumlea mtoto. Hata hivyo, muuguzi huyo anasema kuwa watoto walio na uzani wa chini wanaporuhusiwa kutoka kwenye hospitali haswa zile za umma, wakiwa na kilo 1.8, wazazi wao hushauriwa kuendelea kuwafanyia mpango huo kwa muda mrefu kulingana na uwezo wao wakiwa nyumbani. "Hospitali tofauti za umma, zina vyumba vya Kangaroo Mother Care ambapo akina mama hukaa, kula na kuwa na wanao muda wa saa 24 kila siku. Pia kunahimizwa kuwa mzazi wa kiume aende hospitalini na kumsaidia mama," anasema. Mpango huo unatumika pakubwa nchini Kenya haswa katika hospitali za umma. Kulingana na UNICEF, mpango huu wa KMC, ulibuniwa katika nchi ya Colombia kuwasaidia watoto wa njiti kukuwa wakati ambapo vifaa vya kuwalelea havikuwepo au vilikuwa vichache. "Tafiti nyingi za kisayansi zinaonyesha kuwa Kangaroo Mother Care ni bora zaidi kuliko mtoto anapowekwa kwenye incubator. Mpango huu umedhihirisha kuwa muhimu sana na ulio na faida kwa mtoto," muuguzi anaeleza. Kulingana na data kutoka shirika la Afya Duniani, WHO, kufikia mwaka wa 2024, kulikuwa na asilimia 17.2 ya vifo katika kila watoto 1000 waliozaliwa. Watoto kuzaliwa kabla ya miezi tisa ya ujauzito, maambukizi ya watoto walio chini ya siku 28 na matatizo wakati wa uzazi ni miongoni mwa sababu za vifo katika kipindi hicho kote duniani. "Kiwango cha vifo vya watoto wachanga sana nchini Kenya ni vifo 21 katika kila watoto 1000 wanaozaliwa. Mara nyingi, vifo hivi hutokea katika kipindi cha siku 28 za mtoto kuzaliwa. Ni muhimu sana kwetu kuukumbatia mpango wa Kangaroo Mother Care kwa sababu umeonyesha kuwa na faida kadhaa," anashauri Bi Joyce. Kwa baba huyo, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 54, japo mkewe aliaga dunia miezi tisa tu baada ya kujifungua, anasema kuwa mpango wa Kangaroo Mother Care ulimuokoa mwanae ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 18. "Kangaroo Mother Care ilimuokoa mwanangu. Japokuwa yeye ni mtoto wa njiti, ni kijana hodari aliye na nguvu na anapenda kazi zinazohitaji nguvu nyingi. Mwaka huu atajiunga na chuo anuai kusomea kozi ya ujenzi," anasema mzazi huyo wa watoto wanne.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.