WIRE โ€” WANASIASA waliochaguliwa katika eneo la Mlima Kenya wanaoanza kujitenga na Chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto na kujiunga na Democracy for Citizens Party (DCP) wanakabiliwa na mtihani mpya wa kisiasa. DCP, chini ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kimeweka wazi kuwa kujiunga na chama hicho hakumaanishi mwanasiasa atapewa tiketi moja kwa moja kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa 2027. Onyo hilo linajiri baada ya ushindi wa DCP katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou mnamo Julai 16, ambapo mgombea wa chama hicho Kamau Ngotho alimshinda Muchina Nyaga wa UDA kwa zaidi ya kura 30,000. Ushindi huo umechochea kuhama kwa baadhi ya wanasiasa kutoka UDA na vyama vingine, huku Jubilee na The Service Party cha Mbunge wa Laikipia East Mwangi Kiunjuri pia vikikumbwa na misukosuko hiyo ya kisiasa. Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa DCP John Methu amesema chama hicho kitakuwa makini katika kuwapokea wanasiasa wanaotafuta hifadhi ya kisiasa ndani yake. "Ikiwa ulipigia UDA kampeni Ol Kalou na ulikuwepo katika eneo bunge hilo siku ya kupiga kura, tafadhali usijaribu hata kukaribia DCP," alisema Bw Methu. Pia aliwaonya viongozi ambao walinyamaza wakati wakazi wa Mlima Kenya walidaiwa kutukanwa katika mikutano ya kisiasa. "Ikiwa ulihudhuria mikutano ambako watu wa Mlima Kenya walidhalilishwa na kutukanwa na hukupaza sauti kupinga, jichukulie kuwa hutakiwi DCP," alisema. Bw Methu alisema wale waliounga mkono kuondolewa kwa Bw Gachagua katika wadhifa wa Naibu Rais mnamo 2024 hawataadhibiwa moja kwa moja, akisema kiongozi huyo amewasamehe. Hata hivyo, aliongeza kuwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujiunga na DCP watalazimika kupigania tiketi za chama hicho kupitia kura za mchujo badala ya kupewa tiketi moja kwa moja. Kwa sasa, Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha ndiye kiongozi mashuhuri zaidi aliyepokelewa rasmi na DCP. Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata pia ameonyesha anaelekea DCP, ingawa wakati huo huo anajihusisha na kundi la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna. Mchanganuzi wa siasa Malila Munywoki, hata hivyo, amewatahadharisha wanasiasa wanaohama UDA dhidi ya kudhani kuwa DCP itawapa usalama wa kisiasa. "Nchini Kenya, vyama vya kisiasa vinamilikiwa na watu na kujiunga navyo si haki bali ni fursa unayopewa," alisema. Alisema DCP ilianzishwa kwa msingi wa upinzani dhidi ya Bw Ruto na kwamba, wafuasi wake huenda wasikubali kwa urahisi viongozi wanaohusishwa na utawala wa Kenya Kwanza. Seneta wa Murang'a Joe Nyutu alithibitisha kuwa baadhi ya maafisa wakuu serikalini kutoka Mlima Kenya, Nairobi na Bonde la Ufa wameonyesha nia ya kujiunga na DCP. "Tusubiri kiongozi wa chama chetu atangaze majina makubwa kwa wakati wake," alisema. Bw Kiunjuri, hata hivyo, alikanusha madai kwamba maafisa wakuu serikalini wanajiandaa kuhamia DCP, akimtaja Bw Gachagua kama mwanasiasa mwenye ujuzi mkubwa wa propaganda. Bw Gachagua ameendelea kusisitiza kuwa juhudi zake za kuunganisha Mlima Kenya dhidi ya Bw Ruto zinaendelea vizuri. Alisema baadhi ya maafisa wakuu serikalini wanabaki humo kwa sababu za riziki huku kwa siri wakiunga mkono mipango yake ya kisiasa kuelekea 2027. "Tumekubaliana wabaki serikalini kwa sababu ya kujitafutia unga. Lakini wataendelea kutusaidia kutekeleza ajenda yetu ya 2027," alisema. Alisema upinzani hatimaye utakubaliana kuhusu mgombea mmoja wa urais wa kukabiliana na Bw Ruto.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.