WIRE โ HATUA ya Rais William Ruto kuanzisha mpango mpya wa maendeleo ya muda mrefu imeibua mjadala mkali wa kisiasa huku wakosoaji wakihoji kwa nini Kenya inapanga hadi mwaka 2060 kabla ya kutoa tathmini kamili ya yaliyofanyika chini ya Ruwaza ya 2030. Mzozo huo umeibuka baada ya kuzinduliwa kwa Mazungumzo ya Kitaifa kuhusu Mustakabali wa Kenya baada ya Ruwaza ya 2030, yanayolenga kuwashirikisha Wakenya katika kuamua vipaumbele vya maendeleo baada ya mpango huo wa sasa kufikia mwisho wake. Viongozi wa Kenya Kwanza wanatetea mpango huo wakisema unalenga kuhakikisha maendeleo ya nchi hayaongozwi na vipindi vya uchaguzi bali mipango ya muda mrefu inayoweza kuendelezwa na serikali zinazofuata. Hata hivyo, wapinzani wanasema Serikali inapaswa kwanza kuwaeleza Wakenya kilichofanikiwa, kilichoshindikana na kilichosalia chini ya Ruwaza 2030. Naibu mwenyekiti wa Wiper Patriotic Front na Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior, alihoji muda wa kuanzishwa kwa mpango huo akisema mamilioni ya Wakenya wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi ya kila siku. "Hatutaki mpango wa 2060. Wakenya wengi hawajui watakula nini kesho, na vijana wengi wamepoteza matumaini. Hatuwezi kuwa tunazungumzia Ruwaza ya 2060 katika hali kama hii," alisema Bw Kilonzo. Mbunge wa Tetu, Bw Geoffrey Wandeto, alisema Serikali lazima kwanza ikabiliane na ufisadi ambao unaweza kuharibu mpango wowote wa maendeleo. "Tusiposhughulikia hatari kuu, yaani ufisadi, utakula Ruwaza ya 2030, Ruwaza ya 2060 na Ruwaza ya 2100 kama kiamsha kinywa," alisema Bw Wandeto. Mbunge huyo pia alihoji iwapo Serikali imefanya tathmini ya kina ya Ruwaza ya 2030 ili kubaini yaliyofanikiwa na yaliyoshindikana. "Bado sijaona tathmini yoyote kubwa ya Ruwaza ya 2030. Nini kilifanyika vizuri? Nini kilikwenda vibaya? Nini kinaweza kuboreshwa? Tunaweza kuokoa nini?" aliuliza. Mwanasheria Harrison Kinyanjui, pia ameibua maswali kuhusu kwa nini mpango huo umepewa jina la Ruwaza ya 2060 badala ya Ruwaza ya 2050. Amedai huenda muda huo ukawa umechaguliwa kwa kuzingatia ajenda ya maendeleo ya Muungano wa Afrika ya mwaka 2063. Pia ameibua hofu kwamba mpango huo unaweza kutumiwa baadaye kufungua njia ya kubadilisha Katiba, ingawa hakutoa ushahidi wa kuonyesha kuwa Serikali ina mpango huo. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Watumiaji Kenya (Cofek), Bw Stephen Mutoro, alionya dhidi ya jaribio lolote la kutumia mpango wa maendeleo kama sababu ya kubadilisha Katiba. "Wanaofikiria wanaweza kubadilisha Katiba na kuweka 'ruwaza ya lazima' wanaota ndoto za mchana," alisema Bw Mutoro. Upinzani pia umepinga wazo la kuanzisha ahadi nyingine kubwa ya maendeleo ilhali Ruwaza ya 2030 bado haijakamilika. Msemaji wa Wiper Patriotic Front, Bw Ndegwa Njiru, alisema Kenya inahitaji kwanza tathmini ya kweli ya mafanikio na kushindwa kwa Ruwaza ya 2030. "Kenya haihitaji ahadi nyingine kubwa wakati ahadi zilizotolewa kwa wananchi bado hazijatimizwa kwa kiwango kikubwa," alisema Bw Njiru. Hata hivyo, viongozi wa Kenya Kwanza wamepuuza ukosoaji huo wakisema mipango ya taifa haipaswi kuongozwa na kalenda ya uchaguzi. Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei, alisema Ruwaza ya 2030 yenyewe iliandaliwa kupitia ushirikishaji wa wananchi. "Katika chama chetu, tunaangalia vizazi vitakavyokuja kesho, wala hatufikirii siasa za mwaka ujao," alisema Seneta Cherargei. Mbunge wa Aldai, Bi Marianne Kitany, pia alitetea muda wa kuanzishwa kwa mpango huo akisema kazi ya Ruwaza ya 2030 ilianza wakati wa utawala wa Rais mstaafu Mwai Kibaki. Wakati huohuo, wabunge wanaomuunga mkono aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wameanzisha mashambulizi mapya dhidi ya Serikali ya Rais Ruto. Seneta wa Nyandarua, Bw John Methu alisema Wakenya wameonyesha kutoridhishwa na utendaji wa Serikali katika kipindi cha miaka minne. Alitaja gharama ya maisha, kodi, ukosefu wa ajira na deni la taifa kuwa miongoni mwa masuala yanayowasumbua Wakenya.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.