WIRE โ LICHA ya shinikizo linaloongezeka la kupunguza gharama za ufugaji na kuhakikisha upatikanaji wa malighafi ya chakula cha mifugo, wataalamu wanasema taarifa potovu, changamoto za sera na kutokuwepo kwa uwiano katika kanuni zinaendelea kuchelewesha matumizi ya teknolojia ya kibayoteknolojia katika kilimo nchini Kenya na Afrika kwa jumla. Wanasema kushughulikia vikwazo hivyo ni muhimu katika kuboresha uzalishaji wa chakula cha mifugo, kupunguza gharama na kuimarisha usalama wa chakula. Mkurugenzi wa ISAAA AfriCenter, Dkt Margaret Karembu, anasema upatikanaji wa malighafi bora na nafuu ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokabili sekta ya chakula cha mifugo nchini Kenya. Anasema nchi nyingi zinazoongoza katika uzalishaji wa mifugo zimekubali matumizi ya malighafi ya chakula cha mifugo zinazotokana na mfumo wa bayoteknolojia, hasa mahindi na soya, hatua inayozisaidia kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha mifugo kwa bei nafuu. Kulingana na Dkt Karembu, zaidi ya asilimia 80 ya mahindi na soya zinazouzwa katika soko la kimataifa kwa ajili ya chakula cha mifugo hutokana na bayoteknolojia. Hata hivyo, nchi nyingi za Afrika bado zinakabiliwa na changamoto za kupata bidhaa hizo kutokana na kutokuwa na uhakika wa sera na vikwazo vya kisheria. "Ikiwa Kenya na Afrika zinataka sekta ya mifugo zenye ushindani mkuu, ni lazima tufungue masoko yetu kwa malighafi ya chakula cha mifugo zilizo nafuu, salama na bora, huku tukiwekeza katika utafiti wetu wa kibayoteknolojia ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje," alisema. Alisema uzalishaji wa ndani kwa ndani wa malighafi yanayotokana na kibayoteknolojia unaweza kuunda nafasi za ajira, kuimarisha sekta ya utengenezaji wa chakula cha mifugo na kupunguza kiwango cha fedha zinazotumika kuagiza malighafi nje ya Kenya. Hata hivyo, alisema maendeleo yamekuwa yakikwamishwa na sera zilizogawanyika kuhusu upatikanaji wa malighafi na biashara. [caption id="attachment_191114" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi wa ISAAA AfriCenter, Dkt Margaret Karembu akihutubu Jijini Nairobi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mbali na kanuni za kibayoteknolojia, Dkt Karembu alitaja ushuru wa kaunti unaotozwa wakati wa kusafirisha mazao ya kilimo (cess) kama mzigo mwingine unaoongeza gharama kwa watengenezaji wa chakula cha mifugo. Alisema ada nyingi zinazotozwa bidhaa zinaposafirishwa kutoka kaunti moja hadi nyingine huongeza gharama za uzalishaji na kupunguza ushindani wa wazalishaji wa ndani kwa ndani. "Serikali inahitaji kuoanisha sera zinazoathiri watengenezaji wa chakula cha mifugo. Kupunguza gharama ya chakula cha mifugo hatimaye kutapunguza bei ya mayai, maziwa na nyama, na hivyo kuwanufaisha walaji," alisema. Dkt Karembu alisema malighafi zinazotokana na kibayoteknolojia zimetumika kwa usalama duniani kwa muda mrefu na hazipaswi kulemazwa na vikwazo visivyo vya lazima pale ambapo usalama wake umethibitishwa kisayansi. Kulingana naye, kikwazo kikubwa kwa matumizi ya kibayoteknolojia si sayansi tena, bali ni taarifa potovu na upotoshaji. "Licha ya kutumika duniani kwa zaidi ya miongo mitatu, taarifa za uongo zinaendelea kuzua hofu miongoni mwa walaji na watunga sera, hivyo kuchelewesha utekelezaji wa sera zilizopo," alisema. Alisema kampeni endelevu za uhamasishaji wa umma na mawasiliano yanayotegemea sayansi yanahitajika ili kuondoa dhana potovu kuhusu bayoteknolojia. Pia, alitoa wito kwa nchi za Afrika kuoanisha kanuni zao za kibayoteknolojia, akisema tofauti katika mahitaji ya udhibiti zinafanya biashara ya mipakani kuwa ngumu bila sababu, licha ya nchi nyingi kutegemea viwango vinavyofanana vya kimataifa vya usalama. Dkt Karembu alisema kutokuwa na uhakika wa sera pia huwakatisha tamaa wawekezaji wa ndani kwa ndani na nje kuwekeza katika utafiti na biashara ya kibayoteknolojia. Alisema walaji wanapaswa kupewa fursa ya kuchagua kati ya bidhaa zinazotokana na kibayoteknolojia na zile za kawaida, badala ya chaguo hizo kuzuiwa na taarifa potovu. Kwa kuwa chakula cha mifugo kinachukua zaidi ya asilimia 60 ya gharama za uzalishaji wa mifugo, Dkt Karembu anakadiria kuwa kupunguza gharama ya malighafi kunaweza kushusha bei ya mayai, maziwa na nyama kwa karibu asilimia 30. Akieleza kuhusu usalama wa kibayoteknolojia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kibayoteknolojia ya KALRO, Dkt Martin Mwirigi, alisema tathmini za kisayansi za usalama hufanywa kabla ya zao lolote lililobadilishwa vinasaba kuwafikia wakulima au walaji. [caption id="attachment_191115" align="aligncenter" width="300"] Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kibayoteknolojia ya KALRO, Dkt Martin Mwirigi. Picha|Sammy Waweru[/caption] Alisema watafiti hufanya tathmini pana zinazohusisha kiwango cha virutubisho, sumu na uwezekano wa kusababisha hasara kabla bidhaa kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa idhini. "Lengo ni kuhakikisha mazao yaliyobadilishwa vinasaba yanaendelea kuwa sawa na yale ya kawaida katika thamani ya lishe. Tofauti pekee ni sifa maalum iliyoingizwa, kama vile uwezo wa kustahimili wadudu au magonjwa," alisema. Dkt Mwirigi alitaja aina za viazi zilizobadilishwa vinasaba ili kustahimili ugonjwa wa late blight kama mfano bora, akisema zao hilo hupata uwezo wa kustahimili ugonjwa huo huku ubora wake wa lishe ukisalia vilevile. Alisema wanasayansi pia huchunguza iwapo sifa mpya zilizoingizwa zinaweza kusababisha sumu au hasara kabla bidhaa kuwasilishwa kwa mamlaka za udhibiti (National Biosafety Authority). Kwa upande wa wazalishaji wa chakula cha mifugo, Mwenyekiti wa Association of Kenya Feed Manufacturers (AKEFEMA), Joseph Karuri, alisema utegemezi mkubwa wa Kenya kwa malighafi kutoka nje unaweka nchi katika hatari ya kukumbwa na upungufu wa bidhaa hizo. Alisema karibu asilimia 80 ya soya inayouzwa duniani imebadilishwa vinasaba, huku nchi kubwa zinazozalisha kilimo kama Amerika, Brazil, Argentina na Afrika Kusini zikiwa zimekubali teknolojia hiyo. "Kenya inapaswa kuanza kujiandaa sasa kwa mahitaji ya chakula ya siku zijazo kwani idadi ya watu inatarajiwa kuongezeka maradufu katika miaka 25 ijayo, huku mabadiliko ya tabianchi yakiendelea kupunguza uzalishaji wa kilimo kutokana na ukame unaoongezeka," alisema. Kwa sasa, Kenya huagiza karibu asilimia 80 ya malighafi za chakula cha mifugo kutoka Tanzania, Uganda, Zambia na Malawi. Karuri alisema utegemezi huu unaweza kuwa hatari kwa sababu nchi hizo zinapanua viwanda vyao vya chakula cha mifugo na hivyo kupunguza uuzaji wa bidhaa nje. "Hatupaswi kutegemea nchi nyingine kabisa kutulisha. Uzalishaji wa mahindi na soya nchini utaimarisha usalama wetu wa chakula na kupunguza utegemezi huo," alisema. Alisema sekta ya kuku hutumia takriban asilimia 60 ya chakula chote cha mifugo kinachozalishwa nchini, hivyo kuwa katika hatari kubwa ya mabadiliko ya bei ya mahindi na soya. Mbali na kuunga mkono bayoteknolojia, Karuri alisema sekta hiyo ya chakula cha mifugo inahimiza matumizi ya malighafi mbadala kama azolla, wadudu kama vile BSF, unga wa nyama na mifupa ili kupanua vyanzo vya malighafi na kuimarisha ustahimilivu wa sekta hiyo kwa muda mrefu. AKEFEMA, pamoja na washirika wengine wa maendeleo, iliandaa Mkutano wa Africa Feed and Feed Ingredients Conference (AFEC) 2026, uliofanyika Julai 15 na 16 Jijini Nairobi, ambapo wataalamu na washikadau walijadili mikakati ya kupunguza gharama ya chakula cha mifugo nchini huku wakiimarisha na kukuza sekta hiyo.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.