WIRE โ CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kaunti ya Nairobi kimeanzisha kampeni ya kuimarisha umaarufu wake mashinani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Hii ni siku chache baada ya kushiriki mkutano wa pamoja na chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto, uliofanyika Naivasha, Nakuru. Katika mkutano na wanahabari jijini Nairobi Alhamisi, ulioongozwa na mwenyekiti wa ODM katika kaunti hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Makadara, George Aladwa, viongozi hao walisema wataimarisha ngome za ODM jijini Nairobi huku wakihamasisha wapiga kura kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa urais. "Mikakati yetu ni kulinda ngome za ODM huku tukihamasisha wapiga kura kumuunga mkono rais. Tutatumia mitandao yetu ya mashinani, matawi na viongozi wa wadi kuhakikisha makubaliano ya kisiasa tuliyofikia yanageuzwa kuwa kura," akasema Bw Aladwa. Viongozi hao walisema wataendelea kujenga na kuimarisha ODM huku wakitekeleza majukumu yaliyoafikiwa chini ya Serikali Jumuishi. "Ujumbe kutoka Nairobi ni kuwa ODM itabaki imara, itashinda viti zaidi na kutimiza ahadi zake. Nawahimiza viongozi wote wa matawi na maafisa wa chama kubaki pamoja, wawe wenye nidhamu na kuzingatia malengo ya chama. Tuipange Nairobi, tuimarishe ngome zetu, tushinde viti zaidi na kutimiza ahadi zetu," akasema. Kwa mujibu wa Bw Aladwa, ushindi katika uchaguzi wa 2027 utategemea mipango madhubuti na uhamasishaji wa wapigakura mashinani. Alisisitiza umuhimu wa kampeni za amani na kuheshimu wagombea wote bila kujali misimamo yao ya kisiasa. "Hakuna haja ya matusi. Tunamwambia Rigathi Gachagua aache kumtusi Rais na awe tayari kukabiliana naye katika uchaguzi wa 2027," akasema. Viongozi hao pia walitangaza kuwa mbali na kudai nafasi ya Naibu wa Rais itengewe ODM, chama hicho pia kitataka nafasi ya Gavana wa Nairobi pamoja na viti vingine vya kisiasa. "Tumekubaliana kwamba tunaanza na kiti cha Naibu Rais, ugavana Nairobi, diwani na viti vingine vyote vya kuchaguliwa vipewe ODM. Hatutaruhusu kugawana maeneo hapa; ODM iendelee kushikilia nafasi zake katika maeneobunge ambayo kwa sasa ina nguvu," akasema Bw Aladwa. Alisema chama kinaunga mkono Ruwaza ya 2060 iliyozinduliwa Jumatano, akisema Kenya inahitaji mpango wa muda mrefu wa maendeleo baada ya Ruwaza ya 2030. Kiongozi wa vijana Stazo Omung'ala alisema wanachama wa ODM wataunga mkono uamuzi wa kiongozi wa chama, Dkt Oburu Oginga, kwamba ODM haitawasilisha mgombea wa urais katika uchaguzi wa 2027.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.