WIRE โ MGAWANYIKO uliokumba IEBC baada ya uchaguzi mkuu wa 2022 haukuwa tu mzozo wa kisiasa, bali dalili ya mgororo uliokuwa umetokota ndani ya tume. Kilichotikisa imani ya umma si tofauti za kimaoni miongoni mwa makamishna, bali namna tofauti hizo zilivyojitokeza hadharani wakati Wakenya wakisubiri taasisi iliyopaswa kuzungumza kwa sauti moja kutoa mwelekeo muhimu. Hakuna taasisi ya kidemokrasia inayopaswa kuogopa maoni tofauti. Kinachodhoofisha taasisi ni kuyaficha, kuyanyamazisha au kuyasukuma hadi yalipuke mbele ya umma. Uwazi hujenga uaminifu, huku ukimya na kuficha tofauti zikizalisha mashaka. IEBC mpya inapaswa kujifunza kutokana na yaliyotokea mnamo 2022. Mwenyekiti si mmiliki wa tume, wala makamishna si watazamaji. Sheria imeweka tume ya pamoja ambayo maamuzi yake yanapaswa kujengwa kupitia majadiliano, uwajibikaji na kuheshimiana. Tofauti za kitaaluma zinapaswa kushughulikiwa ndani ya vikao vya tume, badala ya kujitokeza hadharani wakati wa kutangaza matokeo. Funzo kutokana na tume ya Wafula Chebukati si kwamba makamishna hawapaswi kutofautiana. Ni kwamba, tofauti hizo zinapaswa kusimamiwa kwa uwazi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria kabla hazijageuka kuwa mgogoro wa kitaifa. Uchaguzi haujengwi kwa kura pekee; hujengwa pia kwa imani ya wananchi kwa mwamuzi. IEBC ikipoteza imani hiyo, hata uchaguzi ulioendeshwa kwa usahihi unaweza kutiliwa shaka. Utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na kuheshimu maoni ya ndani ndio msingi wa kurejesha na kulinda imani hiyo. Ondieki ni mwalimu wa Kiswahili
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.