WIRE โ€” KAMPUNI mbili zinazohusishwa na marehemu mfanyabiashara Francis Mburu, zimewasilisha kesi katika Mahakama Kuu zikitaka kuzuia Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kurejesha Sh1.5 bilioni zilizolipwa kama fidia ya ardhi kulikojengwa shule mbili za umma eneo la Ruaraka, Nairobi. Afrison Export Import Limited na Huelands Limited, zinataka mahakama izuie EACC kuanzisha mchakato wa kurejesha fedha hizo hadi rufaa yao iliyo mbele ya Mahakama ya Juu itakapoamuliwa. EACC inadai karibu Sh2.5 bilioni kutoka kwa watu binafsi na kampuni, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang'i, Katibu wa Idara ya Uhamiaji Belio Kipsang, pamoja na kampuni zinazohusishwa na familia ya Mburu. Tume hiyo inalenga kurejesha fedha zilizolipwa kampuni binafsi kama fidia ya ekari 13.77 za ardhi hiyo iliyoko Ruaraka, ambayo serikali inasema tayari ilikuwa mali ya umma. Kupitia barua za madai, EACC imewataka walengwa wote kurejesha Sh1.5 bilioni pamoja na riba ya asilimia 12 kwa mwaka tangu Januari 2018, fedha hizo zilipolipwa kampuni ya Whispering Palms Estate Limited. Miongoni mwa waliopokea notisi hizo ni aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Ardhi ya Taifa (NLC) Muhammad Swazuri, makamishna wa zamani Tom Konyimbih na Emma Muthoni Njogu, pamoja na wakurugenzi wa kampuni husika Mark Mungai Mburu na Justin Sam Mburu. Katika stakabadhi zilizowasilisha kortini, Afrison Export Import Limited na Huelands Limited, kupitia mkurugenzi mwenza Mark Mburu, zinasema EACC imechukua hatua mapema mno kurejeshwa kwa fedha hizo kabla ya Mahakama ya Juu kusikiliza na kuamua rufaa yao. Mburu alisema EACC, kupitia barua ya Julai 6, ilitaka fedha hizo zirudishwe na kuonya kuwa hatua za kisheria ingechukuliwa ikiwa kampuni hizo hazingetii agizo hilo. Kampuni hizo zinahoji kuwa kesi yao imepangwa kutajwa Agosti 14 katika Mahakama ya Juu na kwamba hatua ya EACC inaweza kuathiri haki yao ya kusikilizwa kwa usawa. "Uamuzi wa mshtakiwa ni wa haraka mno, hauna mantiki na unakiuka kanuni za utawala wa haki kwa sababu unataka kutekeleza matokeo ya hukumu ambayo bado iko katika mchakato wa rufaa," zilisema kampuni hizo. Rufaa yao inapinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba fidia hiyo ilitolewa kinyume cha sheria. Kampuni hizo zinadai majaji hawakuzingatia kikamilifu ushahidi wao kuhusu umiliki wa ardhi pamoja na historia ya mgogoro huo. Pia, zinasema Mahakama ya Rufaa ilishindwa kutofautisha kati ya masharti ya mipango ya maendeleo ya ardhi na utaratibu wa kikatiba wa kutwaa mali binafsi kwa manufaa ya umma. Kwa mujibu wa kampuni hizo, mahakama ilitafsiri visivyo idhini ya upangaji wa ardhi kana kwamba ingeweza kutumika kuhamisha mali ya kibinafsi kwa matumizi ya umma bila kufuata masharti ya Katiba kuhusu unyakuzi wa ardhi. Aidha, zinadai kuwa mahakama ilikiuka haki za kikatiba za kumiliki mali na usalama wa hati miliki za ardhi. Kampuni hizo zinasisitiza kuwa hakuna fedha za umma zilizopotea na zinaitaka NLC kulipa salio la Sh1.77 bilioni ambalo lilikuwa limeidhinishwa kama sehemu ya fidia.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.