WIRE โ€” RAIS Mwai Kibaki alipozindua mpango wa Ruwaza ya Kenya 2030 mwaka 2008, aliipa nchi mwelekeo wa maendeleo wa muda mrefu. Karibu miongo miwili baadaye, Rais William Ruto sasa anataka Wakenya waamue taifa litachukua mkondo gani baada ya 2030. Akizindua rasmi mdahalo wa kitaifa kuhusu Mustakabali wa Kenya Baada ya Ruwaza ya 2030 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta (KICC) jijini Nairobi jana, Dkt Ruto alisema taifa linahitaji mwongozo mpya wa maendeleo wa muda mrefu unaotokana na matarajio ya wananchi badala ya mahitaji ya kisiasa ya muda mfupi. Rais alisema serikali itatoa jukwaa na rasilimali za kuwezesha mchakato huo, lakini itaacha Wakenya wenyewe waamue maudhui na mwelekeo wa ruwaza hiyo mpya. "Tofauti na miradi ya kawaida ya serikali, huu si mradi wa serikali. Huu ni mradi wa wananchi," alisema Dkt Ruto.Alisisitiza kuwa serikali haitadhibiti mjadala huo. "Serikali haitaongoza mazungumzo. Tutatoa jukwaa ili wananchi waamue," alisema huku akiwahimiza Wakenya kuwasilisha mawazo mbalimbali kuhusu mustakabali wa nchi. Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa kisiasa, magavana, wafanyabiashara, viongozi wa kidini, wanaharakati wa kijamii, wasomi, wanafunzi na watoto, ambao walitoa maoni tofauti kuhusu Kenya wanayotamani kuona siku zijazo. Miongoni mwa walioibua hisia nyingi alikuwa Adrian Ombuni mwenye umri wa miaka saba. "Ndoto yangu kwa Kenya ni kuona shule nzuri kwa watoto wote, hospitali bora kwa kila mtu, maji safi kwa kila nyumba, barabara safi kila mahali na ajira kwa vijana," alisema. Ingawa Adrian ni mdogo mno kuelewa siasa au sera za kiuchumi, kauli yake ilielezea kwa urahisi changamoto kuu ya mjadala huo โ€” jinsi ya kubadilisha ndoto za kitaifa kuwa maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi wa kawaida. Mwanaharakati Daisy Amdany alisema ifikapo mwaka 2060, Adrian atakuwa na umri wa miaka 41. "Kenya inayojadiliwa leo si ya viongozi walio madarakani pekee, bali ya Adrian na mamilioni ya vijana watakaorithi taifa hili," alisema. Katika hotuba yake, Rais Ruto alimpongeza Kibaki kwa kuanzisha Ruwaza ya 2030, akisema iliwezesha Kenya kuwa na malengo ya wazi ya maendeleo pamoja na mfumo wa kupima mafanikio. Hata hivyo, alikiri kuwa utekelezaji wa baadhi ya nguzo za ruwaza hiyo haukufanikiwa kikamilifu. "Katika nguzo zote, ni ile ya uchumi ambayo hatukufanya vizuri vya kutosha," alisema. Mwenyekiti wa Bodi ya Utekelezaji wa Ruwaza ya 2030, Dkt Emmanuel Nzai, alitetea mpango huo akisema umebadilisha nchi kwa kiwango kikubwa. "Ruwaza ya 2030 imebadilisha Kenya. Huu si uvumi, ni ushahidi wazi," alisema huku akitaja miradi mikubwa kama ukanda wa usafirishaji wa LAPSSET. Kwa upande wake, Gavana wa Kisumu Prof Anyang' Nyong'o, ambaye alikuwa miongoni mwa wataalamu waliohusika kuandaa Ruwaza ya 2030, alisema ni muhimu kuanza sasa kupanga maisha ya Kenya baada ya mwaka 2030. Alisema taifa linahitaji kujadili namna ya kujenga uchumi wenye mapato ya juu, thamani kubwa na uwezo wa kukabiliana na misukosuko huku wananchi wengi wakinufaika. Taarifa zinaonyesha kuwa Prof Nyong'o ataongoza timu ya sekta mbalimbali itakayounda ramani mazungumzo hayo yatakayopelekwa hadi ngazi ya mashinani. Mojawapo ya mada zilizojitokeza kwa nguvu katika mkutano huo ni haja ya kulinda mipango ya maendeleo dhidi ya mabadiliko ya kisiasa kila baada ya uchaguzi. "Kenya ni kubwa kuliko uchaguzi wowote. Uchaguzi si suala la uhai au kifo," alisema Rais Ruto. Alionya kuwa viongozi wengi hufikiria uchaguzi ujao badala ya kizazi kijacho, hali ambayo huathiri utekelezaji wa mipango ya muda mrefu. Naibu Rais Prof Kithure Kindiki alisema mojawapo ya changamoto kubwa katika mataifa yanayoendelea ni kuvurugwa kwa sera kila serikali mpya inapoingia madarakani. "Kero kubwa kwa nchi nyingi za Afrika ni kusitishwa kwa sera zilizowekwa na tawala zilizopita," alisema.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.