WIRE โ IDADI ya wanasiasa waliomsaidia Rais William Ruto na chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kujijenga kisiasa katika eneo la Mlima Kenya 2022 wanaohama chama hicho inaendelea kuongezeka. Wanasiasa hao wanasema hatua hii inatokana na mabadiliko ya kisiasa yanayohitaji mikakati mipya ya kujiokoa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Mbunge wa Gatundu Kusini Gabriel Kagombe ndiye mwanasiasa wa hivi punde kutangaza kujiondoa UDA, akisema imekuwa vigumu kuwashawishi wapigakura wa Mlima Kenya kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili. Kwa mujibu wa Bw Kagombe, hatua yake ni suala la kuendelea kujisitiri kisiasa. "Mazingira ya kisiasa yamebadilika kabisa. Huu ni wakati wa dharura na kila mwanasiasa anatafuta namna ya kuendelea kuishi. Wapigakura wangu wanakasirika kila jina la Dkt Ruto au UDA linapotajwa," alisema. Mbunge huyo alisema atarudi kwa wapiga kura wake kuwaeleza sababu za uamuzi wake, ikiwemo kile alichokitaja kuwa "ahadi zisizotekelezwa za UDA za Rais Ruto kwa Mlima Kenya" pamoja na kuongezeka kwa malalamishi kuhusu nafasi ya eneo hilo ndani ya serikali jumuishi. Alisema hatua ya kumfanya abadili msimamo ilitokea wakati wa mkutano wa serikali jumuishi uliofanyika Naivasha Jumatatu, ambapo Gavana wa Kisii Simba Arati alitangaza wazi kuwa ODM inataka nafasi ya Naibu Rais. Kwa mujibu wa Bw Kagombe, kauli hiyo ilituma ujumbe wa kisiasa uliowatia wasiwasi viongozi wa UDA kutoka Mlima Kenya. "Fikiria jinsi tulivyohisi Bw Arati alipodai kiti kinachoshikiliwa na Profesa Kithure Kindiki akiwa hapo hapo. Rais hakukubali wala kukataa. Hiyo inaonyesha mjadala huo unampendeza. Sasa ni wakati wa kutathmini na mimi lazima nijinusuru," alisema. Kagombe, ambaye alikuwa miongoni mwa wabunge waliounga mkono kung'olewa mamlakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, alisema siasa ni mchezo wa maslahi, kukubalika na kuendelea kudumu kisiasa. Kung'olewa kwa Bw Gachagua miaka miwili iliyopita kumeendelea kuzua mgawanyiko wa kisiasa katika Mlima Kenya, huku wapigakura wakitathmini viongozi kwa msingi wa uaminifu wao kwa maslahi ya eneo hilo. Wanasiasa wanaojiondoa UDA sasa wanakabiliwa na changamoto ya kurejesha imani ya wapigakura ambao kwa kiasi kikubwa wameonyesha uhasama dhidi ya chama tawala. Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata alikuwa gavana wa kwanza wa Mlima Kenya aliyechaguliwa kujiondoa rasmi UDA na kuhamia chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua. Hatua yake ilifuatiwa na ya Gavana wa Nyandarua Kiarie Badilisha, aliyehamia DCP Julai 29. Gavana huyo alisema alikuwa akifuata matakwa ya wananchi wake. "Wananchi wa Nyandarua wamezungumza, nami nitatetea kiti changu kupitia tiketi ya DCP," alisema. Katika Kaunti ya Kiambu, Gavana Kimani Wamatangi tayari amesema hatawania muhula mwingine kupitia tiketi ya UDA, hali inayotafsiriwa kama ishara ya kuondoka kwake katika chama hicho, ingawa bado hajatangaza rasmi kujiunga na DCP. Mabadiliko hayo yanajiri huku viongozi mbalimbali wa kisiasa wakitathmini upya misimamo yao kuelekea uchaguzi wa 2027, huku DCP ikionekana kujijenga kama jukwaa kuu la upinzani dhidi ya UDA katika Mlima Kenya. Changamoto za UDA pia zinaonekana nje ya Mlima Kenya. Mwakilishi wa Wanawake wa Lamu Muthoni Marubu amesitisha mpango wake wa kujiunga na chama hicho baada ya miezi kadhaa ya kujaribu kujijenga mashinani katika kaunti hiyo. Bi Marubu, aliyechaguliwa kama mgombea huru mnamo 2022, alisema Rais Ruto alikuwa amemuomba kusaidia kuimarisha UDA Lamu. Alidai alitumia miezi mitatu kuandaa mikutano 42 ya mashinani na kusajili wanachama. Hata hivyo, juhudi hizo zilikwama baada ya mzozo wa kisiasa kati yake na Gavana wa Lamu Issa Timamy, ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Pili wa UDA. Bi Marubu alimlaumu Bw Timamy kwa kuhujumu juhudi zake na kupuuza majaribio yake ya kushirikiana naye kisiasa. Kwa upande wake, Bw Timamy alikanusha madai hayo akisema yeyote anayetaka kuondoka chama ana uhuru wa kufanya hivyo bila kuwasingizia wengine. Mchambuzi wa siasa Mixson Warui alisema mwelekeo wa sasa unaonyesha DCP inavutia zaidi katika Mlima Kenya. Alisema uchaguzi mdogo wa Ol Kalou wa Julai 16 ulionyesha hali hiyo baada ya DCP kupata takriban asilimia 85 ya kura. "Ikiwa matokeo ya Ol Kalou ni kipimo, basi nafasi kubwa ya kuendelea kuwa katika siasa katika Mlima Kenya kwa sasa ni kupitia Bw Gachagua. Lakini kujiunga na DCP si jambo la moja kwa moja kwa sababu kuna utaratibu wa kuwachunguza wanaotaka kuhamia chama hicho," alisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.