WIRE โ LICHA ya kuongezeka kwa wito wa kuwezesha wanawake kushikilia nyadhifa za juu za uongozi, idadi ya wanaojitokeza kuwania viti vya ugavana katika eneo la Pwani kuelekea uchaguzi wa 2027 ni ndogo. Hali hiyo imeibua mjadala kuhusu sababu zinazofanya wanawake wengi kusita kuingia katika kinyang'anyiro hicho, licha ya hitaji la kuvunja ukiritimba wa wanaume na kutimiza kanuni ya katiba ya theluthi mbili ya jinsia. Takribani mwaka mmoja kabla ya uchaguzi ni Gavana Fatuma Achani wa Kwale, na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Jinsia, Aisha Jumwa, pekee waliotangaza hadharani nia yao ya kuwania ugavana. Tofauti na mwaka 2022 ambapo wanawake kadhaa walijaribu bahati yao katika kaunti mbalimbali za Pwani, safari hii wengi wamekaa kimya huku baadhi wakielekeza macho katika nyadhifa nyingine kama ubunge, uwakilishi wa wanawake au nafasi za uteuzi. Kaunti tano kati ya sita za Pwani; Mombasa, Kilifi, Lamu, Tana River na Taita Taveta zinaongozwa na magavana wanaume. Kwale ndiyo pekee iliyowahi kumchagua mwanamke, hatua iliyomweka Achani miongoni mwa magavana saba wanawake nchini, waliojiweka chini ya mwavuli wa G7. Kulingana na tathmini ya wachambuzi wa masuala ya siasa, hali hiyo inaonyesha bado kuna pengo kubwa la uwakilishi wa wanawake katika ngazi za juu za uongozi wa kaunti, licha ya jinsia hiyo kuwa sehemu kubwa ya wapigakura. Moja ya sababu kuu zinazotajwa ni mizizi ya taasubi ya kiume inayoendelea kutawala jamii nyingi za Pwani. Ingawa wanawake wamepiga hatua katika elimu, biashara na taaluma mbalimbali, bado kuna mtazamo kwamba nafasi za kisiasa zinapaswa kushikiliwa na wanaume. Mtazamo huo huathiri namna wanawake wanapokelewa wanapotangaza nia ya kuwania nyadhifa kama ugavana. Wanawake pia hukumbana na mashambulizi ya maneno, dhihaka na kejeli zinazolenga kuwavunja moyo. Mara nyingi hulazimika kujibu maswali kuhusu maisha yao ya kibinafsi au uwezo wao wa kuongoza, darubini ambayo haimuliki wagombea wengi wa kiume kwa kiwango sawa. Akizungumza mjini Diani, Gavana Achani alisema wanawake wanaotaka kufanikiwa kisiasa lazima wawe na uvumilivu sababu watakumbana na mazingira magumu. "Nashangaa jinsi wanaume wanawadhalilisha wanawake. Lazima mwanamke awe ngangari kufanikiwa. Mimi ni simba jike ndiyo maana nimekita kisiasa," akaeleza. Aliongeza kwamba amekuwa akikabiliwa na upinzani mkali lakini anaamini maendeleo aliyotekeleza ndiyo yatamsaidia kutetea kiti chake. Changamoto nyingine ni ukosefu wa uungwaji mkono kutoka kwa vyama vya kisiasa na wafadhili wa kampeni. Wanasiasa wanawake mara nyingi hulazimika kutumia muda mwingi kutafuta fedha za kampeni huku vyama vikionekana kuwaamini zaidi wagombea wanaume wanaodhaniwa kuwa na nafasi kubwa ya kushinda. Gharama kubwa za kampeni pia zimeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanawake wenye nia ya kuwania ugavana. Aidha, baadhi ya wanawake wanaochipuka kisiasa huona kuwa ni afadhali kuwania nyadhifa za ubunge au uwakilishi wa wanawake badala ya kujitosa katika mbio za ugavana ambazo huhitaji rasilimali nyingi na zina ushindani mkali.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.