WIRE โ€” ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua jana alikosoa vikali utawala wa Rais William Ruto akiwasilisha tathmini yake kuhusu sekta mbalimbali. Katika hotuba yake kwa taifa, Bw Gachagua alisema tathmini hiyo inalenga kupima "ahadi dhidi ya utendaji, nia dhidi ya utekelezaji na matarajio dhidi ya matokeo". Alipitia kurasa 39, akitaja alichodai kuwa ni kushindwa kwa serikali katika uchumi na huduma kwa umma, ufisadi, zigo la kodi, magenge ya wahuni, utekaji nyara, ahadi za uongo na kubadilishwa kwa sera. Bw Gachagua alikuwa sehemu ya timu iliyomsaidia Dkt Ruto kushinda uchaguzi wa 2022 na akahudumu kama Naibu Rais hadi uhusiano wao wa kisiasa ulipovurugika na akang'atuliwa ofisini mnamo Oktoba 17, 2024. Kiongozi huyo wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) alisema Wakenya walichagua serikali ya Kenya Kwanza mnamo 2022 kwa kuamini Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi ya Kuanzia Mashinani na ahadi za kuboresha maisha yao. Miaka minne baadaye, alisema serikali imeshindwa kutimiza ahadi hizo. "Mpango huo umeshindwa. Ni batili na wa kupotosha!" alisema Bw Gachagua. Alidai serikali sasa imeelekeza nguvu zake katika mchakato wa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo, Ajenda ya Vipengele 10 na mpango wa maendeleo wa muda mrefu wa ruwaza ya baada ya 2030, badala ya kutimiza ahadi za awali. Gachagua alielekeza sehemu kubwa ya shutuma zake kwa uchumi na gharama ya maisha. Alisema ahadi ya Kenya Kwanza ya kuweka fedha zaidi mifukoni mwa Wakenya imegeuka kuwa mzigo wa kodi, makato ya kisheria na bei za bidhaa kupanda. Alitaja bei ya mafuta ya Petroli ambayo imeongezeka kutoka Sh159.12 kwa lita Agosti 2022 hadi Sh214.03. Dizeli imepanda kutoka Sh140 hadi Sh222.86. Alisema ongezeko hilo limechangia kupanda kwa gharama ya usafiri na chakula huku likipunguza uwezo wa familia kutumia fedha kwa mahitaji mengine. Pia, alikosoa sera za kodi akisema familia sasa zinatumia fedha nyingi zaidi kununua chakula, mafuta, umeme na bidhaa nyingine muhimu. Takwimu za Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) zinaonyesha mfumuko wa bei ulifikia asilimia 6.5 Julai, kiwango cha pili cha juu zaidi katika kipindi cha miezi 30. Gachagua pia alikosoa deni la taifa, akisema limeongezeka kutoka Sh8.66 trilioni Agosti 2022 hadi Sh13.02 trilioni. Alisema zaidi ya Sh4 trilioni zimekopwa katika miaka minne ya utawala wa Rais Ruto, bila maendeleo yanayolingana na kiwango hicho cha madeni. Katika afya, Gachagua alishutumu serikali kwa kutotekeleza ahadi ya Afya kwa Wote na kubadilisha NHIF na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA). Alikosoa kusitishwa kwa mipango ya Linda Mama na Edu Afya, akisema hatua hiyo imeongeza mzigo kwa familia. Katika usalama na haki za binadamu, Gachagua alishutumu serikali kwa kile alichokiita "kuvunjika kabisa kwa sheria na utulivu". Alidai magenge ya wahuni yameruhusiwa kufanya kazi pamoja na polisi na serikali imeshindwa kuwajibisha waliohusika na mauaji na utekaji nyara.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.