WIRE โ KILA kiongozi anaruhusiwa kufanya kampeni mahala popote nchini kwa sababu Kenya ni taifa huru na kila mwanasiasa ana haki ya kuendeleza ajenda yake ya kisiasa. Aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza kuwa analenga kuzuru Kusini mwa Bonde la Ufa kwa misururu ya mikutano ya kisiasa ya kuuza chama chake cha DCP na azma yake ya urais. Kundi la Linda Mwananchi ambalo linaongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna nalo limetangaza kuwa litakuwa na mkutano mkubwa wa kisiasa Kaunti ya Homa Bay wikendi hii. Linda Mwananchi pia ina Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi miongoni mwa wanasiasa wengine. Mbunge wa Emurua Dikirr David Keter alinukuliwa akimtaka Bw Gachagua asitie guu katika eneobunge lake akisema kiongozi huyo wa DCP anastahili kuelekeza nguvu zake maeneo mengine. Bw Keter anadai kuwa Emurua Dikirr ni ngome ya kisiasa ya UDA. Viongozi wengine kama Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho) na Jackson Mandago (Uasin Gishu) nao wamesema kuwa Bw Gachagua yuko huru kufika Bonde la Ufa lakini ajue anafanya kazi bure kwa sababu kura zake haziko huko. Kwa upande mwingine baadhi ya viongozi wa ODM kutoka Kaunti ya Homa Bay wamesema Linda Wananchi wako huru kuzuru kaunti hiyo lakini waepuke lugha ya matusi. Mbunge wa Homa Bay Opondo Kaluma amesema kuwa wanasiasa wa Linda Mwananchi hawafai kuwachokoza raia na kuwatusi huku Gavana Gladys Wanga akionya dhidi ya siasa za uhuni. Mwanzo, katiba iko wazi kuhusu kuzuru na kufanya kampeni kwa mwanasiasa yeyote na Bw Keter hafai kumzima Bw Gachagua asifike Emurua Dikirr. Hawa raia ambao mbunge huyu anamkataza Bw Gachagua asiwahutubie ndio wale wale ambao walimpigia mgombeaji wa DCP Vincent Rotich zaidi ya kura 10,000 kwenye uchaguzi mdogo miezi miwili iliyopita. Hata hivyo, Bw Gachagua naye anastahili kuchunga mdomo na asitoe matamshi ya kuwachochea raia dhidi ya viongozi wao kwa sababu matokeo ya kura yanaamuliwa debeni. Wakati mwingine mdomo wa Bw Gachagua ndio humchongea kwa sababu matamshi yake huwa yanajikita katika jamii moja nchini. Akienda Bonde la Ufa, auze ajenda yake na sera zake kuhusu jinsi atakavyobadilisha maisha ya Wakenya upinzani ukichukua mamlaka badala ya kutumia lugha isiyofaa na kuchochea fujo. Hii haimaanishi kuwa hafai kuzungumzia miradi ya maendeleo ambayo imefeli au ahadi ambazo serikali ilitoa na haijatimiza. Kila dai la Bw Gachagua linastahili kuandamana na ukweli badala ya uchochezi. Mabw Sifuna, Orengo na Owino nao wakifika Homa Bay wanastahili kuzungumzia ajenda yao ya kubadilisha eneo hilo badala ya kuvamia mrengo pinzani wa ODM unaoongozwa na Dkt Oburu Oginga. Watatu hawa wanafahamu fika kuwa Homa Bay ni kati ya kaunti ambazo zimenufaika pakubwa kimaendeleo kutokana na miradi kadhaa inayoendelea katika utawala huu wa Rais William Ruto. Kwa hivyo, wazungumzie mipango yao ya kustawisha na kuimarisha maisha ya watu badala ya kukosoa miradi inayoendelea ambayo kwa kweli inatarajiwa kubadilisha maisha ya watu wa eneo hilo.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.