WIRE โ€” TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) imeweka wazi ratiba muhimu itakayoongoza maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa Agosti 10, 2027, huku wanasiasa wakianza mapema kampeni za kutafuta uungwaji mkono. Kwa mujibu wa mpango wa IEBC wa kuendesha uchaguzi wa 2025-2027 mambo kadhaa yamepangwa kabla na baada ya siku ya kupiga kura. Miongoni mwa hatua muhimu ni usajili wa wapigakura ambao IEBC itafanya kwa siku 30 kuanzia Januari 11 hadi Februari 9, 2027. Zoezi hilo linalenga kuwapa vijana na Wakenya wengine ambao hawajasajiliwa nafasi ya kujiandikisha. Baada ya hapo, IEBC itafanya ukaguzi wa sajili ya wapigakura kuanzia Februari 15 hadi Machi 16, 2027 ili kubaini na kuondoa majina yanayojirudia au kasoro nyingine. Maafisa wa serikali wanaotaka kuwania nafasi za kisiasa watatakiwa kujiuzulu ifikapo Februari 9, 2027, miezi sita kabla ya uchaguzi. Vyama vya kisiasa vitatakiwa kuwasilisha orodha za wanachama wao kwa IEBC ifikapo Machi 16, 2027. Kufikia tarehe hiyo, vyama pia vinapaswa kuwa vimewasilisha majina ya watakaoshiriki katika mchujo, pamoja na tarehe na maeneo ya kufanyia kura hizo za mchujo. Vyama vinapaswa kukamilisha chaguzi zao za mchujo na kutatua malalamishi yanayotokana nazo ifikapo Mei 9, 2027. Wagombea huru pia watakuwa na hadi Mei 9 kuwasilisha majina na alama watakazotumia katika uchaguzi. Kufikia wakati huo, hawapaswi kuwa wanachama wa chama chochote cha kisiasa. Kampeni rasmi zitaanza Mei 2027 na kumalizika Agosti 7, siku mbili kabla ya uchaguzi. Hata hivyo, wanasiasa tayari wameanza kampeni licha ya muda rasmi kutokuwa umefika. IEBC pia imepanga wagombea na vyama kuwasilisha majina ya maajenti wa kitaifa, kaunti, maeneobunge na vituo vya kupigia kura ifikapo Julai 27, 2027. Wakenya wataelekea kupiga kura Agosti 10, 2027. Baada ya uchaguzi, IEBC ina siku saba kutangaza matokeo ya urais. Ikiwa hakutakuwa na kesi, rais mteule ataapishwa Jumanne ya kwanza baada ya siku 14 tangu kutangazwa kwa matokeo. Mtu asiyekubali matokeo ya urais atakuwa na hadi Agosti 17 kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Juu. Mahakama hiyo ina siku 14 kuamua kesi hiyo, kumaanisha uamuzi unapaswa kuwa umetolewa kufikia Septemba 7, 2027. Iwapo Mahakama ya Juu itabatilisha uchaguzi wa urais, uchaguzi mpya utafanyika ndani ya siku 60. Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ametoa wito kwa Bunge, Wizara ya Fedha, vyombo vya usalama na wadau wengine kushirikiana na tume kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa amani na wa kuaminika. Kwa IEBC, safari ya kuelekea Agosti 10, 2027 imeanza rasmi na kila hatua itakuwa muhimu katika kuamua ikiwa Kenya itakuwa tayari kwa uchaguzi huru na wa kuaminika.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.