WIRE โ€” TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) inakabiliwa na pengo la Sh33.5 bilioni katika bajeti inayohitajika kuandaa na kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027, huku mabadiliko ya kiteknolojia na upanuzi wa miundombinu yakiongeza gharama. Stakabadhi zilizowasilishwa Bungeni na IEBC, inayoongozwa na Erastus Ethekon, zinaonyesha kuwa tume hiyo imeomba jumla ya Sh74.8 bilioni kwa kipindi cha miaka mitatu ya maandalizi ya uchaguzi. Hata hivyo, serikali imetenga Sh41.3 bilioni pekee, na kuacha pengo la Sh33.5 bilioni ambalo IEBC inasema linaweza kuhatarisha maandalizi ya uchaguzi huru na wa kuaminika. Miongoni mwa maeneo yatakayoathirika ni malipo ya maafisa wa uchaguzi, ambayo yanahitaji Sh7.63 bilioni. Tume pia ina madeni ya Sh5.75 bilioni, mengi yakiwa ada za kisheria zilizotokana na chaguzi zilizopita. "Madeni haya yamekuwa yakijilimbikiza kwa muda na yataathiri vibaya shughuli za tume katika kuendesha uchaguzi mkuu wa 2027," ilisema IEBC. Kamati ya Bunge ya Sheria na Masuala ya Kikatiba (JLAC) imeonya Hazina ya Kitaifa kuwa upungufu huo unaweza kulemaza uwezo wa IEBC kutekeleza majukumu yake ya kikatiba. Hata hivyo, wabunge wameikosoa IEBC kwa baadhi ya vipaumbele vya matumizi, wakisema ni vya "ubadhirifu na visivyo na umuhimu". "Kwa nini IEBC inasisitiza kutumia Sh9.2 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS wakati wabunge hawajapewa matokeo ya ukaguzi kuthibitisha iwapo vifaa vilivyopo vimepitwa na wakati?" akauliza Mbunge wa Rarieda Dkt Otiende Amollo. IEBC inahitaji zaidi ya Sh10.7 bilioni kununua vifaa vipya vya KIEMS na kubadilisha vile vilivyopitwa na wakati. Tume pia inapanga kuongeza vituo vya kupigia kura kutoka 46,229 vilivyotumika katika uchaguzi wa 2022 hadi 55,393, huku idadi ya wapigakura waliosajiliwa ikitarajiwa kufikia milioni 28.5 mnamo 2027. Wabunge pia wameonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la makadirio ya gharama za uchaguzi, ambayo yamebadilika kutoka Sh57 bilioni hadi Sh61 bilioni, Sh63.9 bilioni na hatimaye Sh74.8 bilioni. Kamati ya Bunge ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba imeitaka Hazina kushughulikia pengo hilo na kutoa ratiba ya wazi ya kutolewa kwa fedha ili shughuli za uchaguzi zitekelezwe kwa wakati. IEBC pia imeonya kuwa kutolipwa kwa madeni ya zamani kunaweza kuathiri uendeshaji wake, ikiwemo kesi za mahakamani na kusababisha wanaotoa zabuni kukataa au kujiondoa katika kutoa huduma. Vifaa vya KIEMS vilinunuliwa 2017 na kwa kuwa teknolojia hubadilishwa baada ya miaka 10, IEBC inasema inalazimika kupata vifaa vipya ili kuhakikisha uchaguzi wa 2027 unaaminika. Mtaalamu wa masuala ya uchaguzi Koki Muli, hata hivyo, amependekeza kupunguza vituo vya kupigia kura kwa nusu na kuruhusu hadi wapigakura 2,000 katika kila kituo ili kupunguza gharama. "Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuruhusu angalau wapigakura 2,000 katika kila kituo. Hili halipaswi kutegemea Bunge kama ilivyo sasa. IEBC inaweza kuamua idadi ya wapigakura kwa kila kituo kiutawala," akasema Bi Muli.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.