WIRE โ MWAKA mmoja kuanzia leo, Wakenya watamiminika vituo vya kupigia kura kufanya uamuzi kuhusu atakayewatawala hadi 2032. Watachagua ama kumkabidhi Rais William Ruto muda mwingine wa miaka mitano au kumpa nafasi kiongozi mpya kuchukua usukani. Katika uchaguzi huo ambao tayari umepachikwa lakabu ya 'Tutam' dhidi ya 'Wantam', wapigakura watawachagua wabunge 290 wa Bunge la Kitaifa, magavana 47 na manaibu wao 47, wabunge wawakililishi wanawake 47, maseneta na madiwani (MCAs) kutoka wadi. Taifa limegawanywa katika wadi 1,450 za uchaguzi. Huu utakuwa uchaguzi mkuu wa nane tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi 1992. Utakuwa vilevile uchaguzi wa kwanza tangu 1997 ambapo jina la Raila Amolo Odinga halitajitokeza, ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, kwenye karatasi za kupiga kura. Bw Odinga aliaga dunia Oktoba mwaka jana na aliwania urais 1997, ubunge wa Langรกta 2007, urais 2013, 2017 na 2022. Mnamo 2022, kulikuwepo vituo vya kura 46,229. Kwenye kura ya 2027, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kuongeza vituo zaidi. Sajili ya IEBC ilikuwa na wapigakura wasiopungua 22.1 milioni 2022, na inatazamiwa kuwa idadi isiyopungua 6.3 milioni itaongezwa kwenye sajili mpya 2027. Tume inapanga shughuli ya usajili Januari mwaka ujao itakayoendeshwa kwa siku 30 kuanzia Januari 11 hadi Februari 9, 2027. amani ya kisiasa inatarajiwa kubadilikabadilika kabla ya siku ya uchaguzi, hasa upande wa upinzani. Hata Rais Ruto ambaye tayari yupo kwenye ushirikiano na ODM inayoongozwa na Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga ndani ya Serikali Jumuishi, angali anavutia vyama zaidi, huku baadhi kutoka upinzani wakitarajiwa kujiunga naye, hasa iwapo watafarakana kuhusu atakayepeperusha bendera ya urais. ย Ili kupanga kambi yake, Agosti 3, Baraza la muungano wa Azimio linaloongozwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, lilipitisha mchakato wa mabadiliko na kuwakaribisha wanasiasa wapya. Baraza hilo liliwajumuisha Naibu Kiongozi wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i, Kiongozi wa PNU Peter Munya na Seneta wa zamani wa Embu Lenny Kivuti katika kamati kuu ya baraza la Azimio. Lilikaribisha vilevile chama cha Justin Muturi cha Democratic Party, People's Democratic Party na Umoja na Maendeleo Party. Aidha baraza liliafikiana kufanya mageuzi na kumteua mgombea mmoja kumenyana na Rais Ruto. Lilianzisha vilevile mazungumzo na chama cha Rigathi Gachagua cha Democracy for the Citizens Party (DCP) na Linda Mwananchi, vuguvugu linaloendeshwa na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna. Kabla ya hapo, Bw Kenyatta alimtaja kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, kuwa kiongozi wa chama cha Azimio, nafasi iliyoshikiliwa na Bw Odinga. Ingawa hivyo, mratibu wa haya yote haya ni mtu ambaye hawezi kuwania binafsi. Bw Kenyatta anazuiliwa na kanuni ya hatamu, hashikilii afisi yeyote muhimu katika mpangilio mpya na anafanya kazi pasipo kumulikwa. Kinara wa People's Liberation Party, Martha Karua na wa DAP Eugene Wamalwa ni vinara katika muungano wa upinzani. Huku upinzani ukijadiliana, Rais vilevile anaendelea kusaka uungwaji mkono mashinani kwa kukutana na makundi mbalimbali mashinani. Katika wiki ya kwanza Agosti pekee, Ikulu iliwakaribisha wazee wa kijiji Jumanne, viongozi wa Kiislamu Jumatano na walinzi wa mashirika ya kibinafsi zaidi ya 5,000 Alhamisi. ย "Mko tayari?" Rais aliuliza katika kikao kimoja. Anaelewa uzito wa kibarua kinachomkabili. "Mtanisaidia kueneza neno hili kwa watu vijijini?" akasema. Matokeo ya utafiti wa TIFA yaliyofanyika kati ya Juni 13 na 22 miongoni mwa wahojiwa 2,048 katika maeneo tisa na kutolewa Julai 24 unamweka rais katika asilimia 24, ambayo haijabadilika kutoka Mei. Hii ni idadi dhaifu kwa rais anayetawala na itabidi Rais Ruto akaze buti ili awe na uungwaji mkono pia maeneo mengine. Seneta Sifuna ni wa pili kwa asilimia 15 akipanda kutoka 10 mnamo Mei na kutoka sufuri mwishoni mwa 2025. Bw Musyoka naye aliporomoka hadi asilimia 13 kutoka kilele cha asilimia 25 Novemba. Wakishajiishwa na uchaguzi mdogo wa Ol Kalou ambapo mwaniaji wa upinzani alimponda wa chama tawala, UDA, muungano wa upinzani unatumai kurudia ushindi huo katika jukwaa la kitaifa.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.