WIRE โ€” MALUMBANO yanayoendelea kati ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya huenda yakawa habari njema kwa Rais William Ruto anapojiandaa kutetea kiti chake katika uchaguzi wa 2027. Kinachoonekana kama mzozo wa kawaida kuhusu vyama kinaweza kuwa na athari kubwa kwa siasa za upinzani, hasa katika eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapigakura. Mzozo huo ulizuka baada ya viongozi wa vyama kadhaa kupinga kauli zinazohusishwa na Gachagua, kwamba vyama vidogo vinafaa kuvunjwa ili vijiunge na Democracy for the Citizens Party (DCP). Miongoni mwa waliopinga wazo hilo ni kinara wa Democratic Party (DP) Justin Muturi, kinara wa Party of National Unity (PNU) Peter Munya na kinara wa Devolution Empowerment Party (DEP) Lenny Kivuti. Viongozi hao walisema umoja wa upinzani haupaswi kujengwa kwa masharti au shinikizo, bali kupitia mashauriano, kuheshimiana na ushirikiano wa hiari. Hata hivyo, malumbano hayo yanaibua swali kubwa kuhusu nani atakuwa na ushawishi mkubwa Mlima Kenya kuelekea 2027. Tangu kuondolewa kwake kama Naibu Rais, Gachagua amekuwa akijaribu kujijenga kama kiongozi mkuu wa kisiasa wa eneo hilo. DCP imekuwa chombo muhimu katika mkakati huo, huku washirika wake wakijaribu kuunganisha wanasiasa wa mlimani chini ya chama kimoja kabla ya mazungumzo ya muungano wa kitaifa. Lakini msimamo wa Muturi, Munya na Kivuti unaonyesha kuwa si viongozi wote wanaompinga Ruto wako tayari kufuata mkondo wa Gachagua. Hilo linaweza kuwa pigo kwa mpango wa Mlima Kenya kuzungumza kwa sauti moja kuelekea 2027. Eneo hilo huwa na nguvu kisiasa linapoungana. Katika chaguzi zilizopita, viongozi walioweza kuunganisha kura za eneo hilo walipata usemi mkubwa katika mazungumzo ya kisiasa kitaifa. Lakini sasa kuna dalili za vituo vingi vya nguvu vita vya ndani vikionekana kuchacha. Jambo linalojitokeza kwenye mzozo huo ni kwamba baadhi ya viongozi wanaompinga Ruto sasa wanatumia nguvu nyingi kumjibu Gachagua, kuliko kueleza namna watakavyompinga Rais katika uchaguzi ujao. Badala ya mjadala kuwa Ruto dhidi ya upinzani, unaanza kuwa Gachagua dhidi ya viongozi wengine wa upinzani na wachambuzi wa siasa wanasema hili linaweza kumfaa Ruto. "Kadiri viongozi hao wanavyobishana kuhusu nani anafaa kuongoza Mlima Kenya, ndivyo wanapoteza muda wa kujenga kampeni moja kubwa ya kitaifa dhidi ya serikali.Kila tofauti ya maoni inaongeza uwezekano wa upinzani kuingia 2027 ukiwa umegawanyika," asema mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki. Kiini cha mzozo huo ni: nani ana haki ya kuzungumza kwa niaba ya Mlima Kenya? Washirika wa Gachagua wamemtaja kama kiongozi wa kisiasa wa eneo hilo kufuatia kuondolewa kwake mamlakani. Lakini wapinzani wake wanasema hakuna mtu aliyepewa mamlaka ya kuwa msemaji wa eneo lote. Muturi, Munya na Kivuti wanasisitiza kwamba hakuna mkutano uliowahi kufanyika kumpa Gachagua mamlaka hayo. Pia wanakumbusha kuwa hata marais wa zamani Jomo Kenyatta, Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta hawakuwahi kudai vyama vingine vivunjwe ili kuonyesha uaminifu kwao. Wanasema Gachagua anaweza kuwa na ushawishi mkubwa, lakini sio eti hana mpinzani. Viongozi hao pia wanaonekana kuhofu kwamba DCP inaweza kuwa chama kikubwa kinachotawala vyama vingine vidogo. Kwao, kulazimisha vyama vidogo kuvunjwa hakutaimarisha demokrasia. Kwa Ruto mzozo huo unaweza kuwa faida kubwa. "Viongozi wanaompinga wanapogawanyika nafasi ya kujenga upinzani mmoja wenye nguvu hupungua. Aidha, mivutano ya hadharani inaweza kuwafanya wapigakura wa Mlima Kenya kutokuwa na uhakika kuhusu upande wa kuunga mkono," asema Dkt Lilian Kimani, mchanganuzi wa siasa. Anasema hii inaweza kumpa Ruto nafasi ya kujaribu kurejesha ushawishi wake katika eneo ambalo wapinzani wameanza kujishindia.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.