WIRE โ€” KAUNTI za Mandera, Wajir na Garissa zilishuhudia ongezeko la mashambulizi ya kigaidi mwezi Julai, hali ambayo imewalazimu maafisa wa usalama kutafuta mikakati mipya ya kukabiliana na tishio hilo. Mandera iliongoza kwa kuripoti visa tisa, ikifuatiwa na Garissa ikiwa na visa vinne na Wajir viwili, kwa mujibu wa ripoti ya kijasusi iliyosambazwa kwa maafisa wa usalama katika eneo hilo. Shambulio la hivi majuzi lilitokea Alhamisi usiku ambapo watu 10 walinusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kukanyaga kilipuzi katika barabara ya Takaba-Wargadud-Elwak, Mandera. Tukio hilo lilitokea karibu na kijiji cha Odole saa 12 jioni. Walionusurika walikimbizwa katika Hospitali Ndogo ya Elwak baada ya kujeruhiwa. Mmoja wa manusura alisema walikuwa wakijadili masuala ya siasa za Mandera wakati mlipuko ulipotokea. "Ndani ya sekunde chache kulikuwa kimya. Niligundua damu ikitiririka usoni. Nilikuwa nimekatwa vibaya usoni," alisema. Naibu Kamishna wa Kaunti ya Mandera Kusini, Tobias Otunga alithibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi umeanzishwa. Afisa mmoja mkuu wa usalama alisema kumekuwa na ongezeko la watu wanaoshukiwa kuwa wanachama wa Al-Shabaab kuingia katika jamii za eneo hilo. "Ujasusi wetu umeonyesha kiwango kikubwa cha wapiganaji hao kupenyeza katika jamii zetu. Hili bado ni tishio kubwa kwa usalama wetu," alisema afisa huyo. Ripoti za kijasusi za Julai 31 zilionyesha kuwa wafugaji wanaoishi karibu na mpaka wa Kenya na Somalia waliona watu waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito. Wafugaji hao waliwaambia maafisa wa usalama kuwa wapiganaji hao walikuwa wameanzisha kambi za muda karibu na mpaka na kuwaonya wakazi wasikaribie maeneo hayo. Mnamo Julai 28, washukiwa wa Al-Shabaab waliwavizia maafisa wa usalama waliokuwa katika doria eneo la Quraqura-Wante, Mandera, na kuwaua maafisa watano. Wanne kati ya waliouawa walitoka Kikosi Maalumu cha Operesheni huku mwingine akiwa polisi wa akiba. Kilipuzi kingine kilicholenga kikosi cha maafisa waliokuwa wakija kutoa msaada kililipuka na kuharibu gari la polisi. Shirika la Armed Conflict Location and Event Data (ACLED) limesema ongezeko hilo ni sehemu ya wimbi pana la mashambulizi ya Al-Shabaab katika kaunti za Kaskazini Mashariki na Lamu. ACLED ilirekodi visa 25 vikiwemo vilipuzi viwili vilivyodhibitiwa katika Mandera, Garissa, Wajir na Lamu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Shirika hilo limesema baadhi ya wapiganaji hao wanakimbilia upande wa Kenya kutokana na operesheni kali za kijeshi nchini Somalia. Maafisa wa usalama pia wamehusisha ongezeko hilo na mpaka usio na ulinzi wa kutosha, uajiri wa vijana katika makundi ya kigaidi na mapigano yanayoendelea upande wa Somalia. MCA wa Garissa Hajir Dahiye ameitaka serikali kupitia upya sera yake kuhusu Jubaland, akisema usalama wa Garissa hauwezi kutenganishwa na hali ya usalama katika eneo hilo la Somalia. Mnamo Julai 26, washukiwa wa Al-Shabaab walivamia kijiji cha Abakaile, Dadaab, na kuharibu mnara wa mawasiliano. Hakuna aliyejeruhiwa katika shambulio hilo. Julai 17, washukiwa hao walifanya mashambulizi yaliyofuatana katika miji ya Fino na Arabia, Mandera, na kusababisha hofu miongoni mwa wakazi. Barabara ya Elwak-Lafey-Mandera imekuwa imefungwa kwa umma tangu 2015 kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara na milipuko ya vilipuzi. Maafisa wa usalama pia wameonya kuhusu ushirikiano wa baadhi ya wenyeji na wanamgambo hao kwa kuwapa taarifa kuhusu mienendo ya maafisa wa usalama na vituo vya polisi. Mkazi wa Wajir Hassan Abdullahi alisema ukosefu wa ajira na ujinga miongoni mwa vijana unawafanya kuwa rahisi kuajiriwa na makundi ya kigaidi. "Tunahitaji mpango wa kuwafikia wananchi kutoka mashinani hadi kitaifa ili kuwaelimisha vijana kuhusu hatari za ugaidi," alisema.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.