WIRE โ WANAHARAKATI wa haki za binadamu na wanaotetea wafanyabiashara wa ngono wameonya kuhusu ongezeko la mauaji ya wanawake Eldoret baada ya wanawake wawili kuuawa katika visa viwili tofauti ndani ya siku tano. Visa hivyo vimeibua wasiwasi kuhusu usalama katika nyumba za kulala ambazo wakazi wanasema zimegeuka kuwa maeneo hatari kwa uhalifu. Kisa cha hivi majuzi kilitokea Alhamisi asubuhi katika mtaa wa Kipkaren ambapo mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 26 ulipatikana umefungwa kwenye gunia na kutupwa katika nyumba ya kupanga baada ya waliokuwa wakiishi humo kutoroka. Siku chache kabla ya hapo, mwili wa mwanamke mwenye umri wa miaka 38, aliyetambuliwa na wenzake kwa jina la Zeddy, ulipatikana katika nyumba ya gesti eneo la Juakali, kando ya barabara kuu ya Eldoret-Webuye. Mauaji hayo yameongeza hofu miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono, huku mashirika ya haki yakisema yanaweza kuwa sehemu ya mtindo unaoibuka wa mauaji yanayowalenga wanawake walio katika mazingira hatari. Wakazi wanasema baadhi ya nyumba hizo za kulala wageni hazina rejista za wageni, kamera za usalama wala mifumo madhubuti ya kudhibiti wanaoingia na kutoka. Kiongozi wa Nyumba Kumi eneo hilo, Solomon Musumi, alisema Zeddy alikuwa akiishi katika mojawapo ya vyumba hivyo. Alisema Jumatatu usiku alipokea mwanaume aliyedhaniwa kuwa mteja, kabla ya wanawake waliokuwa katika vyumba vya jirani kugundua mwili wake asubuhi iliyofuata. "Eneo hili haliwezi kuendelea kuwa maficho ya wauaji. Nyumba hizi hazina rejista za wageni wala kamera za usalama, na hivyo kuwa mitego ya kifo," alisema Musumi. Polisi wamethibitisha wameanzisha uchunguzi kuhusu visa hivyo. Kamanda wa Polisi kaunti ndogo ya Kapseret Zaphaniah Kamren alisema washukiwa wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji ya Kipkaren. "Tunaahidi umma kuwa hatutakoma hadi waliohusika na vitendo hivi vya kinyama wakabiliwe na sheria," alisema. Kwa upande mwingine, Kamanda wa Polisi wa Turbo Patrick Wekesa alisema uchunguzi kuhusu kifo cha Zeddy unaendelea.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.