WIRE โ€” RAISย William Ruto anaonekana kufufua baadhi ya mikakati iliyotumiwa na mlezi wake wa siasa hayati rais Daniel arap Moi ya kuimarisha utawala wa mashinani, baada ya kuwatambua rasmi wazee wa vijiji na kuwaingiza katika mfumo wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAO). Hatua hiyo imezua mjadala mpya kuhusu iwapo serikali inalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi au inajenga upya mtandao wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Kwa miaka mingi, machifu, manaibu wao na makamishna wa mikoa walikuwa nguzo kuu ya serikali za Moi. Mbali na kusimamia usalama na utekelezaji wa sera za serikali, walitumiwa pia kuhamasisha wananchi kuunga mkono chama tawala cha Kanu. Lakini mfumo huo ulikosolewa vikali wakati wa harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa miaka ya 1990, huku viongozi wa upinzani wakidai ulitumiwa kuwanyanyasa wakosoaji wa serikali na kuvuruga shughuli za kisiasa. Ingawa Katiba ya mwaka 2010 na ugatuzi ulipunguza mamlaka ya utawala huo, serikali zilizofuata ziliendelea kuuhifadhi kwa kuubadilisha na kuuita Utawala wa Serikali ya Kitaifa. Sasa, miaka 16 baadaye, Rais Ruto ameupanua zaidi kwa kuwaingiza rasmi wazee wa vijiji katika mfumo huo. Akizungumza katika Ikulu ya Nairobi mbele ya zaidi ya wazee wa vijiji 10,000 kutoka sehemu mbalimbali nchini, Rais alisema wazee 106,000 wameingizwa rasmi katika utawala wa mikoa. Alitangaza kuwa kila mmoja wao ataanza kupokea posho ya Sh3,000 kila mwezi, baada ya kuhudumu kwa miaka mingi bila malipo. Aidha, alisema serikali italipia bima yao ya afya kupitia Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA), kuwapatia simu za kisasa za kurahisisha kazi zao na kuongeza maafisa wa Polisi wa Utawala katika maeneo yao. Pia alimwagiza Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, kutenga fedha katika bajeti ya ziada ili serikali ilipie michango ya SHA kwa wazee hao, wake au waume wao pamoja na watoto wao kuanzia Januari 2027. Rais alisema lengo ni kuwapa wazee wa vijiji nafasi rasmi katika utawala wa serikali na kuimarisha ushirikiano wao na machifu, manaibu wa machifu na maafisa wengine wa serikali. Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Raymond Omollo, alisema huo ni uamuzi wa kihistoria kwa sababu ni mara ya kwanza wazee wa vijiji kutambuliwa rasmi na kupewa malipo ya kila mwezi. Alisema hatua hiyo itaimarisha uongozi mashinani, kuongeza uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hata hivyo, mkutano huo uligeuka wa kisiasa baada ya Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Bw Kimani Ichung'wah kuwataka wazee hao kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027. "Mmengoja kutambuliwa kwa miaka mingi. Rais Ruto ametimiza ahadi hiyo. Mkumbukeni na wakati ukifika, muungeni pia," alisema Bw Ichung'wah. Gavana wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, pia alitaka Rais aungwe kwa muhula wa pili, akisema ametambua mchango wa wazee wa vijiji kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Mkuu wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi, alisema serikali itaendelea kuwaunga mkono wazee hao ili kuimarisha usalama na huduma kwa wananchi, huku akieleza kuwa uongozi wa Rais Ruto umeifanya Kenya kuwa na ushawishi mkubwa zaidi barani Afrika. Lakini viongozi wa upinzani walikosoa mpango huo. Kiongozi wa chama cha DCP, Bw Rigathi Gachagua, alisema serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi ambazo hazijatekelezwa. "Aliahidi machifu vipakatalishi lakini mpaka leo hawajazipata. Sasa anawaahidi wazee wa vijiji simu za kisasa. Kwa nini wamwamini?" alihoji. Pia alisema baadhi ya wazee wa vijiji wamemweleza kuwa posho ya Sh3,000 haitoshi kukabiliana na gharama ya maisha. Wachambuzi wa siasa wanasema hatua ya serikali kuimarisha mtandao wa utawala mashinani inaweza kuboresha huduma kwa wananchi, lakini pia inaweza kupatia utawala huo uzito mkubwa wa kisiasa huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.