WIRE โ€” KUNGURUย wavamizi kutoka India, wanaojulikana kwa kuharibu mazingira na kuangamiza ndege wa asili, wameonekana kwa mara ya kwanza jijini Nairobi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wataalamu wa uhifadhi wa mazingira. Ndege hao walionekana awali katika Soko la Burma na mfanyabiashara mmoja aliyewaona akawafukuza bila kujua hatari wanayoweza kusababisha. Hata hivyo, picha yao ilipofikia wataalamu wa uhifadhi, ilithibitisha hofu ambayo wamekuwa nayo kwa miaka mingi. Kunguru hao, wanaojulikana kama Indian house crow, wamekuwa wakisambaa kutoka ukanda wa Pwani na sasa wameingia Nairobi, zaidi ya kilomita 400 kutoka Mombasa. Kwa miaka mingi, wengi walidhani tatizo hilo lilikuwa la Mombasa pekee. Historia inaonyesha kuwa ndege hao waliletwa Zanzibar miaka ya 1890 kusaidia kusafisha taka za chakula bandarini. Walipoongezeka, walivuka hadi Mombasa mwishoni mwa miaka ya 1940 na kuenea haraka katika ukanda wa Pwani kutoka Diani hadi Lamu. Mtafiti wa Makavazi ya Kitaifa ya Kenya, Bw John Musina, alisema kuongezeka kwa idadi yao kuliwaruhusu kusonga kuelekea maeneo ya bara. "Wamekuwa wakifuata miundombinu kama barabara. Walivuka eneo Tsavo, wakafika Makindu na sasa wameingia Nairobi,' alisema. Alisema kunguru hao ni miongoni mwa viumbe hatari zaidi kwa sababu hushindana na ndege wa asili kwa makazi na chakula huku wakivamia viota vyao na kula mayai pamoja na vifaranga. "Wanazaana kwa kasi kubwa kuliko ndege wa hapa, hivyo kuwafanya kupungua," alisema. Kwa mujibu wa Bw Musina, taka zinazotupwa ovyo katika majaa zimekuwa chanzo kikubwa cha chakula kinachowafanya kuongezeka kwa kasi. "Majaa yanawapa chakula kingi. Hiyo huwafanya wazaane kuliko ilivyo kawaida. Ukifika Mombasa utaona jinsi walivyo waharibifu," alisema. Wataalamu sasa wana hofu kuwa iwapo kunguru hao wataenea Nairobi, wataathiri ndege wanaopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Nairobi, ambayo ni miongoni mwa hifadhi chache duniani zilizo ndani ya jiji kuu. Pia kuna wasiwasi kuwa idadi yao inaweza kuongeza hatari ya ndege kugongana na ndege za abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) na Uwanja wa Wilson. Kwa sasa, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya kwa ushirikiano na Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) zimeanza kufanya uchunguzi kubaini idadi ya ndege hao na maeneo waliyotua. Hadi sasa wameonekana katika eneo la Shauri Moyo na Soko la Burma pekee.Musina alisema hatua za mapema zinaweza kuzuia kuenea kwao. "Tunataka kutumia mbinu zilizofanikiwa Mombasa ili kudhibiti idadi yao kabla hawajaongezeka Nairobi," alisema. Kenya pia inachunguza mbinu zilizotumiwa nchini Afrika Kusini na Sri Lanka kudhibiti ndege hao. Hata hivyo, Bw Musina alionya kuwa juhudi hizo haziwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa nchi jirani. "Tukiwadhibiti hapa lakini wasidhibitiwe Tanzania, watarejea tena. Lazima tushirikiane kikanda," alisema.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.