WIRE โ KAUNTI ya Kisii imezindua rasmi Mfumo Mbadala wa Haki wa mazungumzo maarufu kama Alternative Justice System (AJS) katika juhudi za kukomesha mauaji yanayosababishwa na migogoro ya ardhi ambayo imegharimu maisha ya mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni. Jaji Mkuu Martha Koome Jumanne alizindua Kituo cha AJS eneo la Mashauri pamoja na Mahakama ya Manispaa mjini Kisii. Aliandamana na Gavana wa gatuzi hilo Simba Arati, majaji na maafisa wakuu kutoka kwa Idara ya Mahakama. Akizungumza na wazee, mawakili na wakazi wa Kisii, Koome alisema mahakama za kawaida zimelemewa na idadi kubwa ya kesi na haziwezi tena kumaliza migogoro ya ardhi inayochochea mauaji kwa haraka. "Hatuezi kuendelea kuzika wazazi na watoto wetu kwa sababu ya ardhi. Mahakama zimejaa, kesi zinachukua miaka, na familia zinavunjika kabla ya hukumu kutolewa. Ndiyo maana tunawasihi wakazi kuzungumza kwanza kunapotokea migogoro kama hiyo," Koome alisema. Takwimu za vyombo vya usalama zinaonyesha angalau watu saba huuawa kila mwezi Kisii kutokana na migogoro ya mashamba. Kati ya Januari 2021 na Mei 2022, watu zaidi ya 126 walipoteza maisha, kulingana na aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Kisii kwa wakati huo Francis Kooli. Mahakama ya Kisii pia inasema zaidi ya asilimia 80 ya kesi zilizoko mbele yake ni za mauaji yanayotokana na migogoro ya ardhi. Kituo hicho cha AJS kitatumia Baraza la Wazee waliothibitishwa pamoja na wapatanishi wa mahakama kutatua migogoro ya mipaka, ardhi na ugomvi wa kifamilia. Kesi zitachunguzwa ndani ya siku 14. Ikiwa pande zote zitakubaliana, makubaliano yatasajiliwa mahakamani na kuwa na nguvu za kisheria. Ikiwa mazungumzo yatafeli, kesi itarudi mahakamani. Takwimu kutoka kaunti zilizozindua mfumo huo mbadala zinaonyesha kuwa AJS inamaliza baadhi ya ugomvi ndani ya miezi mitatu ikilinganishwa na miaka mitatu mahakamani. Jaji Mkuu alimwomba Gavana Arati kuwasaidia kifedha wazee hao kwa kuwa watakuwa na jukumu kubwa katika kusikiza kesi. Pamoja na AJS, Koome pia alizindua Mahakama ya Manispaa itakayoshughulikia makosa madogo kama kama vile utupaji taka kiholela, kelele na ukiukaji wa sheria za trafiki. Gavana Arati alisema mahakama hiyo itarejesha nidhamu mjini Kisii. "Kwa muda mrefu mji wetu umeteseka na uchafu. Watu wanatupa taka ovyo. Sasa tutakuwa na mahali pa kuwafikisha watupaji hao wa kiholela mara moja," alisema. Arati alidokeza kuwa tayari amezindua timu ya vijana wa kusafisha na kusimamia sheria za mazingira mjini Kisii, ingawa wakazi wamelalamika kuwa timu hiyo "imekuwa ikiwanyasa". "Tukikukamata ukitupa takataka ovyo, hatutakupa onyo. Tutakupeleka mahakamani," alionya. Ugomvi wa ardhi Kisii ni dondasugu. Watoto hawasubiri hata wazazi wao kufa. Baba akiwa mgonjwa tu, ugomvi wa hati ya ardhi unaanza.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.