WIRE โ€” DOUALA, Cameroon: RAIS wa Cameroon Paul Biya Jumanne alifanya mabadiliko makubwa katika uongozi wa jeshi huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu kutokuwepo kwake hadharani kwa muda wa miezi miwili. Kupitia amri tatu za rais zilizotiwa saini Jumatatu na kutangazwa kupitia redio ya taifa, Biya alipandisha cheo mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Rais kutoka kanali hadi brigedia jenerali. Pia aliwateua makamanda wapya katika maeneo manne kati ya matano ya kijeshi nchini humo na kufanya mabadiliko mengine katika uongozi wa vikosi vya jeshi. Mabadiliko hayo pia yalihusisha kuteuliwa kwa kamanda mpya wa Rapid Intervention Brigade (BIR), kikosi maalum kinachohusika na operesheni za kukabiliana na ugaidi na makundi yenye silaha. Aidha, Meja Jenerali Ebaka Hippolyte alipandishwa kuwa afisa mwandamizi katika Makao Makuu ya Jeshi, huku makanali kadhaa wakipandishwa cheo kuwa mabrigedia jenerali. Hatua hiyo imejiri wakati Biya hajaonekana hadharani tangu Juni 7, alipoondoka Cameroon kuelekea Ulaya kwa kile serikali ilichokitaja kuwa "ziara fupi ya kibinafsi". Hata hivyo, hajarejea nchini, jambo lililozua wasiwasi na uvumi kuhusu afya yake na uwezo wake wa kuendelea kuongoza taifa hilo. Msemaji wa serikali, Rene Emmanuel Sadi, alisema Biya yuko hai na anatarajiwa kurejea nchini humo hivi karibuni, lakini hakutoa tarehe rasmi ya kurejea kwake. Kutokuwepo kwa Biya kulisababisha chama tawala cha Cameroon People's Democratic Movement (CPDM) kuitisha kikao kisicho cha kawaida mwezi uliopita ili kujadili hali ya kisiasa nchini humo. Kikao hicho kilifanyika huku shinikizo likiongezeka kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na sehemu ya umma wanaotaka ufafanuzi kuhusu uongozi wa nchi. Biya, 93, ndiye kiongozi mzee zaidi duniani anayehudumu madarakani. Ameiongoza Cameroon tangu 1982 baada ya kumrithi Ahmadou Ahidjo. Katika kipindi hicho, alishinda chaguzi kadhaa ambazo mara nyingi zilikosolewa na wapinzani pamoja na waangalizi wa kimataifa kwa madai ya kukosa uwazi na usawa. Kwa miaka mingi, Cameroon imekabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo uasi wa waasi wa Boko Haram kaskazini, mzozo wa kujitenga katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi, pamoja na malalamishi ya ukosefu wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Biya amekuwa akitumia muda mrefu nje ya ya nchi, hasa Uswisi, kwa mapumziko au ziara binafsi. Hata hivyo, safari yake ya sasa ndiyo ndefu zaidi kuwahi kushuhudiwa, hali ambayo imeongeza mijadala kuhusu mrithi wake na mustakabali wa uongozi wa Cameroon kuelekea uchaguzi ujao.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.