WIRE — WAKAZI wa vijiji vya Lopii, Nakukulas, Lokwamosing, Lokori na Kahuruko katika Bonde la South Lokichar, Kaunti ya Turkana, wanasema sasa wanaishi kwa hofu ya vikosi vya usalama licha ya miaka mingi wakikabiliwa na mashambulizi ya majangili. Wakazi hao wanadai oparesheni kali iliyoanzishwa mwezi uliopita na kikosi maalumu cha polisi imegeuza eneo hilo kuwa kama kambi ya kijeshi. Wanasema magari ya kivita yanazunguka vijijini huku wakazi wakizuiwa kutembea  kwa uhuru, jambo linalozua hofu kuwa serikali inalenga kulinda maeneo ya mafuta badala ya wananchi. Serikali, hata hivyo, inasema oparesheni hiyo inalenga kukomesha wizi wa mifugo na mashambulizi ya majangili. Mfugaji Meshack Etiir wa kijiji cha Lopii alisema wakazi wamekuwa wakitegemea mtandao wa kutoa taarifa za kiusalama ili kubaini watu wanaoshukiwa kushirikiana na majangili. Alisema taarifa hizo zilisaidia kupanga mikakati na Polisi wa Akiba pamoja na maafisa wa utawala ili kukabiliana na mashambulizi. Kwa mujibu wake, familia nyingi zimeendelea kuwa maskini baada ya kupokonywa mifugo huku juhudi za serikali za kurejesha wanyama hao zikikosa kuzaa matunda. Mwakilishi wa Wadi ya Lokichar, Samwel Lomodo, alisema viongozi wamekuwa wakiripoti mashambulizi ya mara kwa mara katika vijiji vya Lopii, Lokwamosing na Nakukulas bila serikali kuchukua hatua za haraka. Alidai kuwa majangili bado wanaendelea kujificha katika maeneo ya Kailongol, Lokwatuba, Lochakula, Lotongot na Loritit licha ya oparesheni ya kuwasaka. Bw Lomodo alisema badala ya vikosi vya usalama kuwafuatilia majangili na kurejesha mifugo iliyoibwa, vinaelekeza nguvu kwa wakazi wasio na hatia. Naye mkazi wa Nakukulas, Mark Epurui, alisema wakazi hawawezi tena kupeleka mifugo karibu na maeneo ya mafuta wala kutafuta taarifa kuhusu nafasi za kazi zinazotarajiwa wakati uchimbaji wa mafuta utakapoanza tena. Kwa upande wake, Eunice Ateyo wa shirika la Friends of Lake Turkana alisema wanaharakati wa haki za binadamu wamebaini hofu kubwa miongoni mwa wakazi kutokana na uwepo wa magari ya kivita. Alidai baadhi ya wakazi wamefurushwa na nyumba kadhaa kuchomwa moto wakati wa oparesheni hiyo. Mwakilishi wa Wadi ya Lokori/Kochodin Willy Napuyo, alisema ikiwa serikali inapanga kutwaa ardhi kwa ajili ya miradi ya mafuta, wakazi wanapaswa kufahamishwa mapema kuhusu fidia na makazi mapya. Hata hivyo, Kamishna wa Kaunti ya Turkana, Julius Kavita, alitetea oparesheni hiyo akisema ilianzishwa baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi. Alisema serikali itaendelea na juhudi za kurejesha mifugo iliyoibwa na kuwakamata wahusika wa mashambulizi hayo.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.