WIRE โ IDADI ya wanaomezea mate wadhifa wa Naibu Rais katika muungano wa kisiasa unaounga mkono Rais William Ruto imeendelea kuongezeka, viongozi wa Orange Democratic Movement (ODM) pia wakitaka nafasi hiyo. Wiki mbili tu baada ya baadhi ya viongozi kumpendekeza Waziri wa Ushirika na Biashara Ndogo na za Kati, Wycliffe Oparanya kuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, sasa kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga, ametangaza hadharani kuwa anataka wadhifa huo. Akizungumza Jumanne katika Ikulu ya Nairobi wakati Rais Ruto alipokutana na wazee wa vijiji kutoka sehemu mbalimbali nchini, Dkt Oburu alisema ODM haitatoa mgombea urais mwaka 2027 bali itamuunga mkono Rais Ruto. "Wakati huu ODM haitakuwa na mgombeaji wa urais. Mgombea wetu ni Rais William Ruto. Lakini nafasi nyingine zote zinaweza kujadiliwa, hasa ya Naibu Rais. Hamuoni kwamba mimi ninafaa kuwa nambari mbili? Mimi pia nina sifa zinazohitajika," alisema Dkt Oburu. Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 82, alisema ODM itaunga mkono azma ya Rais Ruto kutetea urais kwa muhula wa pili. Hata hivyo, alisisitiza kuwa chama hicho, kikiwa miongoni mwa vyama vikuu katika muungano unaotawala, kitajadiliana ili kipate unaibu rais. Dkt Oburu pia alimpongeza Rais Ruto kwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini na kwa uamuzi wa serikali kutoa malipo ya kila mwezi kwa wazee wa vijiji. "Rais anajitahidi. Upinzani nao unapaswa kueleza wananchi sera zao. Je, wangekuwa madarakani, wangewalipa wazee wa vijiji? Sidhani," alisema. Seneta huyo wa Siaya alisema marehemu kaka yake, Raila Odinga, aliacha ODM ikiwa sehemu ya serikali jumuishi na kwamba chama hicho kitaendelea kushirikiana na Rais Ruto. "Marehemu Raila Odinga alituacha ndani ya serikali jumuishi. Hatutamezwa na Rais Ruto bali tutashirikiana kuunda serikali imara," alisema. Kauli zake zinajiri huku Rais Ruto akizidisha juhudi za kuimarisha uungwaji mkono katika maeneo ya Nyanza na Magharibi, kufuatia kuzorota kwa uhusiano wake wa kisiasa na eneo la Mlima Kenya, ambalo lilimuunga mkono kwa kiasi kikubwa katika uchaguzi wa 2022. Wakati huo huo, mjadala kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto umeendelea pia katika eneo la Mlima Kenya. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki tayari ametangaza kuwa ananuia kutetea nafasi yake mwaka 2027. Prof Kindiki amesema eneo la Mlima Kenya linaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto na halipaswi kuacha mradi walioanza pamoja kabla ya kukamilika. Jina la Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru pia limeendelea kutajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania unaibu rais chini ya muungano unaoongozwa na Rais Ruto.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.