WIRE โ MVUTANO wa kisiasa unaendelea kutokota katika eneo la Mlima Kenya na kutishia juhudi za kuunganisha upinzani kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka ujao. Chanzo cha mzozo huo ni matamshi ya aliyekuwa Naibu Rais na kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua kwamba vyama vingine vya Mlima Kenya vivunjwe na viongozi wake wahamie DCP. Kauli hiyo imekosolewa vikali na viongozi kutoka Mlima Kenya Mashariki, ambao wanamlaumu Gachagua kwa kutaka kujitangaza kinara wa eneo hilo. Wakizungumza Jumanne, viongozi wa Democratic Party (DP), Party of National Unity (PNU) na Devolution Empowerment Party (DEP) walimtaka Gachagua kuheshimu uhuru wa vyama vya kisiasa. Kiongozi wa PNU Peter Munya alisema kila chama ni taasisi huru inayolindwa na Katiba. "Hakuna mwanasiasa mwenye mamlaka ya kuamuru chama kingine kivunjwe, kiunganishwe au kuamua mustakabali wake. Huko ni kudharau wanachama na viongozi waliokijenga," alisema Munya. Aliongeza kuwa Katiba inampa kila Mkenya haki ya kuunda au kujiunga na chama chochote cha kisiasa. "Gachagua hana mamlaka ya kisheria wala ya kimaadili ya kuamua hatima ya vyama vingine," alisema. Hata hivyo, viongozi hao walisisitiza kuwa bado wanaunga mkono juhudi za kuunganisha upinzani ili kumng'oa Rais William Ruto mwaka ujao. Walimuonya Gachagua dhidi ya matamshi yanayoweza kuzua migawanyiko. "Tunataka aache kauli za kugawanya watu na badala yake akubali mazungumzo ya kuheshimiana. Miungano ya kudumu hujengwa kwa usawa, imani na heshima," walisema. Viongozi hao pia walikataa madai kwamba Gachagua ndiye msemaji wa Mlima Kenya. "Hakuna aliyempa mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya watu wote wa Mlima Kenya au vyama vya eneo hili," walisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.