WIRE — RAIS William Ruto amewapa wasomi watano mashuhuri jukumu la kuandaa mpango mpya wa maendeleo utakaoongoza Kenya baada ya kumalizika kwa Ruwaza ya 2030, akisema kazi hiyo inahitaji utafiti wa kina badala ya siasa. Badala ya kuwateua wanasiasa au maafisa wa serikali kuandaa ruwaza hiyo, Rais Ruto aliwachagua maprofesa Hiroyuki Hino, Anyang' Nyong'o, Michael Chege, Karuti Kanyinga na Peter Wanyande kuongoza zoezi hilo. Akipokea ripoti yao mnamo Julai 21, Rais aliwashukuru kwa mchango wao katika kuandaa mkakati wa maendeleo wa muda mrefu. "Ninawashukuru tena Profesa Hiroyuki Hino, Profesa Anyang' Nyong'o, Profesa Michael Chege, Profesa Karuti Kanyinga, Profesa Peter Wanyande na wenzao wote walioshiriki katika kazi hii muhimu," alisema. Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed, alisema uteuzi huo ulilenga kuwaleta pamoja wataalamu wa uchumi wa kisiasa, utawala, sera za umma na mipango ya maendeleo ili kutoa mapendekezo yatakayovuka mipaka ya siasa za uchaguzi. Alisema uzoefu wa wasomi hao unatokana na kazi zao katika serikali mbalimbali, taasisi za kimataifa na vyuo vikuu nchini na nje ya nchi. Profesa Hiroyuki Hino Profesa Hino ni raia wa Japan mwenye tajriba ya miongo kadhaa katika masuala ya fedha na maendeleo. Aliwahi kufanya kazi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) tangu mwaka 1975 na baadaye kuwa mkurugenzi wa ofisi yake ya Asia na Pacific. Pia aliwahi kuwa mshauri wa kiuchumi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga wakati wa Serikali ya Muungano. Kulingana na Ikulu, tajriba yake kuhusu mageuzi ya kiuchumi katika mataifa ya Asia kama Korea Kusini, Singapore, China na Vietnam itasaidia Kenya kuandaa mkakati wa kufikia uchumi wa viwanda. Profesa Anyang' Nyong'o Gavana wa Kisumu, Profesa Anyang' Nyong'o, analeta uzoefu mkubwa katika siasa, utawala na taaluma. Baada ya kupata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere, aliendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Chicago alikopata Shahada ya Uzamili na Uzamivu katika Sayansi ya Siasa. Aliwahi kuwa mhadhiri na baadaye profesa katika Chuo Kikuu cha Nairobi pamoja na kufundisha katika vyuo vikuu vya Mexico na Ethiopia. Katika serikali ya Rais Mwai Kibaki, alihudumu kama Waziri wa Mipango na Maendeleo ya Kitaifa na kushiriki katika mageuzi yaliyozaa Ruwaza ya 2030. Profesa Nyong'o anasema ruwaza mpya haikusudiwi kufuta ile ya 2030 bali kuendeleza msingi uliowekwa na mipango ya awali ya maendeleo. Profesa Michael Chege Profesa Michael Chege ni mtaalamu wa utawala bora, uchumi wa kisiasa na ujenzi wa taasisi za serikali. Kwa sasa anafundisha sera za umma katika Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya kuhudumu katika taasisi mbalimbali zikiwemo UNDP, Ford Foundation na Chuo Kikuu cha Florida nchini Amerika. Amefanya pia kazi za ushauri kwa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo Afrika na mashirika mengine ya kimataifa. Ikulu inaamini mchango wake utasaidia kuimarisha taasisi zinazoweza kuendeleza sera za maendeleo bila kutegemea mabadiliko ya serikali. Profesa Karuti Kanyinga Profesa Karuti Kanyinga ni mmoja wa wataalamu wakuu nchini kuhusu ugatuzi, utawala bora, Katiba na sera za umma. Kwa zaidi ya miaka 30 amefanya utafiti kuhusu haki za ardhi, demokrasia, uchaguzi, ushiriki wa wananchi na maendeleo. Akiwa katika Taasisi ya Tafiti za Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Nairobi, ameongoza tafiti nyingi zilizochangia mageuzi ya utawala nchini. Profesa Peter Wanyande Profesa Peter Wanyande anakamilisha timu hiyo. Yeye ni mtaalamu wa utawala wa umma, taasisi za kidemokrasia na usimamizi wa serikali. Mbali na kuwa mhadhiri wa muda mrefu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, aliwahi pia kuwa mshauri wa sera wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga. Kwa mujibu wa Ikulu, kila mmoja wa wasomi hao analeta utaalamu tofauti unaokamilishana. Kwa pamoja, wamekusanya mamia ya miaka ya uzoefu katika kufundisha, kufanya tafiti, kuhudumu serikalini na kutoa ushauri kuhusu sera za maendeleo. Serikali inaamini kuwa mchango wao utaisaidia Kenya kuandaa ruwaza mpya ya maendeleo itakayodumu kwa vizazi na kuendelea kutekelezwa bila kujali mabadiliko ya kisiasa baada ya uchaguzi.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.