WIRE — SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna na washirika wake Jumanne waliendeleza juhudi zake za kusajili Linda Mwananchi kama chama cha kisiasa watakachotumia kuwania urais mwaka 2027. Viongozi wa kundi hilo walikutana kwa faragha na Msajili wa Vyama vya Kisiasa John Cox Lorionokou, wakitaka maelezo kuhusu uamuzi wa kukataa kuhifadhi jina la chama hicho. Baada ya mkutano huo, msemaji wa Linda Mwananchi Caroli Omondi alisema msajili ameahidi kupitia upya uamuzi huo na kutoa msimamo wake kabla ya mwisho wa wiki. "Msajili ametuhakikishia kwamba atapitia upya uamuzi wake na kutupa majibu kabla ya wiki hii kuisha," alisema Omondi. Hapo awali, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) ilikataa ombi la kuhifadhi jina Linda Mwananchi Party of Kenya (LMPK) ikisema linafanana na majina au kaulimbiu nyingine zilizopo kama Linda Mkenya na Boresha Kenya, jambo linalokiuka Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Mkutano huo ulihudhuriwa na Sifuna, Omondi, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Mbunge wa Mavoko Patrick Makau, Mbunge wa Bumula Jack Wamboka, Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo na aliyekuwa Rais wa LSK, Faith Odhiambo. Osotsi alisema waliamua kumuona msajili baada ya mawakili wao kuwasilisha ombi la kuhifadhi jina hilo lakini likakataliwa. "Tulienda kwa msajili kwa sababu tulikuwa tumewaagiza mawakili wetu kusajili jina hilo. Pia tulimtaka afanye uamuzi wake bila kushinikizwa na mtu yeyote," alisema Osotsi. Awali, mwanaharakati Charles Wanyonyi alikuwa ameomba kusajili jina hilo, hatua iliyopingwa na viongozi wa Linda Mwananchi kupitia kampuni ya mawakili ya Henia Anzala and Associates. Kundi hilo lilieleza kuwa kwa miezi kadhaa limekuwa likifanya mikutano na kampeni nchini kote kwa jina la Linda Mwananchi, hivyo jina hilo sasa linahusishwa moja kwa moja na harakati zake za kisiasa. Lilisema kulisajili jina hilo bila ushiriki wake kungechanganya umma kuhusu umiliki na mwelekeo wa vuguvugu hilo. Harakati za Linda Mwananchi zilianza kama kaulimbiu ya kisiasa kupinga kauli ya "Linda Ground" ya kiongozi wa ODM Oburu Oginga, lakini sasa zimekua na kuwa vuguvugu lenye viongozi, mtandao wa waratibu na ajenda ya kuwahamasisha Wakenya kudai uwajibikaji katika utumishi wa umma.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.