WIRE โ€” MPANGO wa Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta wa kufufua muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 umepingwa vikali na baadhi ya vyama vya upinzani, hali inayotishia kuvuruga juhudi za kuunganisha mrengo huo dhidi ya Rais William Ruto. Chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua pamoja na kundi la Linda Mwananchi linalohusishwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, vimesema havina mpango wa kujiunga na Azimio kwa sasa. Viongozi hao wa DCP na Linda Mwananchi wanasema kipaumbele chao ni kuimarisha vyama vyao kabla ya kuanza mazungumzo kuhusu miungano. Katika chama cha Uhuru cha Jubilee, baadhi ya viongozi pia wanapinga mpango huo wakidai unalenga kumpa kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka, nafasi ya moja kwa moja ya kuwania urais kwa tiketi ya upinzani. Chama cha People's Liberation Party (PLP) cha Martha Karua pia kimeibua wasiwasi kikidai kuna njama za kupuuza ripoti ya kamati ya kiufundi ya upinzani iliyoongozwa na Kipruto Kirwa, ambayo ilipendekeza jina jipya la muungano na mfumo wa kugawana nyadhifa za uongozi. Kiini hasa cha mvutano ni kipengele katika katiba ya Azimio kinachomtambua kiongozi wa muungano kuwa mgombea wa urais moja kwa moja. Mnamo Februari mwaka huu, Uhuru alimteua Kalonzo kuwa kiongozi mpya wa Azimio baada ya marehemu Raila Odinga, ambaye alikuwa mgombea wa urais wa muungano huo 2022. Mnamo Jumanne, Kalonzo alikutana na Gachagua pamoja na kiongozi wa DAP-K, Eugene Wamalwa, katika juhudi za kudhibiti migawanyiko inayozidi kujitokeza. Alisema mazungumzo hayo ni sehemu ya mkakati wa kupanua Azimio na kuimarisha umoja wa upinzani. Hata hivyo, vinara wapya wa Azimio akiwemo Justin Muturi, Peter Munya na Lenny Kivuti, walimshutumu Gachagua kwa madai ya kuwashinikiza wavunje vyama vyao na kuhamia DCP. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alisema haelewi kwa nini kuna haraka ya kufufua Azimio, akidai baadhi ya viongozi wamekuwa wakitengwa kwa kumuunga mkono Fred Matiang'i badala ya Kalonzo. "Tunapaswa kuambiwa kwa nini Azimio inafufuliwa sasa. Kalonzo mwenyewe aliwahi kupendekeza ivunjwe. Ningependa kujua kwa nini ghafla kuna haraka ya kuifufua," alisema Kioni. Kwa upande mwingine, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi alisema kundi la Linda Mwananchi linaendelea kujenga umaarufu wa Edwin Sifuna kabla ya kujadili miungano. "Kwa sasa tunajikita katika kuvumisha Linda Mwananchi na kuhakikisha mgombea wetu anatangaza rasmi azma yake ya kuwania urais. Hatusemi kwamba hatuwezi kujiunga na muungano, lakini kwa sasa tunajenga chama chetu na mgombea wetu, " alisema. Mbunge wa Funyula Wilberforce Oundo alisema kundi hilo halijawahi kujadili suala la kujiunga na Azimio. Kwa upande wa DCP, Mbunge wa Gatanga Edward Muriu alisema chama hicho kitawazia kujiunga na Azimio iwapo kutakuwa na mabadiliko makubwa katika muundo na uongozi wa muungano huo. Alisema ODM bado ni mhimili mkuu wa Azimio, jambo linalohitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya mazungumzo yoyote. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru (Mejja Donk) alisema hakuna chama kitakachokubali "kumezwa" na muungano uliopo bila masharti ya usawa. Naye Gachagua aliwaambia wafuasi wake kuwa hakuna mgombea atakayeteuliwa kwa makubaliano ya viongozi pekee. "Hebu kila chama kitafute uungwaji mkono kivyake kwanza. Tusifikirie kuwa tutaketi mahali na kugawana vyeo," alisema. Katika mkutano ulioongozwa na Uhuru Jumatatu, viongozi walikubaliana kupatia Azimio sura mpya na kuwaleta pamoja viongozi wote wa upinzani kabla ya kumteua mgombea mmoja wa kumenyana na Rais William Ruto mwaka ujao. Katika mabadiliko hayo, Fred Matiang'i, Munya na Kivuti walijumuishwa katika baraza la uongozi wa Azimio huku vyama vya Democratic Party (DP), People's Democratic Party (PDP) na Umoja na Maendeleo Party (UMP) vikijiunga na muungano huo. Muturi alisema mkataba wa Azimio unapaswa kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha vyama vyote vinashiriki kikamilifu katika maamuzi, hasa kipengele kinachompa kiongozi wa muungano tiketi ya moja kwa moja ya urais. Katibu Mkuu wa Azimio Caroli Omondi alisema mazungumzo yanaendelea kuwashawishi Gachagua na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga kujiunga na muungano huo. Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha mazungumzo, muungano huo unaweza kubadilisha jina ili kuwavutia washirika wapya na vijana wa Gen Z, huku ukidumisha wafuasi wa Raila Odinga. Mchambuzi wa siasa anayeishi Amerika Profesa David Monda, alisema kufufuliwa kwa Azimio kunaweza kumuinua Kalonzo kisiasa, lakini mafanikio yake yatategemea kama vyama vingine vya upinzani vitakubali kufanya kazi chini ya mwavuli huo.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.