WIRE โ€” ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju yuko mbioni kupoteza mali nyingine ya thamani baada ya Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) kutangaza mnada wa jumba lake la Entim Sidai Wellness Sanctuary lililoko Karen, Nairobi, ili kurejesha deni la Sh4.5 bilioni. Kwa mujibu wa tangazo la kampuni ya mnada ya Garam, mali hiyo itauzwa kwa mnada mnamo Agosti 25, 2026. Jumba hilo liko katika shamba la ekari 20 na lina nyumba ya kifahari ya mtindo wa kikoloni yenye vyumba tisa vya kulala, vyote vikiwa na mabafu ya ndani. Hatua hiyo inajiri miezi michache baada ya mali nyingine ya Bw Tuju kuuzwa kufuatia kushindwa kulipa mkopo aliouchukua kutoka EADB zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Mnamo Mei 21 mwaka huu, Mahakama Kuu ilisimamisha kwa muda mnada wa Entim Sidai kwa masharti kwamba Bw Tuju awe ameweka Sh50 milioni mahakamani kwa muda wa siku 30 na kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo ndani ya siku 60. Kushindwa kutimiza masharti hayo kungeruhusu mnada kuendelea. Hata hivyo, mahakama ilikubali uuzaji wa mali yake nyingine, Tamarind Karen na Dari Business Park, ikisema uhamisho wa umiliki ulikuwa tayari umekamilika mnamo 2024. Mali hiyo ilinunuliwa kwa Sh450 milioni na kampuni ya Ultra Eureka Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara Jackson Kiplimo Chebett, mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Stabex International. Baadaye kampuni hiyo ilitumia hati ya umiliki wa ardhi hiyo kupata mkopo wa dola milioni 2.5 kutoka Benki ya KCB. Bw Tuju aliweka Entim Sidai na mali nyingine kama dhamana ya mkopo wa dola milioni 9.3 (Sh1.2 bilioni wakati huo) aliopata kupitia kampuni yake ya Dari Limited mnamo Aprili 2015. Kutokana na riba, adhabu na gharama nyingine, deni hilo sasa limefikia karibu Sh4.5 bilioni. Bw Tuju amekuwa akidai kuwa EADB ilikiuka makubaliano kwa kushindwa kutoa awamu ya pili ya mkopo wa Sh294 milioni iliyokuwa imekusudiwa kufadhili ujenzi wa nyumba za kifahari za wastaafu mtaani Karen. Kwa upande wake, EADB imesema haikutoa fedha hizo kwa sababu Bw Tuju hakutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha uthibitisho wa maendeleo ya ujenzi na kutoa dhamana ya ziada. Mzozo huo wa kisheria umeendelea kwa miaka kadhaa huku Bw Tuju akijaribu kuzuia kuporomoka kwa himaya ya biashara aliyojenga kwa miongo mingi.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.