WIRE โ RAIS William Ruto Jumapili alipuuzilia mbali wasiwasi unaozidi kushuhudiwa ndani ya muungano wake wa kisiasa, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya UDA na ODM uko imara na utaendelea kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Akizungumza katika ibada na harambee ya Kanisa la St Stephen's ACK, Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu, Rais aliwataka wafuasi wake kutokuwa na hofu kuhusu viongozi wa ODM kujiunga na serikali. "Wanachama wa ODM ni Wakenya na serikali hii ni kubwa na ina nafasi kwa kila mmoja. Hakuna anayepaswa kukasirishwa na uwepo wao serikalini," akasema Rais Ruto. Kauli yake inajiri huku kukiwa na mjadala mkali kuhusu uchaguzi wa 2027, hasa kuhusu nani atakuwa mgombea mwenza wa Rais Ruto. Baadhi ya viongozi kutoka ODM na Magharibi wamekuwa wakitajwa kuwa miongoni mwa wanaowania nafasi hiyo. Matamshi hayo pia yanajiri siku chache baada ya Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kusisitiza kuwa tiketi ya Ruto na Kindiki 2027 haiwezi kujadiliwa. Hata hivyo, Rais Ruto hakuzungumzia moja kwa moja mjadala huo, badala yake alitetea mpango wake wa maendeleo ya Ruwaza ya 2060 na kutangaza kuwa mazungumzo ya kitaifa kuhusu mpango huo yataanza Agosti 12. Alisema Ruwaza ya 2060 italinganisha ajenda ya maendeleo ya Kenya na Katiba ya 2010, tofauti na Ruwaza ya 2030 ambayo iliandaliwa kabla ya katiba hiyo kupitishwa. "Ruwaza ya 2030 iliandaliwa kabla ya Katiba ya 2010. Ruwaza ya 2060 itaweka maendeleo yetu ndani ya misingi ya Katiba. Lengo letu la kuifanya Kenya kuwa taifa lenye ustawi haliwezi kuzuiwa," akasema. Rais pia aliwashutumu baadhi ya wapinzani wake kwa kuendeleza siasa za ukabila, chuki na matusi badala ya kutoa sera mbadala. Akizungumzia ukame uliokumba Bonde la Ufa Kaskazini, Rais alisema hata yeye amepata hasara katika shamba lake kutokana na ukosefu wa mvua. "Mimi pia ni mkulima na nimepoteza mazao kutokana na ukame huu. Serikali itawasaidia wakulima kwa kuwapa mbegu zinazokomaa mapema na pembejeo nyingine ili wanufaike na mvua zijazo na kuimarisha usalama wa chakula," akasema. Aliongeza kuwa serikali inapanga kupunguza gharama za pembejeo za kilimo kabla ya msimu ujao wa upanzi. Kama suluhu ya muda mrefu dhidi ya ukame, Rais alisema serikali itatumia Hazina ya Kitaifa ya Miundombinu kujenga mabwawa 50 makubwa, mabwawa 200 ya ukubwa wa kati na mabwawa 1,000 madogo ili kupanua kilimo cha unyunyuziaji mashamba maji, hasa katika maeneo kame. Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa UDA na ODM, huku wabunge zaidi ya 10 kutoka Bonde la Ufa Kaskazini wakitangaza hadharani kumuunga mkono Rais Ruto kuwania muhula wa pili 2027. Kwa utani, Rais aliwataka viongozi hao kuhubiri Injili kabla ya siasa. "Kabla ya kuhubiri kuhusu muhula wangu wa pili, hubirini kwanza kuhusu kuja kwa mara ya pili kwa Yesu Kristo," akasema. Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen pia alimshambulia aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, akimshutumu kwa kusambaza taarifa za uongo kuhusu usalama wa taifa. Katika harambee hiyo, zaidi ya Sh50 milioni zilichangishwa kwa makanisa ya St Stephen's, St Peter's na St Mark's ACK, huku Rais Ruto akichangia binafsi Sh25 milioni.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.