WIRE โ RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuongoza mkutano muhimu wa Baraza la Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Jumatatu, hatua inayotafsiriwa kama kurejea kwake katika siasa za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Mkutano huo unafanyika huku viongozi wa upinzani wakiharakisha juhudi za kuunda muungano mpana utakaoweza kukabiliana na Rais William Ruto, ambaye washirika wake wanaonekana kuwa mbele katika kujipanga kisiasa. Ajenda kuu itakuwa mustakabali wa Azimio, muungano aliotumia Raila Odinga katika uchaguzi wa 2022. Baada ya kifo cha Raila mwaka jana, Uhuru alimkabidhi kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka jukumu la kusimamia muungano huo. Kalonzo amekuwa akipigia debe muundo unaofanana na ule wa Narc uliomuingiza Mwai Kibaki mamlakani mwaka 2002, ambapo vyama vilihifadhi utambulisho wao lakini vikaungana nyuma ya mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, juhudi hizo zimekumbwa na pingamizi kutoka kwa kiongozi wa Democracy for Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, ambaye amesema hakuna chama kitakachopewa tiketi ya urais kwa makubaliano ya viongozi pekee. "Kila chama kijipigie debe kwa wananchi. Tusifikirie kuwa watu watakaa mahali wagawane nafasi. Hilo halitafanyika," alisema Gachagua. Kwa miezi kadhaa, viongozi wa upinzani wamekuwa wakizungumzia mkutano mkubwa wa kuunganisha makundi yote yanayompinga Rais Ruto, lakini mkutano huo bado haujafanyika kutokana na ushindani wa ndani wa wanaotamani kuwania urais. Seneta wa Makueni Dan Maanzo alisema Uhuru ataongoza mkutano wa Jumatatu ambao utajadili jinsi ya kupanga upya na kupatia Azimio sura mpya kabla ya uchaguzi wa 2027. Anasema vyama kama Wiper, Jubilee, Kanu na washirika wengine vitashiriki, huku pia kukiwa na mazungumzo ya kuingiza makundi mapya kama Linda Mwananchi ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, DCP ya Gachagua na People's Liberation Party (PLP) ya Martha Karua. Wadadisi wa siasa wanasema upinzani unahofia kuchelewa kujipanga Kenya Kwanza ikijiiimarisha kupitia ushirikiano kati ya UDA na ODM. Maanzo alisema lengo ni kuunda muungano utakaowapa nafasi viongozi wapya bila kulazimisha vyama kuvunjwa. "Tunataka muundo mpya unaoweza kuwaleta pamoja wote wanaotaka mabadiliko," alisema. Mchambuzi wa siasa Dismas Mokua alisema uwezekano wa viongozi kuvunja vyama vyao na kuunda chama kimoja ni mdogo sana. "Kilicho rahisi ni muungano mkubwa ambapo kila chama kitabaki kivyake lakini kishirikiane kumpata mgombea mmoja wa urais," alisema. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Multimedia, Profesa Gitile Naituli, alisema changamoto kubwa si jina la muungano bali uwezo wa viongozi kukubaliana kuhusu ajenda ya pamoja. Wakati huo huo, vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Sifuna linazidi kupata nguvu baada ya kufanya mazungumzo na Kalonzo, mgombea wa Jubilee Dkt Fred Matiang'i na viongozi wengine wa upinzani. Vyanzo vinaeleza kuwa vuguvugu hilo linajisajili kuwa chama cha kisiasa ili kushiriki kikamilifu katika mazungumzo ya kuunda muungano mpya. Kulingana na kura ya maoni ya TIFA, Sifuna anaungwa mkono kwa asilimia 15 katika kuwania urais, akimzidi Kalonzo ambaye ana asilimia 13, huku Dkt Matiang'i akiwa na asilimia 14. Kwa pamoja, wagombea wa upinzani wana uungwaji mkono mkubwa kuliko Rais Ruto. Hata hivyo, swali kubwa ni iwapo DCP ya Gachagua itajiunga na muungano huo. Mbunge wa Embakasi Central Benjamin Gathiru, maarufu Mejja Donk, alisema DCP iko tayari kushirikiana lakini haitaki kumezwa na Azimio. "Tunataka ushirikiano unaozingatia nguvu za kila upande. Si majina makubwa pekee bali pia idadi ya wafuasi," alisema. Naibu kiongozi wa DCP Cleophas Malala pia alisema chama kiko tayari kushirikiana na kundi lolote linalotaka Rais Ruto ahudumu kwa muhula mmoja pekee. Kwa upande wake, Martha Karua alipinga wazo la kuunda chama kimoja cha upinzani. "Hatutarudi katika mfumo wa chama kimoja. Katiba yetu inatambua siasa za vyama vingi na hilo halitabadilika," alisema. Ndani ya Jubilee, baadhi ya viongozi wana wasiwasi kuwa kumpa Kalonzo uongozi wa Azimio kunaweza kudhoofisha mgombea wao Dkt Matiang'i. Hata hivyo, Naibu Kiongozi Mwenza Jeremiah Kioni alisema Kalonzo aliteuliwa kwa sababu ndiye alikuwa kiongozi mkuu zaidi aliyesalia ndani ya Azimio. Mkutano wa Jumatatu unatarajiwa kuwa kipimo muhimu cha uwezo wa viongozi wa upinzani kuweka kando tofauti zao na kujenga muungano utakaoweza kutoa ushindani mkubwa dhidi ya Rais Ruto katika uchaguzi wa mwaka 2027.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.