WIRE โ SERIKALI ya China imekanusha vikali madai kwamba imekubali kuiuzia Iran mamia ya mifumo ya ulinzi wa angani, wakati mapigano kati ya Iran na Amerika yakiendelea kushika kasi na kuzua hofu ya kusambaa kwa vita katika eneo lote la Mashariki ya Kati. Wizara ya Ulinzi ya China mnamo Alhamisi ilisema ripoti zilizodai kuwa Beijing inapanga kuipatia Tehran kati ya mifumo 300 na 400 ya ulinzi wa anga ni 'za uongo na zisizo na msingi wowote.' Msemaji wa wizara hiyo, Jiang Bin, alisema China haijahusika katika makubaliano yoyote ya aina hiyo. Kauli hiyo imejiri siku moja baada ya shirika la habari la Reuters kuripoti, ikinukuu durukutoka sehemu tatu zinazofahamu suala hilo, kwamba Iran ilikuwa inatarajiwa kupokea mifumo ya makombora ya QW-12 na FN-16 yenye thamani ya kati ya Sh7.7 bilioni na Sh9 bilioni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, makubaliano hayo yalidaiwa kuhusisha kampuni moja yenye makao yake Hong Kong iliyokuwa ikifanya kazi kama mpatanishi kati ya Iran na China. Duru hizo zilidai kuwa shehena za kwanza zilitarajiwa kusafirishwa kutoka mji wa Urumqi, magharibi mwa China, kupitia Pakistan kuelekea Iran. Hata hivyo, jeshi la Pakistan limekanusha madai hayo, likisema kuwa taarifa zinazodai nchi hiyo inahusika katika usafirishaji huo ni za kubuni. Mvutano huo umeongezeka wakati Amerika ikiendelea na mashambulizi dhidi ya jeshi la Iran. Mnamo Jumatano, ndege za kivita za Amerika zilifanya mashambulizi mapya dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran, huku mapigano yakisambaa hadi maeneo ya pwani ya Misri baada ya shambulizi dhidi ya bandari moja muhimu katika Bahari ya Shamu. Mashambulizi hayo yamezidisha hofu ya kuvurugika kwa biashara ya kimataifa, hasa usafirishaji wa mafuta kupitia Mkondo wa Hormuz na Bahari ya Shamu. Wataalamu wa masuala ya usalama wanaonya kuwa kuongezeka kwa mapigano kunaweza kuathiri usafirishaji wa bidhaa muhimu na kusababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Wakati huo huo, Iran imeendelea kusisitiza kuwa ina haki ya kujilinda dhidi ya kile inachokiita uchokozi wa Amerika na washirika wake. Serikali ya Tehran imeonya kuwa mashambulizi yoyote mapya yatachochea hatua kali za kulipiza kisasi. China, ambayo ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Iran, imeendelea kutaka pande zote kurejea kwenye meza ya mazungumzo badala ya kutumia nguvu za kijeshi. Beijing imeonya kuwa vita hivyo vinaweza kuhatarisha uthabiti wa uchumi wa dunia na kuzidisha migogoro ya kisiasa katika eneo hilo. Licha ya mazungumzo ya kidiplomasia yanayoendelea kupitia Qatar, Oman na Umoja wa Mataifa, hakuna dalili za haraka kwamba mapigano hayo yatamalizika hivi karibuni. Wachambuzi wanaonya kuwa iwapo vita vitaendelea, mataifa mengi zaidi yanaweza kujikuta yakivutwa katika mzozo huo unaotikisa Mashariki ya Kati.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.