WIRE โ€” VIONGOZI wakuu wa upinzani wamekosoa vikali pendekezo la Rais William Ruto la kuanzisha mwongozo mpya wa maendeleo ya taifa utakaofuata Ruwaza ya 2030, wakisema serikali inajaribu kubadilisha mjadala kutoka kwa matatizo yanayowakumba Wakenya kwa sasa. Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kinara wa vuguvugu la Linda Mwananchi Seneta Edwin Sifuna, aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga na viongozi wengine walisema taifa halihitaji mpango mpya kabla ya serikali kutekeleza ahadi ilizotoa na kushughulikia changamoto za gharama ya maisha, ufisadi na utawala. Rais Ruto alitangaza kuwa kuanzia Agosti 12 ataanzisha mazungumzo ya kitaifa yatakayowaleta pamoja wataalamu, viongozi wa kisiasa, wanavyuo, wafanyabiashara, viongozi wa dini, vijana na wadau wengine ili kuandaa mwongozo mpya wa maendeleo utakaoongoza taifa hadi mwaka wa 2060. Kulingana na rais, mwongozo huo utajengwa juu ya mafanikio ya Ruwaza ya 2030 lakini pia utazingatia mabadiliko ya uchumi wa dunia, teknolojia na fursa mpya za maendeleo. Alisema lengo ni kuhakikisha Kenya inakuwa taifa lenye uchumi wa juu na viwanda imara katika miongo ijayo. Lakini Bw Gachagua alisema pendekezo hilo ni mbinu ya kisiasa inayolenga kuwafanya Wakenya wasahau matatizo ya sasa. "Si jambo la kujadiliwa kwamba rais ambaye amezamisha nchi kwenye mzigo wa madeni na anayeshuhudia uchumi ukidorora sasa anataka kutupeleka mwaka 2060. Huu ni udanganyifu wa kiuchumi unaolenga kufufua siasa zake zilizokwama," alisema. "Amekubali kuwa mfumo wake wa ufadhili wa elimu umefeli. Anapaswa pia kukubali kuwa SHA imefeli na ushuru wa nyumba umewaumiza Wakenya. Hata ruwaza hii mpya imezaliwa ikiwa imekufa," alisema. Kwa upande wake, Bw Maraga alisema hotuba ya rais haikugusia suala ambalo, kwa maoni yake, ndilo linazorotesha maendeleo nchini. "Rais hakutaja hata mara moja neno ufisadi. Kenya inapoteza mabilioni ya fedha kila siku kutokana na ufisadi. Zaidi ya Sh1 trilioni hupotea kila mwaka na pesa hizo zinaweza kubadilisha maisha ya Wakenya," alisema. Aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang'i naye alipinga mpango huo akisema serikali haijatekeleza hata mapendekezo yaliyopo, yakiwemo yale ya Kamati ya NADCO. Seneta Sifuna alisema rais hawezi kutenganisha maendeleo na misingi ya Katiba. ย "Katiba inaanza kwa kusisitiza demokrasia, haki za binadamu, uhuru, usawa, utawala wa sheria na haki ya kijamii. Hauwezi kuzungumzia maendeleo bila kuheshimu misingi hiyo kwanza," alisema. Kiongozi wa Democratic Party Justin Muturi alisema Rais Ruto anapaswa kwanza kutoa tathmini ya utekelezaji wa Ajenda ya Mabadiliko ya Uchumi kuanzia mashiani (BETA) kabla ya kuanzisha mjadala mwingine wa maendeleo. "Wakenya bado wanasubiri kuona matokeo ya ahadi za mwaka 2022. Serikali ichapishe ripoti ya mafanikio yake badala ya kubadilisha mjadala," alisema. Aliyekuwa balozi wa Kenya nchini Amerika Elkanah Odembo alisema Kenya haina uhaba wa sera za maendeleo bali tatizo kuu ni utawala mbaya. Kwa mujibu wake, Ruwaza ya 2030 tayari ina mapendekezo mengi mazuri ambayo hayajatekelezwa ipasavyo kutokana na changamoto za uongozi. Naye Mweka Hazina wa ODM Timothy Bosire alisema ufisadi umeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya taifa. Alisema iwapo serikali itadhibiti ufisadi na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa uhuru, Kenya inaweza kufikia maendeleo bila kuhitaji mwongozo mwingine mpya.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.