WIRE โ ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung'u, amemshutumu Rais William Ruto kwa kuingilia utendakazi wa taasisi huru, akisema mtindo huu umezorotesha uwezo wa kutekeleza majukumu ipasavyo. Akizungumza katika mkutano kuhusu misaada nchini Uswizi, Prof Ndung'u alisema taasisi nyingi zina uwezo wa kufanya maamuzi sahihi lakini zinalemazwa na kile alichokitaja kuwa tabia ya mtu mmoja kutaka kudhibiti kila kitu. "Hivi sasa Rais wa sasa anaingilia utendakazi wa taasisi zote. Nendeni mkaninukuu," alisema Prof Ndung'u, akiongeza kuwa maafisa wengi hulazimika kufuata maagizo kwa hofu. Alisema akiwa Waziri wa Fedha alikataa kushiriki mikataba au mipango ambayo haikuwa sahihi. Hii ni mara ya kwanza Prof Ndung'u kuzungumzia hadharani changamoto alizokumbana nazo akiwa serikalini kabla ya kuondolewa katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofuatia maandamano ya Gen Z dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024. Kauli zake zimeibua tena mjadala kuhusu mtindo wa uongozi wa Rais Ruto. Wakosoaji wanasema anapenda kusimamia karibu kila uamuzi wa serikali, huku wafuasi wake wakimtetea wakisema ni kiongozi anayefuatilia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya serikali. Prof Ndung'u pia alikosoa sera ya kuongeza ushuru ili kuimarisha mapato ya serikali, akisema ushuru mkubwa mara nyingi hupunguza mapato badala ya kuyaongeza. Alisema tofauti za kisiasa ndani ya serikali pia zilichangia ugumu wa kusimamia uchumi alipokuwa Waziri wa Fedha.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.