WIRE โ SAA nne na nusu asubuhi, sauti nzito ya kipaza sauti hupenya vilima na mabonde ya South Mugirango, Kaunti ya Kisii, ikitangaza kifo na safari ya mwisho ya marehemu mwili ukipelekwa nyumbani kwa mazishi. Kwa wakazi wengi wa maeneo ya South Mugirango, Bomachoge Borabu na Bomachoge Chache, huu ni utamaduni uliodumu kwa miaka mingi na ambao bado unatumika licha ya kuenea kwa simu za kisasa, WhatsApp na mitandao ya kijamii. Gari dogo lililofungwa vipaza sauti hutangulia gari la kubeba mwili kutoka mochari ya Kisii, huku watangazaji wawili wakitoa taarifa kuhusu marehemu na mahali atakapozikwa. Tangazo la kwanza hutolewa kati ya saa nne na saa sita mchana familia ikielekea kuchukua mwili. La pili, kati ya saa saba na saa tisa alasiri, hutolewa mwili unaporejeshwa nyumbani na ndilo linalovutia watu wengi zaidi. Bw Jared Mobisa, mmoja wa watangazaji maarufu wa mazishi eneo hilo, anasema kazi yao ni kuhakikisha jamii inajiandaa mapema kumpokea marehemu. "Tunatangaza tukielekea mochari na tunaporudi na mwili. Kufikia wakati msafara unafika nyumbani, wanakijiji wote tayari huwa wamekusanyika," anasema. Familia hulipa kati ya Sh3,000 na Sh5,000 kwa huduma hiyo, gharama inayojumuisha mafuta na umeme wa kuendesha mfumo wa sauti. Kabla ya safari, mtangazaji hupewa maandishi yenye taarifa za marehemu. Huyasoma mara kwa mara hadi ayakariri, kisha hutangaza kutoka kijiji kimoja hadi kingine. Kwa wakazi wengi, mfumo huo bado una umuhimu mkubwa. Bi Alice Moraa wa Ogembo anasema bila matangazo hayo wengi wasingejua mwili unarejeshwa nyumbani kwa mazishi. Hata hivyo, kizazi kipya kinaanza kuhoji iwapo desturi hiyo bado inafaa katika zama za kidijitali. Bi Sharon Kemunto, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Moi, anasema kelele za vipaza sauti humvurugia masomo kila kunapokuwa na mazishi. "Wiki iliyopita kulikuwa na mazishi maeneo matatu. Nilishindwa kusoma hadi nikalazimika kwenda Suneka kutafuta sehemu tulivu," anasema. Ingawa anatambua umuhimu wa mila hiyo, anahoji kwa nini familia zisitumie makundi ya WhatsApp au matangazo mengine ya kisasa kuwafahamisha watu. Hata hivyo anakiri kuwa familia yao ilipofiwa na mjomba wake, tangazo kupitia kipaza sauti ndilo lililowakusanya watu wengi. Kwa Mzee Abel Ombongi wa Etago, huo ndio ushahidi kuwa utamaduni huo bado una nafasi yake. Anasema ujumbe wa WhatsApp huhitaji simu za kisasa na mtandao, ilhali tangazo la kipaza sauti humfikia kila mtu bila gharama za ziada. "Katika safari mbili tu kati ya Kisii na Ogembo, maelfu ya watu huwa wamepata taarifa," anasema. Bi Dorcas Kemunto, mzee wa kanisa, anaamini matangazo hayo ni ishara ya heshima kwa marehemu. "Ukisikia kipaza sauti unajua marehemu anarudishwa nyumbani kwa mara ya mwisho. Watu husitisha shughuli zao na kujiandaa kumpokea," anasema. Anasema wazee wengi vijijini hawana simu za kisasa, hivyo hutegemea matangazo hayo kupata habari. Mzee Joseph Menge, 78, anaongeza kuwa huduma hiyo ni nafuu kuliko matangazo ya redio, ambayo yanaweza kugharimu kati ya Sh5,000 na Sh15,000. Lakini si kila mtu anaunga mkono desturi hiyo. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Gusii, Bw James Matundura, anasema vipaza sauti hivyo vimepitwa na wakati na sasa vinachangia kelele. "Leo tuna simu za mkononi na WhatsApp. Hatuna sababu ya kuwasumbua wagonjwa, wanafunzi na watu wanaofanya kazi kwa kelele hizi," anasema. Mjadala huo unaendelea huku baadhi ya wakazi wakisisitiza kuwa matangazo hayo ni sehemu ya utamaduni wao, ilhali wengine wakitaka mbinu za kisasa zitumike bila kuvuruga maisha ya kila siku.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.