WIRE โ ALIYEKUWA Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa, ambaye analenga kuwania ugavana Kilifi, ametangaza kujiondoa katika chama cha United Democratic Alliance (UDA). Hii ni mara ya pili kwa Bi Jumwa kujiondoa UDA. Mnamo Desemba mwaka jana, mwenyekiti huyo wa Bodi ya Barabara nchini (KRB) alitangaza kuondoka UDA na kujiunga na chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi. Hata hivyo, baada ya PAA kutangaza kuwa hakitawasimamisha wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 bali kitaiunga mkono UDA, Bi Jumwa alijikuta njia panda. Baadaye aliendelea na kampeni zake za mashinani chini ya bendera ya UDA akitarajia kupata tiketi ya ugavana, lakini alikumbana na upinzani kutoka kwa viongozi wa chama katika kaunti hiyo ambao waliweka wazi msimamo wao kumuunga mkono Gavana Gideon Mung'aro wa ODM. Akizungumza katika kikao na wanahabari Alhamisi, Bi Jumwa alitangaza kuwa yeye si mwanachama tena wa chama cha Rais William Ruto, akitaja kile alichodai kuwa ni vitendo visivyo vya kidemokrasia vinavyodhoofisha matakwa ya wananchi wa Kilifi. Mbunge huyo wa zamani wa Malindi alisema amefikia uamuzi huo baada ya mashauriano na wakazi wa Kilifi, kutafakari na kufanya maombi. Bi Jumwa, ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa UDA, alisema kuondoka katika chama hicho halikuwa jambo rahisi kwa kuwa alitumia nguvu na kujitolea kukijenga chama hicho. "Kama wengi wenu mnavyojua, mimi ni mmoja wa waanzilishi wa United Democratic Alliance. Kuondoka katika chama ulichosaidia kukijenga si uamuzi mwepesi," alisema. Hata hivyo, alisisitiza kuwa uongozi ni wa wananchi na si wa vyama vya kisiasa au watu binafsi, akisema demokrasia inapaswa kulinda haki ya wananchi kuchagua viongozi wao kwa uhuru. "Uaminifu wangu kwa watu wa Kilifi utakuwa mkubwa siku zote kuliko uaminifu wangu kwa chama chochote cha kisiasa. Sauti ya watu wa Kilifi ni kubwa kuliko sauti ya UDA," alisema. Bi Jumwa alidai kuwa kumekuwa na juhudi za kuzima matarajio na uchaguzi wa wananchi wa Kilifi. Kulingana naye, vitendo hivyo vinakwenda kinyume na misingi ya demokrasia. Aidha, alifichua kuwa aliwasilisha malalamishi yake kwa Rais Ruto, akieleza matumaini yake kuwa haki, usawa na heshima kwa matakwa ya wananchi zitazingatiwa. Bi Jumwa alisema hivi karibuni atazindua chombo kipya cha kisiasa kitakachoendeleza kile alichokitaja kuwa ni ndoto ya pamoja ya kuijenga Kilifi iliyo bora. Aliwahimiza wakazi wa Kilifi kudumisha amani na umoja, akisema harakati hiyo mpya inalenga kuboresha huduma za afya, kuunda nafasi za ajira, kupanua fursa kwa wakulima, kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na kuimarisha uongozi wenye uwajibikaji. Tangazo hilo linaashiria mabadiliko ya kisiasa kwa mwanasiasa huyo mashuhuri wa Pwani huku mipangilio mipya ya kisiasa ikianza kujitokeza kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2027. Mapema wiki hii, kulikuwa na taarifa kuwa alikuwa akifikiria kujiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi. Kujiondoa kwake kulipokewa vyema na wanasiasa wa Linda Mwananchi ambao wamemkaribisha katika upinzani. Bi Jumwa alisema yuko tayari kumenyana na Bw Mung'aro katika uchaguzi wa ugavana wa Kilifi mwaka wa 2027. Kaunti ya Kilifi imeendelea kuwa ngome ya ODM tangu mwaka 2007.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.