WIRE โ RAIS William Ruto anakabiliwa na uamuzi mgumu wa kisiasa na kikatiba kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 kufuatia kufurushwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua madarakani Oktoba 2024. Ingawa Bw Gachagua aliondolewa afisini kupitia mchakato wa bunge, hatua hiyo haikufifisha ushawishi wake kisiasa. Badala yake, ameibuka kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani kupitia chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), ambacho kinaendelea kujijengea ngome katika eneo la Mlima Kenya. Hali hiyo imeongeza shinikizo kwa Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuthibitisha kuwa anaweza kudumisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika eneo hilo kabla ya uchaguzi wa 2027. Gavana wa Murang'a Irungu Kang'ata, amesema Rais atalazimika kufanya uamuzi kuhusu mgombea mwenza wake, akisema nafasi hiyo ni muhimu katika kuvutia kura za Mlima Kenya. "Tatizo kubwa ni kwamba Mlima Kenya unaonekana kuelekea upande wa Gachagua na DCP. Swali ni iwapo Prof Kindiki anaweza kurejesha kura hizo," alisema. Kauli hiyo imejiri huku kukiwa na mjadala kuhusu uwezo wa Prof Kindiki kuimarisha ushawishi wa Kenya Kwanza katika eneo hilo baada ya Bw Gachagua kugeuka mkosoaji mkubwa wa serikali. Hata hivyo, wataalamu wa sheria wanasema Rais hawezi kumuondoa Naibu Rais kwa uamuzi wake binafsi. Wakili Geoffrey Kahuthu, alisema Katiba imeweka utaratibu maalumu wa kumuondoa Naibu Rais kupitia mchakato wa kuondolewa madarakani au kwa misingi ya kutokuwa na uwezo wa kimwili au kiakili. Kwa upande wake, Prof Kindiki amesema hana mpango wa kujiuzulu. "Wanaoniambia nijiuzulu wamekosea. Siwezi kujenga nyumba, niweke samani halafu niende kuishi msituni. Sitajiuzulu," alisema. Kauli hiyo imezua maswali kuhusu hatua ambayo Rais angechukua ikiwa ataamua kuwa anahitaji mgombea mwenza mwingine ili kuongeza nafasi ya kushinda mwaka 2027. Wakili Timothy Kariuki, alisema jaribio jingine la kumuondoa Naibu Rais ndani ya muhula mmoja lingeleta athari kubwa kisiasa. Alisema hatua hiyo ingeonyesha kuwa tatizo si manaibu rais bali ni Rais mwenyewe. Mchambuzi wa siasa Peter Kagwanja, anaamini Rais anaweza kutafuta njia nyingine za kuwapa nafasi viongozi wenye ushawishi badala ya kubadilisha mgombea mwenza. Alisema huenda akaimarisha nyadhifa nyingine serikalini ili kuwavutia viongozi wa kisiasa na kuongeza uungwaji mkono wa muungano wake. Wakati huo huo, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, anaendelea kushinikiza kuundwa kwa muungano wa kisiasa wa "Mlima Kenya Mashariki" unaojumuisha kaunti za Embu, Meru, Tharaka Nithi, Kirinyaga na Isiolo ili kumuunga mkono Rais Ruto na Prof Kindiki. Lakini matokeo ya uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, ambako mgombea aliyeungwa mkono na serikali alipata kura chache, yamezua maswali kuhusu kiwango ambacho serikali inaungwa mkono katika eneo hilo. Mwanasiasa na mchambuzi Gasper Odhiambo, alisema hali ya Prof Kindiki inaonyesha changamoto kubwa ndani ya Kenya Kwanza. Naye Bw Gachagua alisema hali anayopitia Prof Kindiki inafanana na aliyopitia kabla ya kuondolewa madarakani. Alidai kuwa Rais Ruto alimchagua Prof Kindiki ili kuziba pengo lililoachwa alipoondolewa lakini akasema Naibu Rais huyo ameshindwa kurejesha uungwaji mkono Mlima Kenya. Kwa mujibu wa Gavana Kang'ata, Rais anakabiliwa na uchaguzi mgumu. "Akimdumisha Kindiki anaweza kupoteza kura. Asipomchagua, kura chache alizonazo Mlima Kenya zinaweza kutoweka. Akimuondoa, anaweza kuzua mgogoro mpya kuhusu mrithi wake," alisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.