WIRE โ MABADILIKO kwenye kamati za Seneti yamemvua Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na mwenzake wa Vihiga Godfrey Osotsi baadhi ya nyadhifa zenye ushawishi mkubwa bungeni, hatua inayopunguza ushawishi wao wa kusimamia matumizi ya fedha za umma na kupunguza marupurupu yao kwa hadi Sh240,000 kwa mwezi. Mabadiliko hayo yaliyoidhinishwa Jumanne iliyopita yalimuondoa Bw Osotsi kama mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uwekezaji wa Kaunti na Hazina Maalum, wadhifa aliokuwa ameshikilia kwa miaka minne. Sasa atahudumu kama mwanachama wa kawaida wa Kamati ya Biashara, Ustawi wa Viwanda na Utalii. Kwa upande mwingine, Bw Sifuna, ambaye amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa utawala wa Rais William Ruto ndani ya Seneti, aliondolewa kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti (CPAC) na kuhamishiwa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Hatua hiyo imejiri siku chache baada ya kuvuliwa wadhifa wake wa Naibu Kiranja wa Wachache katika Seneti. Mbali na athari za kisiasa, mabadiliko hayo pia yanagusa maslahi ya kifedha ya wawili hao. Akiwa mwenyekiti wa kamati, Bw Osotsi alikuwa akipokea posho ya Sh15,000 kwa kila kikao cha kamati, kiwango ambacho kilikuwa kinaweza kufikia Sh240,000 kwa mwezi, mbali na mshahara na marupurupu mengine ya ubunge. Sasa, akiwa mwanachama wa kawaida wa kamati marupurupu yake yatashuka hadi Sh7,500 kwa kikao, huku kiwango cha juu kwa mwezi kikibaki Sh120,000. Pia atapoteza baadhi ya manufaa yanayotokana na kuongoza kamati yenye jukumu la kusimamia matumizi ya fedha za umma. Maseneta pia hulipwa gharama za safari moja ya kwenda na kurudi kutoka Bunge hadi kaunti wanazowakilisha kila wiki kwa kiwango kilichoidhinishwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), kulingana na umbali kutoka Nairobi. Hata hivyo, wanaohudumu katika kamati zenye majukumu makubwa ya usimamizi hupata nafasi nyingi zaidi za safari za kikazi, ukaguzi wa miradi na shughuli nyingine za uangalizi. Kwa kuondolewa katika kamati hizo muhimu, ushawishi wa Bw Sifuna na Bw Osotsi katika masuala ya uwajibikaji wa serikali za kaunti unatarajiwa kupungua. Kwa miaka minne, Bw Osotsi aliongoza moja ya kamati zenye nguvu zaidi Seneti, iliyokuwa ikichunguza matumizi ya fedha katika mashirika ya kaunti, kampuni za maji, hazina maalum na taasisi nyingine zinazotumia mabilioni ya fedha za umma. Kamati hiyo mara kwa mara huwaita magavana, maafisa wakuu wa kaunti na maafisa wa uhasibu kujibu hoja za ukaguzi zilizotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kama mwenyekiti, Bw Osotsi alikuwa akiongoza shughuli za kamati, kuelekeza uchunguzi na kuidhinisha ripoti ambazo mara nyingi zilikuwa msingi wa mapendekezo ya Seneti kuhusu ufisadi, matumizi mabaya ya fedha na urejeshaji wa pesa za umma. Akizungumza katika kikao cha Seneti Alhamisi, Bw Osotsi alishutumu uongozi wa ODM kwa kile alichokiita mienendo ya kidikteta. "Ikiwa kuna mtu anataka kumwondoa mwanachama katika kamati yoyote ya Bunge, afuate utaratibu wa kuwasilisha hoja rasmi badala ya kuwatisha wabunge kutia saini ombi la kumuondoa mwanachama ambalo sasa linasambazwa," alisema. Nafasi yake sasa imechukuliwa na Seneta wa Taita Taveta Johnnes Mwaruma, ambaye amehamishwa kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti. Kuondolewa kwa Bw Sifuna kutoka Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti nako kunaonekana kuwa pigo kubwa. Kamati hiyo ndiyo huchunguza ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuhusu serikali za kaunti na huwa mstari wa mbele katika kuhoji magavana kuhusu matumizi ya fedha, zabuni, miradi iliyokwama na madeni yanayosubiri kulipwa. Kwa miaka ya hivi karibuni, Bw Sifuna alijijengea sifa kama mmoja wa wanachama waliokuwa wakitoa maswali makali kwa magavana na maafisa wa kaunti kuhusu hoja za ukaguzi. Maswali yake ya moja kwa moja, msisitizo wa kutaka ushahidi wa stakabadhi na ukosoaji wake wa matumizi yenye utata ulimfanya kuwa mmoja wa sauti kuu za upinzani katika kamati hiyo. Kuhamishwa kwake kwenda Kamati ya Kilimo kunamuondoa katika mstari wa mbele wa usimamizi wa fedha za kaunti na kumpokonya jukwaa ambalo amekuwa akilitumia kuikosoa serikali kupitia vikao vya kamati. Mabadiliko hayo pia yamemwingiza Kiongozi wa Wachache Seneti Stewart Madzayo katika Kamati ya Hesabu za Serikali za Kaunti kuchukua nafasi ya Bw Sifuna. Hatua hiyo imezua mjadala iwapo serikali jumuishi inaondoa kwa makusudi wakosoaji wake kutoka kamati muhimu za uwajibikaji ili kuimarisha ushawishi wake ndani ya Bunge. Hata hivyo, Bw Madzayo ametetea mabadiliko hayo akisema ni ya kawaida na yanalenga kuwapa maseneta nafasi ya kuhudumu katika kamati tofauti kwa ufanisi zaidi. "Tumefanya mabadiliko haya kama sehemu ya utaratibu wa kawaida. Yamekuja wakati ambapo hali ya kisiasa imepamba moto, lakini lengo ni kuwapa wanachama nafasi ya kuhudumu katika kamati mbalimbali ili kuboresha utendakazi," alisema. Wachambuzi wa siasa wanaonya kuwa hatua hiyo inaweza kudhoofisha uwezo wa Seneti kusimamia matumizi ya fedha za umma kwa kupunguza idadi ya sauti huru katika kamati muhimu za uwajibikaji.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.