WIRE โ KIFO cha ghafla cha afisa wa polisi Marjori Bosibori kimewaacha wenzake na jamaa wakiwa na maswali mengi huku uchunguzi ukiendelea kubaini kilichotokea katika saa zake za mwisho. Bosibori, mwenye umri wa miaka 42 na aliyekuwa afisa wa mawasiliano katika Kituo cha Polisi cha Kisii Central, alifariki kutokana na jeraha la risasi kifuani ndani ya chumba cha mawasiliano cha kituo hicho. Afisa huyo alirejea kazini Jumanne baada ya mapumziko mafupi nyumbani kwao, Kisii. Aliripoti kazini kama kawaida, akafanya shughuli zake katika duka moja kubwa mjini Kisii, akazungumza na wenzake na hata kushiriki nao chakula cha mchana. Kwa waliokuwa wakifanya kazi naye, alionekana mtulivu, mwenye bashasha na tayari kuendelea na majukumu yake. Hata hivyo, chini ya saa 24 baadaye, alipatikana amefariki ndani ya chumba cha mawasiliano akiwa na jeraha moja la risasi kifuani huku bunduki aina ya AK-47 ikiwa imelala karibu naye. Kifo chake kimewashtua maafisa wenzake na familia yake. "Aliripoti kazini kama kawaida yake. Hatukushuku chochote. Bado siamini kilichotokea," alisema mmoja wa maafisa aliyekula naye chakula cha mchana siku hiyo. Afisa mwingine alisema Bosibori alikuwa mtu mtulivu na aliyependa kuweka siri maisha yake ya kibinafsi, hali iliyofanya iwe vigumu kubaini alipokuwa akikabiliwa na changamoto. Marafiki zake pia wanamkumbuka kama shabiki mkubwa wa klabu ya Manchester United. Polisi wanachunguza uwezekano kuwa alijitoa uhai, ingawa wanasema bado hawajabaini kilichotokea katika saa zake za mwisho. Kamanda wa Polisi wa Kisii Central, Musa Imamai, alisema Bosibori alimaliza shughuli zake katika duka hilo kabla ya kurejea kituoni muda mfupi baada ya saa sita usiku akiwa na mwenzake. Walipofika kituoni, alimwambia mwenzake kuwa anaelekea chooni. Mwenzake hakushuku chochote. Badala yake, wachunguzi wanaamini aliingia katika chumba cha mawasiliano, ofisi yenye ulinzi mkali ambayo haitumiki sana wakati huo wa usiku, akajifungia kutoka ndani na hakutoka tena. Ilikuwa hadi Jumanne asubuhi afisa mwingine aliporipoti kazini ndipo iligundulika kuwa mlango wa chumba hicho ulikuwa umefungwa kwa muda mrefu. Baada ya juhudi za kuufungua kugonga mwamba, maafisa walivunja mlango. Ndani walimkuta Bosibori ameketi kwenye kiti bila uhai akiwa na jeraha la risasi kifuani huku bunduki ya AK-47 ikiwa sakafuni karibu naye. "Tulimkuta akiwa ameketi na damu ikitoka kwenye jeraha la risasi. Uchunguzi wa awali unaonyesha alipigwa risasi moja kifuani na risasi hiyo ikatokea mgongoni," alisema Bw Imamai. Tukio hilo liliwaacha hata maafisa wenye uzoefu mkubwa wakiwa na mshtuko. Polisi walipata bunduki hiyo, ganda moja la risasi, magazini yenye risasi 29, ufunguo wa ofisi, simu tatu za mkononi na dawa mbalimbali. Bosibori alikuwa bado amevaa sare zake za polisi. Bw Imamai alisema alikuwa miongoni mwa maafisa wachache walioaminiwa kufanya kazi katika chumba cha mawasiliano kutokana na nidhamu na uadilifu wake. "Hii ni ofisi muhimu na ni maafisa wachache pekee wanaoruhusiwa kufanya kazi humo. Bosibori alikuwa mmoja wao," alisema. Aliongeza kuwa wachunguzi wanachunguza kila upande wa maisha yake, ikiwemo iwapo kulikuwa na matatizo ya kifamilia au ya kibinafsi ambayo huenda yalichangia mkasa huo. "Kufikia sasa hatuna fununu zozote kuhusu kilichosababisha kile kinachoshukiwa kuwa kujiua kwake," alisema. Mwili wake ulihamishwa hadi mochari ya Hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii ambako unatarajiwa kufanyiwa uchunguzi kubaini chanzo kamili cha kifo.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.