WIRE โ MAHAKAMA Kuu jijini Nairobi imekataa ombi la kuahirisha Uchaguzi Mkuu wa 2027 hadi Katiba ya 2010 ifanyiwe marekebisho makubwa, ikiwemo kutathmini mihula ya viongozi na kuundwa kwa afisi ya Kiongozi wa Upinzani yenye mamlaka ya kutathmini utendakazi wa serikali. Jaji Patricia Nyaundi aliamua kuwa mabadiliko ya Katiba hayawezi kufanikishwa kupitia mahakama bali lazima yafuate taratibu zilizowekwa na Katiba. Alisema mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa sababu mlalamishi hakufuata njia halali za marekebisho ya Katiba. Kesi hiyo iliwasilishwa na Bernard Mwanzia dhidi ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Mwanasheria Mkuu, Spika wa Bunge la Kitaifa na Spika wa Seneti. Bw Mwanzia alitaka maandalizi ya uchaguzi wa 2027 yasimamishwe akidai Katiba ya sasa ina mapungufu yanayodidimiza umoja wa kitaifa, utawala bora na uthabiti wa uchumi. Alidai kuwa masuala kama mpangilio wa uchaguzi, mihula ya viongozi kuhudumu, matumizi ya lugha za mama katika mabunge ya kaunti, uwakilishi wa viongozi waliochaguliwa, kuhifadhi utamaduni wa Kenya na haki ya maandamano yanahitaji kufanyiwa marekebisho kabla ya uchaguzi mwingine kufanyika. Iwapo ombi hilo lingefaulu, maandalizi yote ya uchaguzi mkuu yangesimamishwa hadi kukamilika kwa mchakato wa marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, IEBC ilipinga kesi hiyo ikisema Katiba tayari imeweka utaratibu wa kuifanyia marekebisho kupitia Bunge au mpango wa kuwashirikisha wananchi. Jaji Nyaundi alikubaliana na hoja hiyo akisema mlalamishi alikimbilia mahakamani kabla ya kutumia njia zinazotambuliwa kikatiba. "Katiba imeweka njia ya wazi, ya kipekee na inayojitekeleza ya kuifanyia marekebisho, na utaratibu huo lazima uheshimiwe," akasema. Bw Mwanzia pia alikuwa akipendekeza kuanzishwa kwa afisi ya Kiongozi wa Upinzani iliyo na mamlaka ya kutathmini utendakazi wa serikali, kupitia upya mfumo wa ugatuzi na uwakilishi bungeni.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.