WIRE — TANGU akiwa kijana mdogo Francis Karanja alivutiwa na shughuli ya kufuga sungura. Alipokuwa darasa la tano alimpa mamake, Rachel Chebet, ombi moja: amnunulie sungura kadha afuge ili aboreshe somo lake la kilimo katika mtaala mpya wa elimu ya umilisi na utendaji (CBE). Mamake akaahidi kumnunulia baadaye kwani mahali walipoishi wakati huo hapakuwa na nafasi kubwa ya kufanya ufugaji wowote. Mwaka 2024 Chebet alinunua mabati, mbao, nyaya za kuweka ua, misumari na vifaa vingine akajenga vyumba vidogo tisa vya sungura kwa gharama ya Sh10,000. Pia alinunua sungura wanne - ndume wawili na jike wawili kwa Sh500 kila moja. Karanja, 15, ambaye sasa yuko darasa la nane katika shule ya Michinda mjini Elburgon, Kaunti ya Nakuru, asema ilikuwa furaha tele mama alipomtimizia ombi lake. "Sungura walinunuliwa wakati wa likizo na hilo lilinipa fursa nzuri ya kuwatunza," aeleza. [caption id="attachment_190590" align="alignnone" width="2560"] Francis Karanja, 15, mwanafunzi wa Gredi ya Nane katika shule ya Michinda, Elburgon ambaye ni mfugaji sungura. Picha|John Njoroge[/caption] Baada ya miezi mitatu sungura mmoja alizaa wana watano na mwingine saba. Karanja anapokuwa shuleni mamake ndiye huchukua jukumu la kutunza sungura hao. Pia wanakusanya mkojo na kinyesi cha mifugo hao kutengeneza mbolea asili ili kutumia katika shamba lao dogo la nyumbani. Mkojo wanakusanya takriban lita 10 hadi 20 kila wiki. Bidhaa hii ina nitrojeni nyingi na ni kiungo bomba katika kuunda mbolea asilia, na huuzwa kama andazi moto. Hivyo, baada ya kumimina kiwango wanachohitaji kuunda mbolea asili yao, mkojo ambao husalia wanawauzia wakulima wa eneo hilo Sh70 kila lita. Kipindi cha ujauzito cha sungura huwa kati ya siku 28 na 35. Hata hivyo, Chebet na mwanawe wameweka ratiba ili kwamba sungura wa kike anajamiiana na ndume baada ya miezi mitatu, ili kuzuia wana wengi kuzaliwa kila mara hasa wakati wa kiangazi ambapo ni vigumu kupata lishe yao ya kutosha. Mbali na kuuza mkojo, Karanja anasema wao pia huchinja sungura hao kupata nyama. "Baada ya muda fulani sungura wakiongezeka kuwa wengi sana hasa wakati wa kiangazi malisho yakididimia, mama huchinja kadha tunatumia kutengeneza mchuzi nyumbani. Mchuzi wa nyama ya sungura ni mtamu sana," aeleza kwa itabasamu. Kwa mujibu wa afisa wa mifugo eneo la Kuresoi Kaskazini, Nicholas Rono, ufugaji sungura ni tija tosha. Mfugaji anahitaji tu kuhakikisha amejenga vyumba vizuri vya malazi, vinasafishwa kila wakati na kuzuia unyevunyevu kwani huleta magonjwa kama vile nimonia ambayo husababishwa na baridi. "Sungura pia huvamiwa na utiriri kwenye kichwa, mapua na masikio, tatizo ambalo hufanya wajikune sana kwenye ngozi na kuwaletea mwasho mkali. Kuna dawa ya unga ambayo wafugaji wanahitaji kupaka sehemu hizo ili kuzuia tatizo hilo," aeleza Rono. Anaongeza kuwa lishe ya sungura inafaa kuwa bora yenye virutubisho kamili na kiwango cha kutosha, hasa kwa vijike waliojifungua kwani baadhi hugeuka kula wanawao wakilemewa na njaa. Karanja huuza sungura wake kwa ajili ya ufugaji au nyama. Sungura aliyekomaa huwa kati ya Sh500 na Sh700 kulingana na saizi, na Sh300 kwa mwana wa sungura. "Ninatumia pesa hizo kuongeza lishe, na senti zinazosalia ninanunua vifaa vyangu vya shule. Kielimu mradi huu umefanya somo la kilimo kuwa kati ya zile ninazopenda zaidi shuleni," asema. [caption id="attachment_190591" align="alignnone" width="2560"] Kijana Francis na mamake Rachel Chebet wakikusanya mkojo wa sungura ulio na soko bomba ambapo lita moja huuzwa Sh70 sokoni. Picha|John Njoroge[/caption] Sungura hawana misimu pevu au kavu hivyo mfugaji hupata mauzo wakati wowote kulingana na hitaji la soko. Katika hatua ya kukuza ujuzi wa usimamizi wa biashara, anadokeza kwamba kwa usaidizi wa mamake wanaweka kila siku kumbukumbu za taarifa za ufugaji wa sungura wao kila siku. Ili kusawazisha kazi ya shule na mradi wake wa sungura, Karanja ana ratiba ya kibinafsi ili kufanya mambo kwa mpangilio na urahisi. Kwa sasa ana zaidi ya sungura 100 huku lengo likiwa kufikisha zaidi ya sungura 600 ifikapo Desemba. "Tamanio langu ni kufuga sungura zaidi ili kuvuna mkojo ya kuunda mbolea asili ya kutosha kukidhi mahitaji ya wakulima msimu wa upanzi, hasa katika kilimo cha viazi na mboga," asema. Mamake asema sio tu manufaa ya kifedha wanapata kutoka kwa mradi. "Ufugaji pia umemfunza maadili ya nidhamu, uwajibikaji na kumzuia kutangamana na vijana watundu kwani huwa ana shughuli nyingi za kufanya anaporejea jioni kutoka shule au wakati wa likizo," aeleza Chebet.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.