WIRE — SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna anaendelea kutamba katika ulingo wa siasa. Nyota yake Sifuna inaendelea kung'aa kwenye ramani ya humu nchini kwa mwendokasi wa ajabu. Sifuna ni mwanafunzi mmakinifu wa siasa za watangulizi wake Raila Amollo Odinga na kigogo wa siasa Michael Kijana Wamalwa ambao walionyesha umahiri hata katika wimbi kali la upinzani. Baada ya kubanduliwa katika wadhifa wa katibu mkuu wa chama cha ODM, Seneta Sifuna hajafa moyo. Ufuasi wake Unaendelea kushamiri huku akifanikiwa kupata kibali katika kila eneo analozuru nchini. Hili linashuhudiwa kupitia umati wa watu wanaojitolea kuhudhuria mikutano anayoandaa pamoja na wenzake katika mrengo wa Linda Mwananchi. Safari yake Sifuna katika siasa ni sura ya siasa ya aliyekuwa waziri mkuu na kinara wa ODM Raila Odinga. Raila ndiye mwanasiasa wa pekee aliyelipinga wimbi la chama kikuu cha upinzani cha FORD katika mwaka wa 1994 na baadaye kujiuzulu. Raila alithamini demokrasia na nguvu za wananchi zaidi ya nguvu za dola. Sifuna amehitimu katika chuo cha mwamba aliyegundua kuanza mapema akiwa na nguvu na mvuto kwa wananchi. Hulka yake seneta huyo inachukuliana na yake Kijana Wamalwa ambaye alipendwa na wengi wa wapigakura katika ukanda wa magharibi. Ni wazi kuwa Sifuna ni mmoja wa viongozi walioweza kuwavutia wananchi wengi zaidi kisiasa katika eneo la Magharibi. Siasa yake inatikisa ngome za wanasiasa wakongwe wakiwemo Musalia Mudavadi, Moses Wetang'ula, Wycliffe Oparanya na wengine. Mvutano kati ya Raila na Wamalwa ulichangia FORD Kenya kusambaratika baada ya Jaramogi Oginga kufariki dunia. Raila alionekana kama aliyetaka kurithi chama naye Wamalwa akitaka kuwa kiongozi wa chama hicho. Hatimaye Ford Kenya iligawanyika mara tatu. Hii ndiyo njia ya chama cha ODM baada ya Raila kuondoka. Sharti Sifuna ajichongee kao lake la siasa kwa nyakati zijazo akifahamu kuwa ufuasi na ushabiki humwandama mtu jasiri anayejijengea chama chake. Raila aliviunda vyama kadhaa kama silaha yake dhidi ya serikali. Ni bayana kuwa Sifuna yuko njiani kukiunda chama chake. Tukielekea katika uchaguzi mkuu wa 2027, Sifuna ana nafasi murua ya kujinadi kupewa fursa ya kugombea kiti cha urais au kumpiga pambaja mgombea mwingine kuwania kiti hicho. Kibarua kikubwa ni kuwa kuna wanasiasa wa upinzani ambao huenda hawatampa nafasi hiyo kwa madai ya kukosa tajriba ya kisiasa. Kinachobakia ni kujijenga kisiasa wala si kutafuta ushindi wa kiti cha urais. Kadi yake Sifuna kama mgombea wa urais ni bora hasa kwa ushawishi alio nao kwa vijana na wananchi wanaotaka mabadiliko. Hata hivyo, haijadhihirika iwapo viongozi katika upinzani watakubali kumuunga mkono ama ukosefu wa umoja katika upinzani utalemaza uwezo wake. Sifuna hana la kupoteza upinzani ukishinda au ukikosa kushinda urais. Atakuwa ameuboresha msingi wake wa kisiasa kwa siku za usoni.

"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."

This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.