WIRE โ BARAZA la Chuo Kikuu cha Kenyatta jana lilimteua Profesa John Okumu kuwa Naibu Chansela wa chuo hicho baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa kuajiri ulioendeshwa na Tume ya Utumishi kwa Umma (PSC). Uteuzi huo ulitangazwa Jumatatu kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Profesa Clara S. Momanyi, ambaye alisema uamuzi huo ulifanywa kwa mujibu wa Sheria ya Vyuo Vikuu na kwa idhini ya Waziri wa Elimu. Profesa Okumu anafahamu vyema Chuo Kikuu cha Kenyatta kutokana na kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa miaka mingi. Aliwahi kuwa Naibu Chansela anayesimamia Masuala ya Kitaaluma kwa miaka 10, pamoja na kushikilia nyadhifa nyingine za juu za usimamizi. Baraza lilimsifu kama msomi na msimamizi mwenye tajriba kubwa katika uongozi wa elimu ya juu, utafiti na maendeleo ya taasisi. Prof Momanyi alisema ana imani kuwa tajriba na uwezo wa Profesa Okumu katika kupanga mikakati, kusimamia taasisi na kushirikiana na wadau utasaidia kuimarisha maendeleo ya chuo hicho. "Tunamkaribisha Profesa Okumu katika nafasi hii muhimu na tunatoa wito kwa wanajamii wote wa chuo na wadau kumpa ushirikiano anaohitaji ili atekeleze wajibu wake na afanikiwe," akasema. Profesa Okumu alikuwa akishikilia wadhifa huo kwa muda tangu mwishoni mwa Januari 2026 baada ya kumrithi Profesa Paul Wainaina, aliyestaafu baada ya kuhudumu kwa miaka minane. Katika mahojiano yaliyofanywa na PSC, Profesa Okumu alipata alama 84.5, akiwashinda Profesa Stephen Odebero na Profesa Godfrey Mse. Hata hivyo, uteuzi huo ulikumbwa na changamoto za kisheria baada ya Profesa Waceke Wanjohi, Naibu Chansela wa Masuala ya Kitaaluma na mmoja wa waliowania wadhifa huo, kufikisha kesi Mahakama Kuu akidai ndiye aliyepata alama za juu zaidi na kwamba aliondolewa isivyo haki. Mnamo Aprili, Jaji Njoki Mwangi alitoa amri za muda zilizokizuia chuo kujaza nafasi hiyo hadi kesi hiyo isikizwe, huku pia akiamuru mkataba wa Profesa Wanjohi uongezwe. Mvutano huo uliibua sintofahamu kuhusu hatima ya nafasi hiyo kwa miezi kadhaa kabla ya Baraza la Chuo kuthibitisha rasmi uteuzi wa Profesa Okumu. Uteuzi huo unatarajiwa kuleta utulivu katika uongozi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta na kuweka msingi wa utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.