WIRE โ UKOSEFU wa ajira unaozidi kushuhudiwa nchini umeanza kuwasukuma vijana wengi kuingia katika biashara haramu huku baadhi wakitumbukia kwenye mitandao ya utengenezaji wa filamu za ngono zinazouzwa kwa wateja wa mataifa ya kigeni. Katika mwezi mmoja uliopita pekee, maafisa wa polisi wamevamia nyumba kadhaa katika kaunti za Kiambu, Nairobi, Kajiado na Nakuru na kuwaokoa zaidi ya wanawake 50 waliokuwa wakidaiwa kulazimishwa kutengeneza filamu za ngono. Hii ni baada ya kudanganywa kwa ahadi za ajira zenye mishahara minono. Wiki nne zilizopita, polisi walivamia nyumba moja eneo la Ngoigwa, Thika, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wakazi. Vijana kadhaa wenye umri wa kati ya miaka 18 na 30 walikamatwa wakishukiwa kutengeneza filamu za ngono zilizokusudiwa kuuzwa katika masoko ya nje ya nchi. Polisi walinasa kompyuta, kamera na vifaa vingine vilivyokuwa vikitumiwa kurekodi filamu hizo. Miezi michache kabla ya hapo, maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) walivunja mtandao mwingine jijini Nakuru baada ya kuvamia sherehe ya ngono katika eneo la Naka Estate. Mfanyabiashara mmoja alikamatwa akishukiwa kuwavutia vijana, wakiwemo wasichana wa shule wenye umri wa miaka 13 hadi 17, kushiriki katika kurekodi filamu ya ngono zilizokuwa zikununuliwa barani Ulaya. Mnamo Julai 21, DCI iliwaokoa wanawake watano waliokuwa wakizuiliwa katika nyumba moja eneo la Mihang'o, Embakasi Mashariki, Nairobi. Uchunguzi ulionyesha kuwa walikuwa wameahidiwa kazi zenye mishahara mizuri lakini badala yake wakalazimishwa kutengeneza filamu ya ngono kwa ajili ya biashara ya mtandaoni. "Waathiriwa walidanganywa kwa ahadi za ajira zenye mapato mazuri lakini wakageuzwa watumwa wa kutengeneza filamu ya ngono kwa manufaa ya biashara," akasema Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin. Siku tatu baadaye, polisi waliwaokoa wanawake wengine 48 katika maeneo ya Ongata Rongai na Kiserian, Kaunti ya Kajiado, walikokuwa wakishikiliwa na magenge mawili yanayoshukiwa kujihusisha na biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu na unyanyasaji wa kingono. Moja ya nyumba hizo ilikuwa imegeuzwa studio ya kisasa ya kamera za mtandaoni yenye kompyuta, kamera na vifaa vya kurusha matangazo ya moja kwa moja kwa wateja wa ng'ambo. Kwa mujibu wa wachunguzi, magenge hayo huwavutia vijana wasiokuwa na ajira kwa matangazo ya kazi kama watayarishaji wa filamu, wapiga picha, wanamitindo, wasaidizi wa masoko ya kidijitali au wafanyakazi wa nyumbani. Wakishakubali kazi hizo, huzuiliwa katika nyumba za kupanga na kulazimishwa kushiriki katika biashara hiyo haramu. "Magenge haya yanatumia ukosefu wa ajira na ugumu wa maisha kama silaha. Vijana huahidiwa mishahara mikubwa, safari za nje ya nchi na nafasi za kazi, lakini baadaye hulazimishwa kutengeneza filamu za ngono," akasema afisa mmoja mkuu wa DCI aliyeomba kutotajwa. Maafisa wa upelelezi pia wamebaini kuwa baadhi ya washukiwa hutuma fedha kupitia simu au zawadi za thamani ili kujenga uaminifu kwa waathiriwa kabla ya kuwalazimisha kutuma picha na video za ngono. DCI imesema mitandao hiyo sasa inaendesha shughuli zake katika miji ya Nairobi, Nakuru, Kisumu, Eldoret na Thika. Imetoa wito kwa vijana kuwa waangalifu wanapotafuta ajira na kuhakikisha wanathibitisha waajiri kabla ya kukubali ofa yoyote.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.