WIRE — Bondia wa Kenya Jane Kavulani ametuma onyo kali kwa mpinzani wake Roman Asefa Abate wa Ethiopia akiahidi kumwangusha kwa kushinda kwa 'Knockout' yaani KO katika raundi za kwanza, watakapokutana katika mashindano ya ndondi yatakayofanyika Jumamosi hii kwenye ukumbi wa Edge Convention Centre jijini Nairobi. Kavulani, anayefanya mazoezi katika ukumbi wa Pal Pal Gymnasium uliopo Gikomba jijini Nairobi, alisema amejiandaa vya kutosha na hana shaka ya kuibuka mshindi dhidi ya Methiopia huyo ambaye atakuwa akicheza pambano lake la kwanza la kulipwa. "Nimefanya maandalizi ya kutosha. Lengo langu ni kumaliza pambano mapema kwa KO na kuwapa mashabiki ushindi wa kujivunia," alisema Kavulani. Hata hivyo, Asefa naye ameonyesha kujiamini akisema ananuia kuanza maisha yake ya ndondi za kulipwa kwa ushindi na kurejea Ethiopia akiwa ameshinda pambano lake la kwanza. Zaidi ya mapambano hayo ya wanawake uzani wa featherweight, mashabiki watashuhudia jumla ya mapambano 11 kwenye usiku huo wa ngumi uliofadhiliwa na SportPesa na kuandaliwa na promota Maurice Odera kupitia kampuni ya UFS BXNG. Pambano kuu la usiku litamshuhudia bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki Javan Buyu akipambana na Ramadhani Idd wa Tanzania kuwania taji la Universal Boxing Organisation (UBO) Inter-Continental Lightweight katika pambano la raundi 10. Buyu anatarajiwa kutumia uzoefu wake mbele ya mashabiki wa nyumbani huku Idd akinuia kuvuruga mipango ya Mkenya huyo kwa kutwaa taji hilo na kuliondoka nalo Tanzania. Buyu, ambaye ni bingwa wa Kenya na Afrika Mashariki, ana nafasi ya kutwaa taji lake la tatu la kulipwa na kuwa miongoni mwa mabondia wachache wa Kenya kushinda mkanda wa ngazi ya mabara. Bondia huyo amesema yuko tayari kwa mtihani huo baada ya kufanya maandalizi ya miezi mitatu bila kuacha jambo lolote kwa bahati. "Nimekuwa nikifanya mazoezi na kumuomba Mungu kwa ajili ya taji hili. Mimi na timu yangu tumefanya kazi kubwa kujiandaa kwa Julai 25 na tuko tayari. Tumeimarisha kila eneo muhimu litakalotupa ushindi," alisema Buyu. Buyu alitwaa ubingwa wa Kenya Oktoba mwaka jana baada ya kumshinda Christopher Osicho kabla ya kuongeza mkanda wa PST kwa kumcharaza Mtanzania Nasoro Madimba kwa Technical Knockout katika raundi ya tatu mapema mwaka huu. Amesema tayari amemchunguza Ramadhani kupitia video zake. "Ni bondia mzuri, ningempa alama saba kati ya 10, lakini nina kila kitu kinachohitajika kumlazimisha akate tamaa. Namwahidi pambano zuri, lakini aandae moyo wa kukubali kushindwa," alisema.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.