WIRE โ ALIYEKUWA Gavana wa Migori, Okoth Obado, Michael Oyamo na Caspal Obiero wameanza maisha mapya gerezani baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mwanafunzi Sharon Otieno, kukikabiliana na utaratibu mkali wa maisha ya wafungwa. Watatu hao wataishi maisha anayopitia kila mfungwa bila kujali hadhi yake. Watatu hao walipelekwa katika Gereza la Mahabusu la Industrial Area Alhamisi jioni, lakini walikuta chakula cha jioni tayari kimekwisha. Wafungwa walikuwa wamemaliza ugali na maharagwe yaliyokuwa yameandaliwa, hivyo wakalazimika kulala bila chakula cha gerezani siku yao ya kwanza. Walikuwa wamekula matunda na kunywa soda kabla ya kuondoka Mahakama ya Milimani majira ya saa kumi na moja na nusu jioni. Katika gereza hilo, waliwekwa katika bweni Block G, sehemu ambayo mara nyingi hutumiwa kuhifadhi mahabusu na wafungwa mashuhuri. Walilala chumba kimoja na aliyekuwa Kamanda wa Kituo cha Polisi cha Nairobi Central, Samson Talaam, ambaye anakabiliwa na kesi ya mauaji ya mwalimu Albert Ojwang. Walikabidhiwa godoro, kitanda na blanketi kabla ya kufungiwa. Kwa Obado, hali hiyo ilikuwa na kejeli yake. Mnamo 2018 akiwa gavana, alitoa televisheni kwa Gereza la Industrial Area ili wafungwa waweze kufuatilia habari. Televisheni hiyo ndiyo iliyokuwa katika chumba alicholala usiku huo. Chumba hicho pia kiliwahi kutumiwa na aliyekuwa Mbunge wa Sirisia John Waluke na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu baada ya kupatikana na hatia katika kesi zao za ufisadi. Hii si mara ya kwanza kwa Obado na wenzake kufungwa katika Block G. Walikaa hapo Septemba 2018 walipokamatwa kwa mara ya kwanza kuhusiana na mauaji ya Sharon, kabla ya kuachiliwa kwa dhamana. Obado alikaa humo kwa siku 33. Baada ya kuhukumiwa, wafungwa hukabidhiwa rasmi kwa Huduma ya Magereza Kenya. Kwanza hupimwa afya, kisha hukabidhiwa sare mbili za gerezani huku nguo zao, simu, fedha, saa, vito na mali nyingine zikihifadhiwa hadi watakapoachiliwa. Afisa mmoja wa magereza alisema wafungwa hupangiwa sehemu ya kulala kulingana na kiwango cha hatari wanachoweza kusababisha na si hadhi yao. "Kanuni ni usawa. Wafungwa maarufu hawapaswi kupewa matibabu maalumu. Tunawapanga kulingana na kiwango cha hatari na hali zao," alisema. Maisha gerezani huanza saa kumi na mbili alfajiri kwa kuhesabiwa wafungwa. Hesabu hiyo hurudiwa mara kwa mara siku nzima. Kiamsha kinywa huwa uji iliyo na sukari kidogo. Baadaye wafungwa hukutana katika kikao kinachojulikana kama "bunge la wafungwa" kutoa malalamishi yao kabla ya kupangiwa kazi kama kupika, kulima au usafi. Chakula cha mchana huwa wali na maharagwe, ugali na maharagwe, ugali na mboga, ugali na nyama, githeri au viazi. Mlo wa mwisho hutolewa kati ya saa tisa na saa tisa na nusu alasiri, kisha wafungwa hurudishwa vyumbani kabla ya milango kufungwa saa kumi na mbili jioni. Familia zinaweza kutembelea wafungwa mara kwa mara, lakini kila ziara hudumu dakika zisizozidi 10 na husimamiwa na maafisa wa magereza. Simu hupigwa kupitia simu maalumu ya ustawi wa wafungwa, huku mazungumzo yakifanywa kwa Kiswahili au Kiingereza ili yaweze kufuatiliwa. Fedha pia haziwezi kukabidhiwa mfungwa moja kwa moja. Huwekwa kwenye akaunti yake kupitia ofisi ya ustawi, kisha hutumika kununua bidhaa katika duka la gereza. Afisa huyo alisema siku za kwanza gerezani huwa ngumu kwa wafungwa wengi kwani wengi hupitia mshtuko wa kisaikolojia. Kwa sababu hiyo, hupatiwa ushauri nasaha na maafisa wa ustawi pamoja na wafungwa waliopata mafunzo ya ushauri. Ingawa Obado alikuwa gavana aliyesimamia bajeti ya mabilioni ya pesa na misafara ya magari ya serikali, maisha yake sasa yatafuata ratiba sawa na ya maelfu ya wafungwa wengine: Kuamka alfajiri, kuhesabiwa mara kadhaa, kula chakula cha gharama nafuu, kufanya kazi anazopangiwa na kulala katika mabweni yenye wafungwa wengi huku akisubiri hukumu na rufaa yake.
"We aggregate wires to encourage regional discovery, sending readers directly back to the original source to explore full coverage."
This is a normalized overview of the breaking feed event. The complete, official release detailing all points, background context, and statements remains hosted by the original publisher.